METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 25, 2019

Waziri wa Maji Asitisha Vibali vya Ujenzi wa Miradi kwa Wakandarasi kwa Kukosa Uadilifu


  
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wafanyakazi kutoka Kampuni ya Shanxi inayotekeleza Mradi wa Maji wa Tandangongoro katika Manispaa ya Lindi.
Ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Nandambi katika Manispaa ya Mji wa Lindi ukiwa umekamilika ambapo mradi wote utakapokamilika utagharimu jumla ya kiasi cha Shilingi milioni 825.
Wakazi wa Kijiji cha Kineng’ene wakiteka maji katika Mradi wa Maji wa Kineng’ene katika Manispaa ya Lindi.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nandambi na kuwahikikishia kuwa Serikali itatoa fedha ya kununua mabomba ya kusambaza maji ili kazi hiyo iliyobaki iweze kukamilika haraka iwezekanavyo na waanze kupata huduma ya maji.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akimuonyesha gharama za mabomba Mkandarasi wa Kampuni ya Canopy inayotekeleza Mradi wa Maji wa Ng’apa Vijijini. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Shaibu Ndemanga.
Mkandarasi akiendelea na kazi ya ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Tandangongoro katika Manispaa ya Lindi.
………………….
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema kuanzia sasa amesitisha kutoa vibali vya ujenzi wa miradi ya maji kwa wakandarasi kutokana na wengi wao kuwa wadanganyifu katika makadirio ya gharama za utekelezaji wa miradi hiyo na kuisababishia Serikali mzigo mkubwa na kukwama kwa miradi mingi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli imekuja akiwa ziarani mkoani Lindi akitembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maji katika Manispaa ya Mji wa Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo inaenda kwa kasi na kukamilika kwa wakati.
Profesa Mbarawa amesema baada ya kutembelea miradi mingi ya maji amegundua tabia ya wakandarasi wengi wasio waadilifu kuweka gharama kubwa ili kupata faida kubwa, na kumfanya kuchukua uamuzi wa kusitisha vibali vya ujenzi kwa wakandarasi na kutoa kazi hizo kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na Mamlaka za Maji.
Akifafanua kuwa maamuzi hayo yamelenga kukomesha tabia hiyo ya wizi wa fedha za Serikali na kuokoa fedha nyingi zinazoweza kutumika katika utekelezaji wa miradi katika maeneo mengine mengi na pia kuipa nafasi Serikali kukamilisha ujenzi wa miradi yake kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi na Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Halem Construction Co. Ltd wakae chini na kufikia makubaliano ya kuiacha Wizara ya Maji ifanye utaratibu wa manunuzi ya bomba za kusambaza maji kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Nandambi kwa dhumuni la kuhakikisha unakamilika kwa wakati kutokana na mkandarasi huyo kusuasua.
Profesa Mbarawa amesema fedha za ununuzi wa mabomba hayo zipo na ndani ya wiki mbili mabomba yatakuwa yamefika site kwa ajili ya kukamilisha mradi huo unaotakiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Septemba, 2019 kwa gharama ya Shilingi milioni 825.
Aidha, wakazi wa Kijiji cha Nandambi wamweleza Waziri wa Maji, Prof. Mbarawa kuwa hatua hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwao ikizingatiwa kuwa mradi huo ulioanza utekelezaji wake Agosti, 2018 na unatakiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019 bado mkandarasi hatoi matumaini ya kukamilisha mradi huo kwa asilimia 100 pamoja na ujenzi wa tenki kuwa umekamilika.
Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa Mkoa ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema Serikali ya Mkoa wa Lindi itahakikisha mazungumzo hayo yanafanyika pasipo kupoteza muda ili hatua iliyobaki ikamilike na wananchi wa Nandambi wanufaike na maji.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com