Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya Majalada ya
Ardhi katika Ofisi za ardhi za jiji la Tanga mwishoni mwa wiki wakati wa
ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tanga.
Katikati ni Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga
Strawton Thobias.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na Mkuu wa Idara ya
Ardhi katika halmashauri ya Jiji la Tanga Strawton Thobias mwishoni mwa
wiki alipowasili katika jiji hilo wakati wa ziara yake ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya eneo lenye
mgogoro lililopo Mtaa wa Independence katikati ya jiji la Tanga wakati
wa kutembelea maeneo yenye mgogoro wa ardhi katika jiji hilo mwishoni
mwa wiki. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela na kushoto ni
mtoto wa mmiliki wa eneo hilo Paul Charles.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na
uongozi na watendaji wa sekta ya ardhi wilaya ya Pangani mkoani Tanga
mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta
ya ardhi mkoani Tanga. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya
Pangani Zainab Issa.
……………………
Na Munir Shemweta, WANMM TANGA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la
Tanga Daud Mayeji kupitia viwanja vyote vinavyodaiwa ni mali ya jiji
hilo lakini vinamilikiwa na watu wengine.
Hata hivyo, wakati Dkt Mabula
akitoa agizo hilo eneo maarufu la ufukwe katika jiji la Tanga la Bathing
Club lililopo Raskazone Tanga limerejeshwa kwa halmashauri ya jiji la
Tanga baada ya mmili wake kulitumia kwa muda mrefu.
Eneo hilo la ufukwe ambalo
wananchi walikuwa wakienda kwa kulipia limeelezwa kuwa ni moja ya maeneo
ambayo nyaraka zake zilikuwa zikioonesha linamilikiwa na Jiji la Tanga
lakini lilikuwa chini ya watu wengine.
Dkt Mabula aliagiza kupitiwa
kiwanja kimoja baada ya kingine na kuwataka wamiliki wake kwenda na
nyaraka zinazoonesha umiliki wa maeneo yao kama ni halali na kama ni
halali walipataje maana bado yanasomeka kama mali ya jiji la Tanga.
‘’ Ikibainika kuwa wamiliki
wake wanamiliki isivyo halali maeneo hayo basi mali hizo zote lazima
zirudi serikalini maana kumbukumbu zinaonesha maeneo hayo bado ni mali
ya jiji la Tanga’’ alisema Dkt Mabula.
Akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga
Martine Shighela wakati wa kutembelea baadhi ya maeneo hayo, Dkt Mabula
aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kwenda mtaa kwa mtaa,
kuyatambua maeneo husika na kupata nyaraka zinazoonesha umiliki wa
maeneo hayo kama ni halali na kama ni halali ifahamu yalipatikanaje
wakati hadi sasa kumbukumbu zinaonesha ni mali ya jiji la Tanga.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, agizo hilo ni kwa halmashauri zote
hasa katika yale maeneo yaliyotaifishwa na serikali na kuwa mali ya umma
lakini bado yanaendelea kumilikiwa na watu wengine huku wengine
waliouziwa maeneo wakishindwa kukamilisha malipo yao.
‘’ Kuna baadhi ya maeneo
serikali iliwarudishia wenyewe na mengine serikali ilipangisha kama
rasilimali zake lakini bado maeneo hayo yanamilikiwa na watu wengine.’’
alisema Naibu Waziri.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga
Daud Mayeji alimueleza Naibu Waziri kuwa katika jiji lake kuna maeneo
yanaoyoonesha kuwa yanamilikiwa na jiji lakini maeneo hayo bado
yanamilikiwa na watu wengine na jiji lake lilifanikiwa kurejeshewa eneo
la Bathing Club lililopo Raskazone.
Aidha Mayeji alisema jiji lake
linakabiliwa na chanagamoto ya baadhi ya maeneo yake kumilikiwa na
taasisi za serikali ambazo zimeshindwa kulipa fidia maeneo iliyotwaa kwa
wananchi.
Mkurugenzi wa Halamashauri ya
Wilaya ya Handeni William Makufwe alitaka kuwekwa kwa gharama halisi za
upimaji kwa kuwa hivi sasa kumekuwa na tofauti kubwa ya gharama za
upimaji jambo linalowafanya wanapotoa maagizo ya upimaji na kutaka
kutolewa muongozo wa gharama za upimaji, upangaji kwa nchi nzima ili
kuondoa sintofahamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Gracian Makota ameomba kupatiwa Afisa
Ardhi Mteule kwa kuwa anayewahudumia sasa kutoka Korogwe wakati mwingine
anashindwa kufanya hivyo kutokana na changamoto au geographia ya wilaya
ya Kilindi hasa pale inapotokea miundombinu kuharibika.
Wakati huo huo, Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu
watunza kumbukumbu wa Masijala ya Ardhi katika halmashauri za Jiji la
Tanga na ile wilaya ya Pangani mkoani Tanga kwa kushindwa kuzingatia
taratibu za utunzaji majalada ya ardhi jambo alilolieleza kuwa
linasababisha migogoro ya ardhi.
Akiwa katika ziara yake mkoani
Tanga, Dkt Mabula alibaini utunzaji wa kumbukumbu za Majalada ya ardhi
usiozingatia taratibu za utunzaji na kuagiza ofisi ya Ardhi Kanda ya
Kaskazini kuhaskikisha inatoa mafunzo kwa watunza kumbukumbu za Majalada
ya ardhi kwa halmashauri zote za mkoa mzima wa Tanga ili waweze kutunza
kumbukumbu vizuri.
0 comments:
Post a Comment