****************
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amevitaka vyama vya msingi vya ushirika mkoani Rukwa kuhakikisha
wanalipa madeni wanayodaiwa na wadau wa kilimo ikiwemo mabenki pamoja
na wauzaji mbalimbali wa pembejeo ili wadau hao waweze kuendeleza
uaminifu na hatimae kuwa na mahusiano mazuri yatakayoleta maendeleo ya
wananchi katika mkoa.
Amesema kuwa kutolipa madeni chama
kinajiweka katika mazingira ya kutokopesheka na wadau kukosa uaminifu
hata kwa vyama vingine na kunasababisha wadau hao kushindwa kufikisha
huduma kwa wakulima na hatimae kilimo kukosa tija, vyama vya ushirika
kuyumba na kuongeza kuwa dawa pekee ya kukopa ni kulipa.
“ Vyama vya Msingi vina madeni
tena madeni makubwa, kwa mfanokuna kile chama cha Katazi AMCOS pamoja na
Rukwa Farmers vyote vipo kule Wilaya ya Kalambo vinadaiwa shilingi
milioni 395, vyama viwili sijajua kwengine lakini pale Mpui wanadaiwa
Shilingi Milioni 485 au 490, lakini wao wamejipanga nilikuta mzigo
mkubwa sana wa mahindi, tani zaidi ya 600, na waliniambia deni
wanamaliza, lakini vile vyama viwili hata mahindi yaliyoko kwenye
maghala yalikuwa hayazidi magunia 250 sasa watalipaje deni, ukiuliza
wanasema kwamba hawakupata mavuno ya kutosha, lakini nje ya hapo
wanauza” Alieleza.
Hivyo alitoa rai kwa vyama vya
ushirika kuliangalia jambo hilo kwa karibu kwa kuchambua vyama vyote
vinavyodaiwa, wadau wanaowadai, siku waliyokopa na siku wanayotakiwa
kurudisha mikopo, aina ya mikopo, walichorejesha tangu kukopa ili kuwa
na orodha kamili na kuwafuatilia katika urejeshaji wa mikopo hiyo kwani
kwa kufanya hivyo watajenga Imani kwa wanaowakopesha na hatimae
kukopesha zaidi.
Mh. Wangabo aliyasema hayo
alipokuwa akifungua mkutano wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ufipa
Cooperative Union Ltd (UCU) katika mkutano uliowajumuisha wadau wa
kilimo katika mkoa ili kuona namna ya kuinua kilimo chenye tija pamoja
na kuhuisha ushirika ndani ya mkoa.
Aidha, Wakati akiwasilisha mada
yake kwa wakulima Meneja wa Benki ya Manedeleo ya Kilimo Tanzania (TADB)
Kanda ya Nyanda za juu Kusini Dickson Pangamawe alisema kuwa viongozi
wa shirika ndio nguzo ya wanaushirika, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha
kuwa wanachama wanafaidika na ushirika huo na kuhakikisha kuwa mikopo
wanayoipata inawafikia wakulima wao.
“ Nyinyi ndio mtakaotujengea
uamini kule kwa wakulima, sisi kama benki ya kilimo tuna fursa ya mikopo
ya aina zote, kama wakulima wapo ‘serious’ na uongozi wao utasimama
imara, tutawakopesha wataweza kufanya shughuli zao za kilimo bila ya
shida yoyote, kwahiyo nitoe rai kwa viongozi wa ushirika, mara nyingi
kumekuwa na shida na wakulima wanashindwa kuwa waaminifu kwasababu
wanashindwa kusimamiana vyema katika vyama vyao, kwahiyo nyie muwe imara
ili kuturuhusu sisi tuweze kuwawezesha,” Alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda wa
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Sumbawanga Abdillahi
Nyangasa alishauri kuwa ili wakulima waweze kujikomboa alitaja mambo
matatu makubwa ikiwemo Fedha, Masoko na Mkulima mwenyewe na kuongeza
kuwa wao kama NFRA wanasimama katika kumhakikishia mkulima masoko na
hivyo wakulima wanahitaji fedha za mikopo kutoka katika mabenki na wao
kuwa tayari kutumia fedha hizo kwaajili ya manufaa ya kilimo chao.
“Mtazamo wa NFRA ni kuwafanya Wana
Rukwa na Watanzania wengine tubadilike tuwe na uwezo wa kuuza bidhaa
zetu za mazao ndani na nje ya nchi, bahati nzuri mkoa umeshaweza
kulichukua hili na kulifanyia mkakati kwa maana ya ndugu zetu maafisa
ugani, kazi ianzie shambani, tuna kiwango kikubwa sana tunachokipoteza
cha mahindi tunayolima kwa hatua ya mwisho ya ubora, asilimia 30 mpaka
40 wakati mwingine mazao yanaharibika kwasababu ya kutozingatia kilimo
chenye tija,” Alisitiza.
Mkoa wa Rukwa una matrekta 124
yanayomilikiwa na wakulima binafsi hali iliyopelekea Mh. Wangabo
kuvitaka vyama vya ushirika kusimamia kauli mbiu yao ya “ Ushirika,
Pamoja tujenge uchumi” kwa kuanza na kumiliki matrekta ili kuwawezesha
wanachama wao waweze kulima kwa tija na kuongeza mazao na sio kutegemea
kilimo cha majembe au kutumia wanyama.
0 comments:
Post a Comment