
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia akiwasalimia wanafunzi wa shule ya Sekondari Bogwe wakati
alipowasili shuleni hapo kwa ajili ya mahafali ya 22 ya shule hiyo

Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa mahafali ya 22 ya
kidato cha nne katika shule ya sekondari Bogwe Kasulu Mkoani Kigoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akipata maelezo ya namna microscope
inavyofanya kazi kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari
Bogwe

Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akimtunuku cheti mhitimu wa kidato cha
nne katika shule ya sekondari Bogwe

Wanafunzi wa kidato cha nne shule
ta sekondari Bogwe wakifuatilia hotuba ya waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia (hayupo pichani)wakati wa mahafali ya 22 ya shule hiyo

Waziri wa Elimu, Saynsi na
Teknolojia prof. Joyce akiteta jambo na Mmoja wa wanafuzi wa kidato cha
nne Feodola Binigila anaesoma masomo ya jioni Bogwe sekondari mara baada
ya kumtunuku cheti cha ufaulu katika masomo.
……………….
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 14 kwa Kamishna wa Elimu
kuhakikisha anawasilisha mapendekezo ya namna ya kurekebisha waraka wa
elimu unaoruhusu mwanafunzi awe mtoro bila kutoa taarifa ndani ya siku
tisini.
Waziri Ndalichako ametoa agizo
hilo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya
Sekondari Bogwe iliyoko Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma ambapo
amesema waraka huo hauko sawa na wanafunzi wanautumia vibaya kwa
kutokwenda shule jambo linalowapelekea kukosa masomo.
Amesema ni lazima sasa kuwa na
mfumo ambao mwanafunzi anapokuwa haonekani shuleni ndani ya muda ambao
wataalamu wataona ni muafaka mzazi apate taarifa kwani taratibu zilizopo
sasa ni za kuwadekeza wanafunzi.
” Kama mwalimu asipofika shule
ndani ya siku tano amejifukuzisha kazi, iweje mwanafunzi siku
tisini?uwiano uko wapi? Kamishna hili jambo nimeshalizungumza na umeanza
kulifanyia kazi tangu mwezi wa saba. Muda ni mrefu nilizungumza katika
kikao cha Wizara.
Kamilisha kazi na watendaji acheni uzito, angalia kazi
ya Mhe. Rais na mimi Waziri wenu, twende pamoja vinginevyo utakaa
pembeni,” aliongeza Waziri Ndalichako.
Katika hatua nyingine, Waziri
Ndalichako amewataka wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya
Sekondari Bogwe kusoma kwa bidii ili kufuta historia ya matokeo mabaya
ya mitihani ya Taifa katika shule hiyo kwani Serikali imetumia fedha
nyingi kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya
shule nchini ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.
“Ukiangalia kwa mfano katika shule
yenu hii ya Bogwe Serikali imetoa shilingi milioni 378 ambazo zimejenga
miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukumbi ambao mnafanyia
mahafali sasa kazi iliyobaki kwenu ni nini? someni kwa bidii hamna cha
kulaumu Serikali imetelekeza kazi kwenu sasa,” aliongeza Waziri
Ndalichako.
Amewataka wanafunzi hao kuwa
mabalozi wazuri na mfano mzuri wa kuigwa mahali popote watakapokuwa ili
kuijengea sifa shule waliyosoma na kuwa wazalendo na Taifa ikiwa ni
pamoja na kuilinda nchi kwa gharama yoyote.
“Kamwe msikubali kutumika na watu
ambao wanataka kuvuruga amani, umoja na mshikamano katika Taifa hili,
Muasisi wa Taifa hili Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere alifanya kazi kubwa kujenga amani, mshikamano na umoja.
Tuendelee kumuenzi kwa kuhakikisha tunalinda tunu za Taifa
alizoziacha,’alisema Waziri Ndalichako.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya
Kasulu Kanali Simon Anange ametoa wito kwa wazazi kote nchini
kuzingatia malezi bora kwa watoto wao ili kutengeneza kizazi chenye
maadili kitakachosaidia katika ujenzi wa taifa.
Awali, akizungumza katika mahafali
hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bogwe David Kindanda alimweleza Waziri
Ndalichako shule imetekeleza mikakati ya kuinua kiwango cha taaluma
shuleni hapo akiahidi kuongeza bidii na mbinu za ufundishaji ili
kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao akisisitiza
kudhibiti utoro na kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike ambao amedai kuwa
bado hawafanyi vizuri.
“Pamoja na mikakati hiyo Mhe.
Waziri tunaomba sheria inayompa mwanafunzi nafasi kuwa mtoro kwa siku
tisini mfululizo ndio afukuzwe shule irekebishwe kama ulivyowahi
kusikika ukisema wazi. Sheria hiyo inahitaji marekebisho kwani
mwanafunzi hawezi kusomeshwa shule bure halafu kuwa mtoro wakati wapo
wanaotafuta fursa na wanaikosa,” alisema Mkuu wa shule ya Sekondari
Bogwe.
Akisoma risala ya wahitimu wa
Kidato cha nne Shule ya Sekondari Bogwe, mhitimu Faraji Joseph
ameishukuru Serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia huku wakiiomba kuwasaidia kupata maji shuleni hapo kwani kwa
sasa wanayafuata mto Bogwe jambo ambalo ni hatari kwa wanafunzi hasa
wakati wa vumbi la kiangazi.
0 comments:
Post a Comment