
Baadhi ya washiriki wa Kongamano
la Uwekezaji Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati alipofungua Kongamano hilo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Pwani mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha Mwongozo wa uwekezaji Mkoani Pwani
baada ya kuuzindua katika Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Pwani
alilolifungua kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mjini
Kibaha, Oktoba 19, 2019. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji), Angela Kairuki na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mhandisi Evarest Ndikilo.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizindua Mwongozo wa uwekezaji Mkoani Pwani katika Kongamano la
Uwekezaji Mkoani Pwani alilolifungua kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Pwani Mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019. Kulia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki na kushoto ni Mkuu
wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo.

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kongamano la
Uwekezaji Mkoa wa Pwani kwenye ukumbi wa Mkuu wa Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Pwani mjini Kibaha, Oktoba 19, 2019.

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest
Ndikilo wakitazama malighafi ya Pazolana inayotumika kutengeneza Saruji
wakati Waziri Mkuu alipotembelea banda la kampuni ya saruji ya Tanga
katika Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Pwani lililofunguliwa na Waziri
Mkuu kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani mjini Kibaha,
Oktoba 19, 2019. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Uwekezaji), Angela Kairuki na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa kampuni
hiyo, Mhandisi Benedict Lema.

Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Elibariki
Parsalam kuhusu utengenezaji wa chakula cha kuku wakati alipotembelea
banda la kampuni ya Hill Feeds katika Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa
Pwani alilolifungua kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Oktoba 19, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………….
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ameitaka mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo lake la kuandaa
makongamano ya uwekezaji ihakikishe inafanya hivyo mara moja.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumamosi, Oktoba 19, 2019) wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji kwa
mkoa wa Pwani katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza
viongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutekeleza agizo nililolitoa Juni 18,
2018 wakati wa kongamano la tatu la uwezeshaji wananchi kiuchumi la
kuhakikisha mikoa yote inaandaa kongamano la uwekezaji na inakuwa na
mwongozo wa uwekezaji wa mkoa. Mikoa ambayo haijatekeleza agizo hilo,
ifanye hivyo mara moja,” amesema.
Waziri Mkuu amesema mkoa huo
umeweza kubaini fursa zilizopo katika mkoa wa Pwani na kuzitangaza
kupitia mwongozo wa uwekezaji ambao pia ameuzindua leo.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo isemayo: ‘‘Ijenge
Tanzania, wekeza Pwani mahali sahihi kwa uwekezaji (Build Tanzania,
Invest in Pwani, the Best Place for Investment)” ina maana kuwa, licha
ya mkoa wa Pwani kubainisha na kutangaza fursa za uwekezaji na biashara
zilizopo, unajipambanua vizuri na kuonyesha kuwa ni kwa namna gani
umejiandaa na umetengeneza mazingira bora yanayovutia wawekezaji wa
ndani na nje.
“Ili kudhihirisha dhamira ya
dhati ya kukuza uchumi kupitia viwanda, nimeelezwa kuwa mkoa umetenga
hekta 53,016 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ambavyo vitatumia
rasilmali zilizopo ndani ya mkoa na maeneo mengine ya nchi kwa lengo la
kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wanachi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri wahakikishe wanasimamia miundombinu inayoelekea kwenye
viwanda vilivyopo kwenye maeneo yao.
“Kila mmoja ahakikishe maji,
umeme na barabara vinafika kila eneo ambalo mwekezaji anataka kujenga
kiwanda. Nitumie fursa hii kuwaomba mlete mabadiliko chanya yanayotokana
na maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano.”
Mapema, akimkaribisha Waziri
Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji), Bibi Angella Kairuki alisema kwamba Serikali
imeanza kutekeleza mapendekezo ya mpango wa kuboresha mazingira ya
biashara na uwekezaji nchini (Blueprint for Improving Business
Environment Regulatory Licensing in Tanzania) kwa kuondoa tozo 163
zilizokuwa zikilalamikiwa na wawekezaji.
“Pia tumetenganisha majukumu
ya TBS ya TFDA ambayo sasa ni TMDA. TBS itashughulika na vyakula na TMDA
itashughulika na dawa na vifaatiba. Vilevile, tumeondoa ada za usajili
sehemu za kazi ambazo zamani ilikuwa ni sh. 28,000 na sasa hivi
zinatolewa bure,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Mhandisi Evarist Ndikillo aliwataka watu wote wanaotaka kuwekeza nchini
waufikirie kwanza mkoa wa Pwani kwa sasabu uko kimkakati na una fursa
nyingi ikiwemo hali nzuri ya usalama na kwa maana hiyo mitaji yao
italindwa.
“Mkoa wetu uko kwenye eneo la
kimkakati la kuwezesha biashara kwa kuwa uko karibu na bandari ya Dar es
Salaam na uwanja wa ndege; uko karibu na soko kubwa ambalo ni Dar es
Salaam; unapitiwa na reli zote kwenda mikoani na nchi jirani; unapitiwa
na barabara kuu itokayo Dar es Salaam na pia una bandari kavu ya Kwala.”
Mbali ya hivyo, Mkuu huyo wa
Mkoa alisema faida nyingine ambayo mkoa huo unayo ni uwepo wa
miundombinu ya maji, umeme na nishati ya gesi asilia ambayo imeanza
kutumiwa na baadhi ya viwanda kama Goodwill na Lodhia Steel.
Naye Dkt. Tausi Kida,
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi ya Kijamii (ESRF) ambayo ilisimamia
uandaaji wa mwongozo wa uwekezaji kwa mkoa wa Pwani, alisema taasisi yao
inasaidia kuandaa na kuchambua fursa zilizopo kwenye mikoa mbalimbali.
“Hadi sasa tumekwishaisadia mikoa 17 kuandaa miongozo ya uwekezaji na
kwa sasa mikoa 12 imeshakamilisha na mikoa mitano iko kwenye hatua
mbalimbali,” alisema.
Akitoa taarifa kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela ambao ni wadhamini
wakuu, Afisa Mkuu wa Biashara, Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts alisema
benki hiyo imeendelea kugusa sekta zote za uchumi na hivyo kuongeza tija
kwenye mnyororo mzima wa uzalishaji.
Alisema huduma zao zimelenga
kuongeza tija na ufanisi katika sekta ya viwanda nchini ikiwemo utoaji
wa mikopo ya biashara kwa ajili ya kuongeza mikopo ya uendeshaji
(working capita loans) na mikopo ya uwekezaji (investment loans).
“Benki yetu inatoa mikopo ya
biashara na uwekezaji katika maeneo mbalimbali ambapo mikopo ya kilimo
ni shilingi bilioni 357, uzalishaji wa viwanda (shilingi bilioni 214),
biashara (shilingi bilioni 347), mahoteli (shilingi bilioni 87) na sekta
ya madini (shilingi bilioni 91),” alisema.
0 comments:
Post a Comment