METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 27, 2017

UTAJIRI WA FIKRA NI KICHOCHEO KIKUBWA CHA MAENDELEO YA UCHUMI WA VIWANDA

Na Debora Charles

Itakumbukwa kuwa tangu Taifa la Tanzania limejipatia Uhuru wake, Maendeleo ya viwanda yamekuwa yakipewa kipaumbele na msukumo mkubwa katika Mipango ya vipindi mbalimbali, japo utekelezaji wake umekuwa ukitumia mikakati inayotofautiana kwa kuzingatia mfumo wa Sera za usimamizi wa uchumi.

Kabla ya Azimio la Arusha, Sekta ya Viwanda iliendelezwa na Sekta Binafsi na Serikali. Baada ya Azimio la Arusha Serikali ilitekeleza katika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ambapo shughuli zote kuu za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na viwanda zilianza kumilikiwa na kuendeshwa na Serikali. Aidha msisitizo huu ulikuwa KUJITEGEMEA ambapo viwanda vililenga kuzalisha bidhaa zinazotumika Kwa wingi nchini na hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje (Import Substitution).

Hata hivyo kuyumba kwa uchumi nchini na kuvunjika kwa Mfumo wa Kisoshalisti Duniani kuliifanya Tanzania kuachana na Mfumo wa Uchumi wa Ujamaa na Kujitegemea na badala yake kufungulia milango kwa wawekezaji binafsi na kuondoa vikwazo vya Biashara na Uwekezaji, Mfumo ambao mpaka sasa Taifa limeendelea kuutumia katika kukuza na kuendeleza Sekta ya viwanda nchini.

Hotuba aliyoitoa Mhe. Rais Dr. John Magufuli Bungeni 20 November, 2016 ilibainisha aina kuu tatu ya viwanda vinavyofikiriwa na Serikali ya Awamu ya Tano; viwanda vitakavyozalisha Ajira nyingi, viwanda vitakavyozalisha bidhaa nyingi na viwanda vitakavyozalisha bidhaa za kuuzwa nje.

Katika kuhusianisha Uchumi wa Viwanda na Ongezeko la Ajira, Prof. Honest Ngowi kupitia makala yake ya “Uelewa Juu ya Azma ya Uchumi wa Viwanda ni Muhimu kwa Mafanikio Yake” iliyotoka August 31, 2017 katika gazeti la Mwananchi aliwahi kuandika; Matamanio ya Serikali ni kuwa na viwanda vitakavyoajiri watu wengi. Ili hili litokee ni lazima kuelewa nadharia na kanuni za msingi za uchumi. Viwanda vya kuajiri watu wengi vitakuwa ni vile vinavyotumia nguvukazi kubwa kwa maana ya misuli badala ya mashine na mitambo.

Hivyo ili viwanda vya kutumia mitambo ya kisasa na mashine vizalishe ajira nyingi ni lazima kuimarisha na kuendeleza MNYORORO WA THAMANI. Lazima kuelewa vizuri na kuhakikisha kunakuwapo mwingiliano sahihi wa kisekta. Ni lazima sekta zote ziendelezwe ili kufanya sekta ya viwanda ipate malighafi, soko, mtaji hata wafanyakazi wengi na wenye ubora unaotakiwa, Alisema.

Kwa kufanya hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imefanya juhudi zake za hali na mali katika kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali wa Sekta hii nchini kama ambavyo baadhi yake imeainishwa hapo chini;

Ikiwa kikwazo kikubwa cha biashara ya Afrika ni ukosefu wa Miundombinu ya Usafiri. Hali ambayo inakadiriwa kuongeza gharama za biashara kwa asilimia 40 barani Afrika na kusababisha mchango wa Afrika kwenye biashara duniani kuwa chini ya asilimia 5. Serikali ya Awamu ya Tano ilizindua mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa ya Standard Gauge inayokadiriwa kutembea kwa speed 160 kwa saa na kubeba uzito mkubwa wenye mzigo wa takribani tani 1000 kupitia treni zitakazokuwa zikitumia Reli hiyo, ambayo ni sawa na Maroli ya Semitrela 500 yenye uwezo wa kubeba tani 20 kila moja.

Reli hii inakadiriwa kuongeza maradufu biashara ya nchi yetu na mataifa mengine, kuimarisha na kukuza sekta nyingine nchini, kuwezesha malighafi kusafirishwa kwenye maeneo ya viwanda, kuwezesha bidhaa zinazozalishwa viwandani kusafirishwa kwenye masoko husika kwa wakati na kwa haraka, kukuza sekta ya utalii, kusaidia kutunza barabara zetu na KUONGEZA AJIRA NYINGI KWA WATANZANIA WENGI.

Kadharika katika kuimarisha Sekta ya Usafiri wa Anga, Serikali ya Awamu ya Tano tayari imekwisha nunua ndege na imetenga kiasi cha Shilingi Bil 100 kwa ajili ya kuanza kukarabati viwanja katika mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa na Musoma. Katika kuinua Sekta ya Afya, Serikali imeongeza Bajeti ya madawa hospitalini kwa mwaka 2017 kutoka bil 31 hadi bil 250 ambapo bil 33 zimetumika kununua vitanda kwenye Mahospitali huku katika Sekta ya Elimu, Serikali imeweza kuanzisha Mfumo wa Elimu Bure kwa shule za msingi na Sekondari, kununua Vifaa vya Maabara kwa zaidi ya shule 1996 za Sayansi na kuongeza Shule za kidato cha tano na sita.

