Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiangalia pamba iliyochambuliwa
na kufungwa kwenye robota katika kiwanda cha kuchambua pamba cha
Alliance Ginneries Ltd, wakati wa ziara ya viongozi wa mkoa huo ya
kukagua mwenendo wa ununuzi wa pamba, iliyofanyika Septemba 08, 2019.
Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa
Pamba nchini , Bw. Boaz Ogola ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha
kuchambua pamba cha Alliance Ginneries Limited kilichopo Bariadi Mkoani
Simiyu, akimweleza jambo viongozi wa Mkoa huo walipotembeelea kiwandani
hapo kwa lengo la kujionea namna kiwanda hicho kinavyonunua pamba kutoka
kwa wakulima katika ziara iliyofanyika Septemba 08, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka akiangalia pamba iliyochambuliwa na kufungwa kwenye robota
katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginneries Ltd, wakati
wa ziara ya viongozi wa mkoa huo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa
pamba, iliyofanyika Septemba 08, 2019.
*******************
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amewakikishia wakulima wa pamba mkoani Simiyu kuwa
Serikali itahakikisha mwezi huu wa Septemba pamba yote inanunuliwa kwa
bei elekezi ya shilingi 1200 kwa kilo na wakulima kulipwa fedha zao,
ambapo amesema hadi sasa zaidi ya kilo milioni 54 zenye thamani ya
shilingi bilioni 65.1 zimenunuliwa na wakulima wamelipwa fedha zao.
Mtaka ameyasema hayo wakati wa
ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu katika vyama vya ushirika vya
msingi (AMCOS) na Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginneries
Limited wilayani Bariadi, iliyofanyika Septemba 08, 2019 kwa lengo la
kujionea mwenendo wa ununuzi wa pamba, ambapo amewataka wanunuzi kutumia
fedha walizopewa dhamana na Serikali kwa ajili ya kununua pamba
zitumike kuwalipa wananchi badala ya kuzielekeza mahali pengine au
kufanya tofauti na makubaliano.
Amesema makisio ya mkoa ya
mavuno yalikuwa ni kuvuna kilo milioni 180 ambapo hadi sasa pamba
iliyokusanywa ni kilo milioni 132.7 ambayo thamani yake ni shilingi
bilioni 159.3 na kati ya hizo kilo milioni 54.2 zenye thamani ya
shilingi bilioni 65.1 zimelipiwa na ambazo bado hazijalipiwa ni kilo
milioni 78.5 ambayo thamani yake ni zaidi ya shilingi milioni 94.2.
Ameongeza kuwa kuelekea katika
kipindi cha mvua za vuli Mtaka ni vema wakulima kutoa pamba majumbani na
kupeleka kwenye vyama vya ushirika ili iweze kununuliwa na kutunzwa
mahali salama, huku akitoa wito pia kwa wanunuzi kujielekeza kwenye
maeneo ambayo ni magumu kufikika kipindi cha mvua na maeneo ambayo
maghala yake si salama sana.
Aidha, Mtaka amewakata viongozi wa
vyama vya ushirika kuwa waadilifu badala ya kushirikiana na machinga
kuwanyonya wakulima kwa kuuza pamba chini ya bei elekezi ya shilingi
1200 na kuwataka wanunuzi kununua pamba kwa mujibu wa utaratibu kwa kuwa
watakaobainika kufanya umachinga watachukuliwa hatua na pamba hiyo
itapigwa mnada kama ilivyofanyika hivi karibuni Wilayani Bariadi.
“Ujumbe huu uwafikie wanunuzi wote
wa pamba wanaokuja kununua pamba Simiyu , pamba itanunuliwa kwenye
vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS)kwa bei elekezi ya shilingi 1200
kwa kilo, pamba haitanunuliwa kienyeji kwenye nyumba za watu usiku wa
manane kwa bei ndogo, atakayekamatwa asije akalaumu vyombo vya
sheria”alisema Mtaka.
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Enock
Yakobo amewataka wanunuzi wa pamba mkoani Simiyu kuhakikisha kuwa
wanawalipa wakulima fedha zao kwa wakati ili waweze kujikimu na mahitaji
yao na kujiandaa na msimu ujao wa kilimo.
Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa
Pamba nchini, Bw. Boaz Ogola amesema Serikali imewahakikishia wanunuzi
wote kuwa itakuwa tayari kufidia hasara itakayopatikana endapo watapata
hasara wakiuza kwenye soko la dunia baada ya kununua pamba kwa shilingi
1200, hivyo mwenendo wa ununuzi wa pamba nchini ni mzuri ambapo hadi
tarehe 01/09/2019 kilo milioni 210 zimeshanunuliwa nchi nzima.
Kwa upande wao Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif
Shelakaghe wamesema pamba inaendelea kununuliwa katika maeneo yao huku
wakisema wataendelea kusimamia na kuhakikisha pamba inanunuliwa kwa
kufuata utaratibu uliowekwa na wananchi wanapata fedha zao.
Awali wakulima wamesema kuwa
baadhi ya makampuni ya ununuzi pamba hayajawalipa fedha zao hivyo
wakaomba Serikali kuwasaidia kuongea na wanunuzi wa zao hilo ili fedha
zao zipatikane kwa wakati waweze kununua chakula na mahitaji mengine na
kujiandaa na msimu ujao.
“Sisi tunaitegemea pamba na
hapa kuna makampuni tunawadai fedha zetu tunaiomba serikali itusaidie
tupate fedha zetu tuna mambo mengi ya kufanya,tunataka tununue chakula
kabla bei haijapanda sasa hivi kila mara bei ya mahindi inapanda”alisema
Charles Ng’andwe kutoka Kijiji cha Ibulyu Bariadi.
0 comments:
Post a Comment