METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, December 2, 2018

PAMOJA FOUNDATION YAZINDUA HOSTEL YA WASICHANA KWA SHULE ZA SERIKALI



Na Mwandishi wetu

Katika kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu kwa ufanisi zaidi taasisi ya Pamoja Foundation kwa ufadhili wa taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation imezindua hostel kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa shule za serikali.

Uzinduzi wa hostel hiyo  uliogharimu jumla ya shilingi milioni 50 umefanywa leo na Diwani wa Kata ya Tuangoma   Mohamed Suleiman kwa niaba ya Mbunge wa jimbo la Mbagala Ally Mangungu katika eneo la Mzinga wilaya ya  Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hostel hiyo, Diwani wa Kata ya Tuangoma  Selemani amepongeza ubunifu uliofanywa na  taasisi ya Pamoja foundation kwa kuanzisha mradi wa kusaidia wasichana hasa katika masuala ya elimu na kuzitaka taasisi nyingine kushirikiana katika kusaidia masuala ya elimu ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.

Aidha, aliwaasa wananchi wengine kuiga mfano wa mwananchi wa eneo la Mzinga kwa kutoa eneo la wakfu  kwa ajili ya kujengwa hostel  hiyo ambapo alisema uamuzi huo utawezesha kujenga hostel nyingi  na kubainisha kuwa  eneo la Tuangoma  ulipo mradi wa viwanja 20000 yeye kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo la Mbagala ataangalia namna ya kupata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa hostel kwa kuwa katika mradi huo kuna maeneo yametengwa kwa ajili ya shule.

Diwani huyo wa kata ya Tuangoma alizishauri taasisi nyingine kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi  wanaoshindwa  kuendelea na masomo katika fani mbalimbali katika eneo la uchumi  ili baadaye nao waweze kusaidia watu wengine.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Pamoja Foundation Haji Mrisho alisema hostel iliyozinduliwa  yenye uwezo wa kuwatunza wanafunzi 40 itajulikana pia kama Kituo cha Kuendeleza Wanafunzi ni  kwa ajili ya wanafunzi wa shule za serikali.

Kwa mujibu wa Mrisho, uamuzi wa kuanzisha hostel hiyo unatokana na  utafiti uliofanywa na taasisi yake katika wilaya za Ilala, Temeke na Kigamboni kuonesha wanafunzi wanaoishi shule za bweni wanafanya vizuri  ukilinganisha na na wale wa shule za kutwa.

Mkurugenzi huyo wa Pamoja Foundation alisema, kiwanja ilipojengwa hostel ni kiwanja kilichotolewa wakfu na kubainisha bila msaada huo ingekuwa vigumu  kuamilisha mradi huo  lengo kuunga mkono juhudi za ardhisetikali elimu bure na kuhamiasisha  kuunga mkono Serikali kwa kuwa wadau wanaweza kusaidia aidha kwa maabara, hostel ama madarasa.

Alisema Taasisi yake imeanzisha hosteli hiyo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano kutoa elimu bure na mwakani taasisi hiyo inatarajia kuanzisha hostel ya wavulana sambamba kuwa na kituo cha mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha watakaoshindwa kuendelea na masomo katika viwango tofauti kupata taaluma zitakazowasiadia kimaisha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Pamoja Foundation, mbali na makazi wanafunzi watakaoishi katika hostel hizo watapatiwa elimu,vifaa mbalimbali vya  kujisomea pamoja na mpango wa afya ili wasihangaike katika masuala ya elimu.

Mrisho alibainisha kuwa, awali taasisi ya Pamoja Foundation ilikuwa na  mpango wa kupanga jengo kwa ajili ya hostel lakini kupatikana kwa jengo la kudumu kumewapa faraja kubwa kwa kuwa sasa wamepata mradi wa kudumu.

Mrisho alisema, lengo Ia uanzishwaji hostel ya wasichana kwa wanafunzi wa shule za Serikali ni kuwawezesha kusoma vizuri hasa ikizingatiwa watoto wa kike wamekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo majukumu mengi wanapokuwa majumbani ukilinganisha  wavulana.

Mlezi wa Kituo cha Malezi cha Ibnu Jazar kilichopo Vikundi Picha ya Ndege Dar es Salaam Mfaki Mohamed alishauri wasichana watakaopata fursa ya kukaa katika hosteli hiyo kutunzwa vyema ikiwa ni pamoja na wale watakaokuwa na jukumu la kuwalea kuzungumza  nao katika  njia iliyo bora na  kuachana na ile dhana ya kuona kuwa viboko  kama  njia pekee ya kuwalea  wasichana ama wanafunzi na kusisitiza ulelewaji  mzuri kwa wasichana basi kutaepusha mzozo.

Kwa mujibu wa Mfaki kwa sasa kuna adui  mazingira  kwa wasichana ambapo kumekuwa na vishawishi vinavyorudisha nyuma wasichana hasa katika masuala ya maadili na kushauri  njia bora ya kukabiliana na hali hiyo ni kuwandaa  wasichana  kimaadili ili kuepukana vishawishi  mbalimbali kwa wale watakaopata fursa katika  hosteli hiyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com