
Na Nuru Ikupa, DSM
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo, amesema Tanzania inaungana na mataifa mbalimbali duniani katika
kuhakikisha kuwa dunia inakuwa ni mahala salama pa kuishi na ili kufiki
athma hiyo Tanzania inashirikiana na nchi nyingine duniani kuweka juhudi
za pamoja katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira na matumizi ya
kemikali hatarishi.
Naibu Waziri Nyongo alisema,
Tanzania imesaini Mkataba ujulikanao kama Minemata wenye lengo la
kudhibiti matumizi ya kemikali ya zebaki inayotumika kukamata dhahabu
kutokana na athari ya kemikali hiyo kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Alisema mkataba huo unawataka nchi
wanachama kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 matumizi ya zebaki katika
kukamata dhahabu yanafikia mwisho na njia mbadala inapatikana.
Nyongo aliyasema hayo jana tarehe
18 Oktoba, 2019 alipokuwa katika mahojiano ya moja kwa moja katika
studio za TBC Taifa jijini Dares Salaam alipoalikwa ili kuzungumzia
dhana ya usimamizi wa sekta ya madini wenye kuleta tija na manufaa kwa
jamii na taifa.
Nyongo aliendelea kusema zebaki
iliyopo sasa nchini itaendelea kutumiwa na wachimbaji wadogo wakati
huohuo Serikali ikiendelea na juhudi ya kupata teknolojia mbadala na
isiyokuwa na madhara kwa mazingira na wananchi itakayo wasaidia
wachimbaji wadogo katika uchenjuaji wa madini.
Amesema, serikali inafanya tafiti
mbalimbali ili kupata teknolojia mbadala ya uchenjuaji wa dhahabu na
pindi itakapopatikana Serikali kupitia vituo vya mfano vilivyopo nchini
itatoa elimu ya uchenjuaji kwa njia hiyo ili kuwawezesha wachimbaji
wadogo wa madini nchini kupata uelewa wa njia hiyo na hivyo kuachana na
matumizi ya zebaki.
Naibu Waziri Nyongo aliongeza kuwa
kutokana na utegemezi wa wachimbaji wadogo kwa kemikali hiyo,
haiwezekani kusimamisha matumizi yake kwa haraka kwani wengi hujikita
kwenye uchenjuaji kwa kutumia kemikali hiyo kunakowawezesha kujipatia
kipato na kutunza familia zao.
Aidha, amewaasa wachimbaji wadogo
kutumia kemikali hiyo kwa njia salama ili kuepusha athari zitokanazo na
kemikali hiyo. Amesema serikali ipo macho kuhakikisha inawaelimisha
wachimbaji wadogo namna bora ya matumizi ya kemikali hiyo ikiwa ni
pamoja na kuwashauri kutomwaga maji ya zebaki karibu na mito na makazi
ya watu ili kuepusha athari zake.
Pamoja na kuzungumzia suala hilo,
Naibu Waziri Nyongo alisema ili kuhakikisha kuwa madini yanatutoa
watanzania na kukuza uchumi wa nchi na wananchi sharti wafuate taratibu
na sheria za nchi.
“Chimba madini, uza madini yako
kwenye masoko ya madini, acha kuuza kwa njia za panya, sheria itachukua
mkondo wake, tutakukamata, tutataifisha madini, na utapata hasara”.
Alisisitiza.
“Ukipata madini lipa kodi lipa
tozo fedha hizo ziende kwenye mfuko wa Serikali, Serikali iwekeze kwenye
miradi mikubwa ya maendeleo, ijenge shule, ijenge hospitali na
barabara, ipende nchi yako. Ukichimba ukashindwa kulipa kodi umeisaliti
nchi yako umeusaliti uchumi wa nchi yako”. Alikazia.
Alimalizia mahojiano hayo kwa
kuueleza umma wa watanzania kuwa fasheni ya utoroshaji wa madini
imepitwa na wakati kwani serikali ina wigo na mkono mrefu hivyo hivyo
hakuna atakayejaribu kutorosha madini hayo atakayefanikiwa kwani
atakamatwa na atafilisika.
0 comments:
Post a Comment