******************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka vijana na jamii kwa ujumla wasikwepe jukumu la
kuwatunza wazee kwa sababu nguvu zao za uzalishaji mali zimepungua
kutokana na kazi waliyoifanya wakiwa vijana kwa ajili ya maendeleo na
ustawi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa
Kutokomeza Mauaji ya Wazee uliozinduliwa Januari, 2019 ili kwa
kutokomeza ukatili kwa wazee ifikapo 2023 na kuhakikisha wazee na watu
wenye ulemavu wanatambuliwa na kulindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu,
ukatili na mila potofu.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 29, 2019) wakati akizindua kambi
ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee na watu wenye ulemavu katika
viwanja vya Kichanganimjini Iringa. Kambi hiyo imeandaliwa na Mbunge wa
Viti Maalumu, Dkt. Ritta Kabati katika kuadhimisha siku ya Wazee
Duniani.
Amesema
wajibu wa kuwahudumia au kuwasaidia wazee na watu wenye ulemavu ni wa
kila mmoja na wanapaswa watambue kwamba wazee hao wamelitumikia Taifa
kwa muda mrefu tena kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaletea na
kuhakikisha wanapata mafanikio hayo ambayo wanajivunia sasa.
“Kwa msingi
huo, tunao wajibu wa kuwajali wazee wetu kwa hali na mali ikiwa ni
sehemu ya matunda ya uwajibikaji wao kwetu na kwa Taifa kwa ujumla.
Hivyo basi, tutumie vema Kambi hii kuwasaidia wazee wetu na watu wenye
ulemavu kwa kutambua afya zao na kuwapatia matibabu ya kiafaya ili
waendelee kuwa salama na wenye furaha nasi tuvune busara zao.”
Kutokana na
umuhimu wa kuwatunza wazee na kuwasaidia watu wenye ulemavu, Waziri Mkuu
ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wananchi na wadau
mbalimbali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa fursa, haki na ustawi wa
wazee ikiwemo kuondokana kabisa na vitendo vya ukatili dhidi yao.
“Vituo vyote
vya kutoa huduma za afya vya umma kutoa huduma bora na za haraka kwa
wazee wetu wenye vitambulisho. Tengeni dirisha maalumu kwa ajili ya
kuwahudumia ili wasikae kwenye foleni muda mrefu. Serikali itaendelea
kuweka miundombinu na mazingira rafiki ili kuwawezesha kupata mahitaji
yao.”
Kadhalika, Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia maelekezo yake kwa
Halmashauri zote nchini kuwatambua wazee wasiojiweza na kuwapatia
vitambulisho vya matibabu bila malipo. “Namshukuru Mbunge wa Viti Maalum
Ritha Kabati amebainisha mafanikio yanayoendelea kupatikana kutokana na
utekelezaji wa agizo hilo.
“Haidhuru
nasi tukiiga mfano wa Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalumu na
kaka yangu Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu kwa moyo wao wa
kizalendo kabisa kuona kuna haja ya kusaidia na kuunga mkono juhudi za
Rais wetu mpendwa Dkt. John Magufuli za kuwahudumia wanyonge.”
Hata hivyo,
Waziri Mkuu ameendelea kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha
zoezi hilo linakuwa endelevu kwa kuwatambua na kuwapatia vitambulisho
wazee wote nchini wasio na uwezo ili waweze kunufaika na huduma ya
matibabu bila malipo pamoja na huduma zingine za kijamii.
Vilevile,
Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Novemba 2019 nchi inatarajia kufanya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wazee kama sehemu ya jamii wana haki ya
kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuchagua viongozi wanaoona watafaa
kuwaongoza na wao kuchaguliwa kuongoza katika nafasi mbalimbali. Hivyo
wasaidiwe kushiriki zoezi hilo.
Kwa upande
wake, Waziri Mkuu Mstaafu na Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa
Iringa, Peter Pinda alimpongeza Dkt. Ritta kwa uamuzi wake wa kuandaa
kambi hiyo ambayo itatoa fursa kwa wazee kupima afya zao na kupatiwa
huduma pamoja na kutoa viungo bandia kwa baadhi ya walemavu.
“Uzee ni hali
siyokwepeka upende usipende ila unaweza kucheleweshwa kutegemea na aina
ya matunzo wanayopatiwa. Nashauri wazee wapate vyakula bora tena kwa
uwiano sahihi, vyakula hivyo ni pamoja na vya jamii ya mizizi, mikunde,
nafaka, mbogamboga na nyama ili waweze kuimarisha afya zao.”
Awali, Waziri
Mkuu alipokea taariza za ujenzi wa jengo la Ustawi wa Jamii Manispaa ya
Iringa lilojengwa kwa ufadhili wa Mkurugenzi wa Kundi la Makampuni ya
Asas, Salim Abri kwa gharama ya sh. milioni 60.
Kwa upande
wake,Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Iringa Tiniel Mmbaga alisema
kukamilika kwa jengo hilo kutawawezesha kutoa huduma bora kwa jamii na
kwa wakati kwani awali maafisa watano walikuwa wakilundikana katika
chumba kimoja hali iliyosababisha wateja kushindwa kueleza matatizo yao
baada ya kukosekana kwa usiri.
Alisema kwa
siku wanashughulikia malalamiko yahusuyo masuala ya migogoro ya familia
ikiwemo matunzo ya watoto kuanzia 15 hadi 30 pamoja na wanawake zaidi ya
50 ambao kila mwezi wanakwenda kuchukua fedha kwa ajili ya matunzo ya
watoto zinazotolewa na wenza wao kufuatia kuwepo kwa migogoro baina yao.
Shughuli
hiyo, imehudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine
Mahiga, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI Josephat
Kandege, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira
na wenye UlemavuStela Ikupa pamoja na Maafisa wengine wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment