*******************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja
ya alama ili kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, hivyo
itaendelea kusimamia uendelezaji, usanifu na urasimishaji wa Lugha ya
Alama ya Tanzania, ambao ameuzindua leo(Jumamosi, Septemba 28, 2019).
Amesema hatua
hiyo itawezesha utoaji wa elimu katika ngazi mbalimbali pamoja na
kuboresha mawasiliano katika jamii na tayari imetoa mafunzo ya lugha
hiyo awamu ya kwanza kwa walimu 82 wa shule za Sekondari nchini na
kwamba zoezi hilo ni endelevu.
Ameyasema
hayo leo (Jumamosi, Septemba 28, 2019) wakati akihutubia wananchi
kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani katika Uwanja wa
Kichangani – Kihesa, wilayani Iringaakiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani Iringa.
Kaulimbiu ya siku
ya Viziwi Duniani kwa mwaka huu inasema “Haki ya Matumizi ya Lugha ya
Alama kwa wote”. Kaulimbiu hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya mawasiliano
miongoni mwa Watanzania ambao ni Viziwi.
“Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kurasimisha Lugha ya
Tanzania, kutayarisha vifaa vya kufundishia Lugha ya Alama ya Tanzania
na kufundisha walimu katika shule za Msingi na Sekondari nchini.
Mchakato huo utachukua muda wa takribani miaka miwili kukamilika.”
Amesema
Serikali itahakikisha kuwa lugha ya alama ya Tanzania inatambulika na
kutumika kikamilifu kama chombo cha mawasiliano miongoni mwa Viziwi
nchini ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa
Taifa lao.
Waziri Mkuu
ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli imedhamiria na inatekeleza kwa dhati jitihada za kutoa
kipaumbele kwa Watanzania wanyonge ambao hawakuwa wakinufaika ipasavyo
na rasilimali za nchi.
“Serikali
yenu sikivu inatambua vikwazo vya aina hiyo na inatekeleza maelekezo ya
Ilani ya CCM ya 2015/2020, ambayo inaielekeza Serikali ihakikishe watu
wenye ulemavu wanapata elimu kwa kupata vifaa maalumu na kushiriki
katika shughuli za kijamii.”
Hivyo, Waziri
Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwekeza kwenye
miundombinu na mazingira rafiki yatakayowawezesha watu wenye ulemavu
kwenda wanapotaka, kutumia vyombo vya usafiri na kupata habari kama
walivyo wengine. Amesema katika ofisi yake ataajiri mkalimani wa lugha
za alama.
Amesema
Serikali itaendelea kuboresha mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu kwa
kuwawezesha kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi kwa kutumia lugha ya
alama, alama mguso, maandishi ya nukta nundu, maandishi yaliyokuzwa au
njia nyingine zinazofaa.
Waziri Mkuu
amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza
kurasimisha Lugha ya Tanzania, kutayarisha vifaa vya kufundishia Lugha
ya Alama ya Tanzania na kufundisha walimu katika shule za Msingi na
Sekondari nchini. Mchakato huo utachukua takribani miaka miwili
kukamilika.
“Serikali kwa
kutambua umuhimu wa kuwa na shule maalumu ya Serikali ambayo inahudumia
watoto wenye mahitaji maalumu imeanza ujenzi wa Shule Maalumu Patandi
katika Mkoa wa Arusha. Shule hiyo inatarajiwa kuchukua wanafunzi 600 wa
Msingi na Sekondari na itagharimu sh. bilioni 2.8.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema katika mapitio ya Kanuni za Maudhui ya Vyombo vya
Habari, Kanuni za mwaka 2011, Serikali imeingiza kipengele kipya
kinachovitaka vyombo vyote vya habari kuwa na wakalimani wa lugha ya
alama kwa vipindi muhimu. Baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo Shirika la
Habari Tanzania (TBC) vimekuwa vikitekeleza agizo hilo.
“Napenda
kutumia maadhimisho haya kuagiza vyombo vyote vya habari kuhakikisha
kwamba agizo hili linatekelezwa ipasavyo. Serikali kwa upande wake
itaendelea kuhakikisha kuwa haki na mahitaji ya Watu wenye Ulemavu
vinapatiwa ufumbuzi kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Watu wenye
Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010.”
Amesema
anajua ajua changamoto wanazokumbana nazo viziwi wanapotaka kupata
huduma mbali mbali katika vituo vya kutolea huduma za afya, mahakama,
vituo vya polisi, nyumba za ibada na maeneo mengine muhimu kwa kuwa
hayana wakalimani wa lugha ya alama.
Waziri Mkuu
ametoa wito kwa taasisi zote za Serikali na binafsi zihakikishe zinakuwa
na wakalimani wa lugha ya alama. “Pia naagiza kwamba mitaala ya vyuo
vya Afya, Polisi, Mahakama na vinginevyo ihakikishe inazingatia kuongeza
kozi ya Lugha ya Alama kama somo la lazima. Hii itasaidia kuzalisha
watalaamu wa lugha ya alama ambao wataweza kuwahudumia wenzetu viziwi
ipasavyo.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Nidrosy
Mlawa ameishukuru
Serikali kwa kuwaamini watu wenye ulemavu na kuwateuwa kushika nafasi
mbalimbali za uongozi, lakini waomba iongeze nafasi za ajira kwa watu
wenye ulemavu ili nao waweze kujikwamua kiuchumi na kusaidia Taifa.
Pia, ameiomba
Serikali iwe na wakalimani wa lugha za alama kwa ajili ya kuwawezesha
watu wenye ulemavu waweze kupata taarifa zinazolewa na viongozi wao.
Wameomba Serikali ikamilishe mchakato wa urasimishaji wa Lugha ya Alama
ya Tanzania. WaziriMkuu amesemamaombi na mapendekezo yao ni ya msingi na
muhimu kwa maisha ya Viziwi. Lengo la Serikali ni kuboresha huduma zetu
kwa Viziwi hapa nchini.
Maadhimisho
hayo yamehudhuliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI
Josephat Kandege, Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana,
Ajira na wenye UlemavuStela Ikupa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu pamoja na viongozi wa
CHAVITA.
0 comments:
Post a Comment