Kwa kuzingatia kuwa Sekta ya Kilimo ndio uti wa mgongo katika kukuza Uchumi wa Viwanda nchini Tanzania na kwamba sehemu kubwa (asilimia 80) ya watanzania ni wakulima, Serikali kupitia Bajeti yake ya 2017/18 imefuta tozo 80 zinazotokana na kilimo zikiwemo tozo zote za mbolea zilizokuwa zikitozwa na Tanzania Bureau of Standards (TBS), Tanzania Atomic Energy Commision (TAEC) na Weight and Measures Authority (WMA) wakati wa kununua na Tozo zote za viwango vya Ubora na Ukaguzi zilizokuwa zikitozwa na Tanzania Bureau of Standards (TBS). Kadharika tozo 7 zinazotokana na ufugaji na hata zile zilizokuwepo kwenye uvuvi nazo zimetolewa.

Baadhi ya Wataalamu wa masuala ya uchumi walikuwa wakiilalamikia Serikali kuwa ina Sera, Mipango na Mikakati mizuri ya kuendeleza viwanda lakini mipango hiyo imekuwa ikishindwa kutengewa fedha za kutosha kuitekeleza. Katika kuondoa kikwazo hiki, Serikali ya Awamu ya Tano imepitisha Bajeti ya Shilingi trillion 31.6 katika mwaka Mpya wa Bajeti 2017/2018. Ambapo fedha za Maendeleo zimeongezeka kutoka trillioni 11.8 kwa mwaka 2016/2017 hadi kufikia shilingi trillioni 11.9 kwa bajeti ya mwaka 2017/2018 ambapo ni sawa na wastani wa asilimia 38 ya bajeti yote.

Hata hivyo, Ili kuondokana na vikwazo vya Mifumo ya kifedha isiyo imara Serikali imeendelea kutoa rai kwa wafanyabiashara, wakulima na wawekezaji juu ya kutumia fedha za ndani katika kufanya mauzo na manunuzi ya bidhaa au malighali zinazozalishwa. Kutumia fedha za ndani zitaondoa hasara zinazotokana na kupanda na kushuka kwa thamani ya fedha za kigeni hususani Dola za Kimarekani jambo ambalo huathiri Maendeleo ya Sekta ya Viwanda nchini.

Shirika la Fedha Duniani- International Monetary Fund (IMF) limekuwa likieleza kuwa kwa sasa Dola ya Kimarekani ni fedha ambayo ipo katika wasiwasi wa kuporomoka.  Ni vyema wawekezaji na wafanyabiashara kubadili mfumo wa kuwekeza kwa kutumia fedha hizo na badala yake kuwekeza kwenye Mali (Assets) kwa sababu muda si mrefu pesa ya China inaweza kupanda na Dola ikashuka thamani.

Ikizingatiwa kuwa Kiswahili ndio lugha pekee ya kimataifa ambayo haina mahusiano na wakoloni hapa Afrika. Ni lazima Sera zetu ziongoze wawekezaji wanaoingia ndani ya nchi kutumia lugha ya Kiswahili ili kusaidia kuikuza na kusababisha mawasiliano kuwa rahisi hususani wakati wa uzalishaji kuwepo na maelewano baina ya wazawa na wenyeji.

Kitu chenye nguvu kubwa na uwezo wa kuamua hatma ya maisha yetu ni FIKRA. Huu ndio mtaji pekee kama Taifa, tunaweza kuutumia katika kuchochea Maendeleo yetu wenyewe. Lazima tutengeneze mazingira mazuri ya KUNAWIRISHA FIKRA zetu kupitia kujifunza kwa wenzetu waliofanikiwa. NI UTAJIRI WA FIKRA pekee ndiyo utatuwezesha kutambua thamani, umuhimu na faida za Rasilimali tulizo nazo na kuchokoza kiu ya mafanikio kwa mtu mmoja mmoja.

Kadharika Ushindi wa mapambano huletwa na matumizi ya silaha tulizonazo mikononi mwetu wenyewe. Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika kupitia kitabu chake cha Azimio la Arusha katika misingi ya Ujamaa na Kujitegemea; “Lakini ni dhahiri kwamba tumefanya makosa katika kuchagua silaha; kwani silaha tuliyoichagua ni fedha. Tunataka kuondoa unyonge wetu kwa kutumia silaha ya wenye nguvu, silaha ambayo sisi wenyewe hatuna”.

Tutumie UTAJIRI WA FIKRA zetu kujituma kufanya kazi kwa mikakati na malengo thabiti, kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora unaostahimili ushindani wa masoko ya nje, kubuni biashara sahihi kupitia mazingira wezeshi na rafiki yanayotengezwa na Serikali na mwisho KUZALISHA PESA zitakazokuwa chachu ya KUJILETEA MAENDELEO.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com