Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga, akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani)
Na
Mwandishi Wetu
KAMPUNI
ya UTT AMIS inayomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango,
imeanzisha huduma mpya ya Mfuko wa Hati Fungani ‘Bond Fund’ ili kuiwezesha
jamii iweze kuzifikia fursa za uwekezaji na kujikomboa kiuchumi.
Kuanzishwa
kwa mfuko huo kumeongeza idadi ya mifuko na kufikia sita yote ikisimamiwa na
kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 2013
ikichukua jukumu ya usimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja kutoka kwa
Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT).
Akiuzungumzia mfuko huo, Mkurugenzi wa Masoko na
Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga, alisema utatoa fursa kwa wawekezaji
wadogo, wakati kuzifikia fursa za uwekezaji zilizokuwa zikifikiwa na wawekezaji
wachache, wakubwa.
Alifafanua kuwa, baadhi ya bidhaa hizo zinaeleweka
kirahisi ambapo namna ya kuzifikia, kuwekeza ni rahisi lakini wakati mwingine
hazitoi faida shindani kwa wawekezaji.
Alisema mfuko huo utaondoa changamoto
ambazo huwakuta wawekezaji kwenye soko la fedha ambalo lina bidhaa nyingi
zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya watumiaji.
“Mbali
ya Mfuko wa Hati Fungani, UTT AMIS inasimamia mifuko mingine ya uwekezajiambayo
ni Mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha,
Watoto, Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi.
“Kuanzishwa kwa Mfuko
wa Hati Fungani kumetokana na mahitaji ya wawekezaji pamoja na uchambuzi wa
bidhaa za kifedha zilizoko kwenye soko la mitaji kwa sasa,” alisema.
Mbaga
alisema mfuko huo utawekeza kwenye hati fungani zilizoorodheshwa katika soko la
hisa kwa asilimia 90, asilimia 10 itakuwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.
Lengo
ni kuwawezesha wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha kutokana na uwekezaji wao waweze
kufanya hivyo, kumfanya mwekezaji achague kama anapenda kukuza mtaji au kupokea
gawio kila mwezi, kila miezi sita kulingana na hitaji lake.
Alisema kampuni hiyo pia inatoa huduma ya usimamizi
wa mali za kifedha ili kukidhi mahitaji maalum kwa wawekezaji binafsi wa kipato
cha kati, cha juu na taasisi.
Aliongeza
kuwa, baadhi ya wawekezaji hasa wadogo ni vigumu kuwekeza katika baadhi ya
bidhaa kwenye soko la fedha, Mfuko wa Hati Fungani umeratibiwa ili kuondoa
changamoto hizo.
“Mwekezaji
anapata faida sawa na wawekezaji wakubwa, akihitaji fedha anauza baadhi ya
umiliki wake kwenye mfuko kwa utaratibu rahisi bila kupoteza faida aliyoipata.
“Mfuko
pia unawafaa wawekezaji wakubwa kwani ina faida shindani, gharama ndogo za
kuwekeza, ukwasi wa kutosha, usalama wa mtaji, hatari ndogo za uwekezaji,”
alifafanua.
Alisema
mfuko huo hutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza, kushiriki katika masoko ya
mitaji, kufaidika na uwekezaji huo, umeanzishwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji
wa kipato cha chini, kati na kipato cha juu.
Mbaga
alisema watu binafsi, kampuni, taasisi, vikundi rasmi wanaweza kushiriki katika
uwekezaji kwenye mfuko huo, lengo ni kuwafanya wawekezaji wawe na ushiriki
mpana kupitia uwekezaji wa vipande, kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba
kupitia hati fungani na masoko ya fedha.
Mfuko
huo unatoa fursa ya uwekezaji rahisi wa muda mrefu kwa wawekezaji wanaopenda kuwekeza
ili kukuza mtaji, kupata gawio kila mwezi au baada ya miezi sita kama
anavyohitaji.
