
*Waziri Mkuu asema inalenga kuvutia wanunuzi wa ndani na nje ya nchi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
katika msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu ambao unatarajiwa kuanza
hivi karibuni, Serikali imepanga kuimarisha mifumo ya ununuzi wa zao
hilo ili kuvutia wanunuzi wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.
Pia, Waziri Mkuu amesema
Serikaliitatoa nafasi ya kwanza ya ununuzi kwa wenye viwanda nchini,
hivyo amewataka waandae mahitaji yao na kuyawasilisha kwenye mamlaka
husika ili wawe na uhakika wa kupata malighafi ya kutosheleza mahitaji
ya viwanda vyao.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge
la 11, Bungeni jijini Dodoma. Amesema wakulima wataarifiwa kuhusu
utaratibu wa uuzaji wa zao hilo kwenye kikao cha wadau kitakachofanyika
hivi karibuni.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga
kupanua soko la korosho kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya
kutengeneza bidhaa nyingine zitokanazo na korosho zikiwemo siagi,
maziwa, mvinyo na sharubati pamoja na kuendelea kujenga maghala ya mfano
na yenye viwango kwa ajili ya kuhifadhia korosho katika maeneo ya
kimkakati.
Ili kuhakikisha mpango huo
unatekelezwa, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara na
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha zinasimamia upatikanaji wa
masoko mapya ya mazao mbalimbali.
Amesema Wizara hizo, zinapaswa
kuzingatia maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Dkt. John Magufuli,
alipokutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi. Pia
taasisi zinazohusika na utafutaji wa masoko ikiwemo Soko la Bidhaa
(TMX), TanTrade na Bodi zote za Mazao zijielekeze katika kutafuta masoko
ya mazao yanayozalishwa nchini.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika
msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 224,964 za korosho ghafi zenye thamani
ya sh. bilioni 729.90 zilikusanywa. Kati yake tani 222,825 zilikusanywa
na Serikali. “Korosho zilizolipwa ni tani 197,547 na Serikali
inakamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha tani 25,278. Hivi sasa,
korosho yote imenunuliwa na inasafirishwa. Aidha, baada ya zoezi hilo
Bodi ya Mazao Mchanganyiko itarudi kulipa madeni yaliyobaki kwa wakulima
na wenye maghala.”
Akizungumzia ununuzi wa zao la pamba,
Waziri Mkuu amesema mgogoro wa kibiashara kati ya mataifa makubwa
umesababisha kuporomoka kwa bei ya pamba katika soko la dunia kinyume na
matarajio kuwa bei ingeongezeka.
“Ili kukabiliana na hali hiyo,
Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusimamia makubaliano kati
ya Benki Kuu na Benki zilizotoa mikopo kwa makampuni yanayonunua pamba
kulingana na mitaji yao ili kununua pamba yote kwa wakati.”
Waziri Mkuu ametaja hatua nyingine
kuwa ni pamoja na kuhamasisha kampuni hizo zipeleke fedha za malipo ya
wakulima, kudhibiti udanganyifu kupitia mizani, kusimamia malipo ya
wakulima na makato ya pembejeo katika maeneo yaliyobainika kutokea kwa
vitendo hivyo.
Kuhusu zao la tumbaku, Waziri Mkuu
amesema hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2019 mauzo ya tumbaku ya mkataba
yalikuwa yamekamilika, huku jumla ya kilo milioni 60.59 zenye thamani ya
Dola za Marekani milioni 92.79 ilinunuliwa. Kiasi hicho, ni sawa na
asilimia 105.7 ya lengo la kuzalisha kilo milioni 57.31 za tumbaku ya
mkataba.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema
tathmini ya masoko imeonesha uwepo wa tumbaku ya ziada kiasi cha kilo
milioni 12.22 ambayo ilizalishwa nje ya mkataba katika maeneo
mbalimbali. “Serikali inaendelea na majadiliano na makampuni ya ununuzi
kwa lengo la kuhakikisha tumbaku yote inanunuliwa.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza
Wizara ya Kilimo ihakikishe inawasimamia ipasavyo mawakala waliopewa
jukumu la kusambaza pembejeo kwa wakulima ili ziwafikie wakulima kwa
wakati na kwa bei inayohimilika na ubora unaohitajika.
Amesema katika kipindi cha kuanzia
Septemba 2019 maeneo mengi nchini huanza kupata mvua za vuli ambazo ni
ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo, hivyo Serikali lazima
ihakikishe wakulima wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora,
mbolea na viuatilifu kwa ajili ya msimu huu mpya wa kilimo.
Waziri Mkuu amesema hali ya uzalishaji
wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa toshelevu. “Kwa mfano,
katika msimu wa kilimo wa 2018/2019 uzalishaji ulifikia takriban tani
milioni 16.41 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.84.”
Amesema hivi sasa wafanyabiashara wa
mazao ya chakula wanaendelea kusafirisha na kuuza mazao hayo ndani na
nje ya nchi. “Serikali inawahimiza wananchi wote wahifadhi chakula cha
kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani hususan wakati huu tunapoingia
kwenye msimu mpya wa kilimo kwa mwaka 2019/2020.”
0 comments:
Post a Comment