
************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) afuatilie sababu za mikoa ya Tanga na Njombe
kutotekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na
mazao ya misitu.
Amesema makampuni yanayonunua
nguzo lazima yahakikishe yanazingatia sheria ya nchi ikiwemo ulipaji wa
kodi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kampuni zote zilizonunua nguzo
bila ya kulipa kodi zifuatiliwe na zilipe kodi yote waliyoikwepa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati alipotembelea kiwanda cha
kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya kilichoko Mafinga wilayani
Mufindi akiwa katika siku ya tatu za ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.
“Naibu Waziri TAMISEMI hakikisha
unakwenda mkoani Njombe na uaanze kuzungumza na mkuu wa mkoa, tunataka
kujua kwa nini hawajaanza kutekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya
ushuru unaotokana na mazao ya misitu hali iliyosababisha wanunuzi
kumbilia huko na kuacha kununua mazao hao katika mkoa wa Iringa.”
“Tunataka tujue ni nani huyo
anayewakataza wasilipe kodi na tuangalie anamahusiano gani na viongozi
wa mkoa huo. Ukaangalie makampuni hayo yanamahusiano gani na viongozi
hao hadi wasilipe kodi na tutajua kama kampuni hizi ni zao au za ndugu
zao.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
itahakikisha inawabana wafanyabiashara wote walionunua nguzo kwenye
mikoa hiyo ambao hajalipa asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya
misitu ili waweze kulipa kiasi chote walichokikwepa..
Amesema Serikali inahitaji kodi
kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na haoni sababu ya mikoa hiyo
kushindwa kutoza kodi iliyowekwa kwa mujibu wa sheria. Kitendo cha mikoa
hiyo kutotoza kodi hakikubaliki na wafanyabiashara wote waliochukua
nguzo bila ya kulipa kodi hiyo watalipa kodi yote kuanzia walipioanza
kuchukua nguzo.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imeweka mikakati ya wafanyabiashara wafanye biashara zao katika
mazingira bora na kwa kuzingatia sheria za nchi na pia Rais Dkt. John
Magufuli amezuia nguzo zote za umeme kuagizwa kutoka nje ili kuwawezesha
wafanuyabiashara wa ndani kuuza nguzo pamoja na wananchi kupata ajira.
“Hata tulipokuwa tunanunua nguzo
kutoka nje zilikuwa zinatoka hukuhuku na walichokuwa wakifanya ni
kuzichukua huku na kuzipeleka nchi jirani na kuziweka kwa wiki kisha
wanabadilisha vibao na kuzirudisha tena nchini.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Ally Happi alimweleza Waziri Mkuu kwamba wateja wa mazao ya misiti
wameanza kupungua na kwenda mikoa ya Tanga na Njombe kwa kuwa katika
mikoa hiyo haijaanza kutekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru
unaotokana na mazao ya misitu, hivyo ameiomba Serikali iwasaidie.
Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda
cha kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya, Benedicto Mahenda alisema
kiwanda hicho kilianzishwa 2007 kwa ajili ya uchakataji wa mbao na 2016
kilianza kuzalisha nguzo za umeme wakiwa na mtambo wenye kuzalisha nguzo
100 kwa siku. Kiwanda kimeajiri watumishi 350.
Meneja huyo alisema katika
kuitikia wito wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga uchumi kupitia sekta ya
viwanda, walifanya mabadiliko kwa kujenga kiwanda kikubwa na cha kisasa
cha kuzalisha nguzo za umeme chenye uwezo wa kuzalisha nguzo 1,500 kwa
siku.
Alisema malighafi za kiwanda hicho
wanazipata kutoka katika shamba la miti la Sao Hill lililoko chini ya
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na kwenye mashamba ya wakulima wadogo.
Soko kubwa la bidhaa zao ni TANESCO kupitia utekelezaji wa miradi ya
REA.
Pia, Meneja huyo alimshukuru Rais
Dkt. Magufuli kwa uamuzi wake wa kuzuia nguzo zisitoke tena nje ya nchi
na kutumia nguzo zinazozalishwa na viwanda vya ndani. “Tunamshukuru sana
Mheshimiwa Rais kwa kutuamini na kututia moyo wawekezaji wa ndani na
kutuonyesha soko la kuuza bidhaa zetu.”
0 comments:
Post a Comment