************************
Na. Idara ya Habari-NEC
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi kwa wananchi juu ya mazoezi mawili
tofauti yanayoendelea Nchini ya kuandikisha wapiga kura na
kuwatahadharisha kwamba Kadi ya Mpiga Kura inayotolewa na Tume
haitatumika kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwenzi
ujao.
Akizungumza
Jijini Dar es Salaam leo (10.10.2019), Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume,
Dkt. Wilson Mahera Charles amesema kwamba uandikishaji unaoendelea ambao
ulianza tarehe 08, Oktoba 2019 unahusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika tarehe 24 Novemba 2019 ambao hausimamiwi na Tume.
“Tume ya Taifa ya
Uchaguzi inapenda kuwataarifu wananchi kuwa uandikishaji unaofanyika
kuanzia tarehe 08, Oktoba 2019 hadi tarehe 14, Oktoba 2019 na kusimamiwa
na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI)
kupitia Halmashauri mbalimbali kote Nchini unahusika na uchaguzi wa
serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba 2019.
Mwananchi
asipojiandikisha hataweza kupiga kura katika uchaguzi huo,” amesema Dkt.
Mahera.
Aliongeza kwamba
mwananchi ambaye hatajiandikisha kwenye uandikishaji unaofanywa na
OR-TAMISEMI hatapata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za
Mitaa wa Novemba 24 mwaka huu, hata kama atakuwa na Kadi ya Mpiga Kura
inayotolewa na Tume na kwamba uchaguzi huo hausimamiwi na Tume bali
unasimamiwa na OR-TAMISEMI
Amewataka
wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo la
kujiandikisha ili wapaete fursa ya kuwachagua viongozi wa mitaa yao siku
hiyo ya tarehe 24 Novembe 2019.
Aidha, Dkt.
Mahera amesema kwamba Tume kwa mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ina jukumu la kuandikisha
Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.
“Uandikishaji
huo (wa OR-TAMISEMI) ni tofauti na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura unaofanywa na Tume kwenye mikoa mbalimbali Nchini.
Uboreshaji huu unahusu Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Madiwani wa Tanzania Bara utakaofanyika mwakani 2020,”
amesema.
Dkt. Mahera
ameeleza kwamba zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
linaendelea kwa sasa katika mikoa ya Tabora, Katavi na Halmashauri ya
Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ambako uboreshaji utafanyika kuanzia
tarehe 14 Oktoba hadi tarehe 20 Oktoba mwaka huu.
Ameongeza kwamba
zoezi hilo litaendelea kwenye mikoa ya Songwe, Dodoma na Singida kuanzia
tarehe 26 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba 2019.
“Wanaostahili
kujiandikisha ni wale ambao wana miaka 18 na wale ambao watafikisha
miaka 18 mwakani (2020) kabla ya uchaguzi, lakini pia zoezi linawahusu
wale ambao kadi zao zimeharibika au zimepotea ili wapate fursa tena ya
kuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alismema Dkt. Mahera.
0 comments:
Post a Comment