“Kimsingi
Mfuko wa Hati Fungani una mipango miwili ya uwekezaji ili kukidhi matakwa
tofauti ya wawekezaji, kuna mpango wa kukuza mtaji, gawio kila mwezi na gawio
kila baada ya miezi sita.
“Mpango wa kukuza mtaji, gawio la mara kwa mara
halitatolewa kwa wawekezaji badala yake faida iliyopatikana itarudishwa kwenye
uwekezaji wa awali kwa kununua vipande vitakavyonunuliwa kwa bei ya wakati huo.
“Mpango
huo utawafaa wawekezaji wanaohitaji kuweka akiba kwa malengo maalum mfano
kujenga nyumba au wafanyakazi wenye kipato na wangependa kuwa na fedha ya akiba
kama dharura itatokea au kwa matumizi ya baadae wanaweza kuchagua mpango wa
kukuza mtaji,” alisema.
Mbaga
alifafanua kuwa, wawekezaji katika mpango huo wanaweza kuuza kiasi chochote cha
uwekezaji kama watakidhi vigezo ya mfuko vinavyohusu uuzwaji wa vipande.
Mpango wa gawio kila mwezi hutokana na mahitaji
ya kifedha ya mwekezaji na anavyochagua kwenye fomu ya maombi ya kuwekeza
kwenye mfuko.
Wawekezaji
ambao wanahitaji kuchukua faida kila mwezi mfano wastaafu wanaopata fedha zao
za mkupuo, kuwekeza kwenye mfuko wanashauriwa kupokea gawio kila mwezi ili
wapate kipato cha kuishi bila kupoteza fedha walizopata.
Mbaga
alisema wawekezaji wengine wanaopata fedha nyingi kwa mara moja mfano wachimba
madini wadogo, wanaweza kuchagua kupata gawio kila mwezi ili waweze kuendesha
shughuli zao bila kuathiri mtaji walioupata.
Pia
wawekezaji watakaojiunga na mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vyote ili
mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko vinavyohusu uuzwaji wa vipande vya mfuko.
Wawekezaji
wanaopata fedha nyingi kwa msimu kama wakulima wa mazao mbalimbali, wanaweza
kuchagua gawio la kila miezi sita ili waweze kupata fedha wakati wa kuandaa
mashamba yao, kulima na kuvuna ili waweze kuendesha shughuli zao, kufuata msimu
bila kupoteza mtaji.
Akizungumzia
gharama za kuwekeza, Mbaga alisema hakuna gharama yeyote wakati wa kujiunga au
kujitoa kwenye Mfuko wa Hati Funganui, wawekezaji wataruhusiwa kununua, kuuza
vipande kwa thamani halisi ya kipande itakayokuwepo.
“Wawekezaji
wote wa ndani na nje ya Tanzania kama Sheria ya Soko la Mitaji na Dhamana
inavyoruhusu, wanaweza kuwekeza kwenye mfuko huu,” alifafanua.
Kuhusu ununuzi wa vipande, alisema vinaweza
kununuliwa siku yoyote ya kazi isipokuwa kipindi cha kufunga vitabu ambacho
hakitazidi siku saba za kazi.
Alisema
kuanzia Septemba 16, mwaka huu hadi Oktoba 16, mwaka huu, itakuwa kipindi cha
mauzo ya awali hivyo ni vizuri Watanzania wakachangamkia fursa hiyo.
Kiwango
cha chini kitakuwa sh. 50,000 na thamani halisi ya kipande itakuwa sh. 100
ambapo maombi ya kununua vipande yanaweza kuwakilishwa katika tawi lolote la
Benki ya CRDB; ofisi za madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es
Salaam; Ofisi za Shirika la Posta au Wakala yoyote atakayeteuliwa na UTT AMIS.
“Uwekezaji
katika mfuko huu kwa wawekezaji walio nje ya Tanzania, awasiliane na ofisi za
madalali waliosajiliwa wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au ofisi za UTT AMIS
ili kupata taarifa na muongozo zaidi.
Anaongeza
kuwa, thamani ya mwanzo ya kipande itakuwa sh.
100. Thamani ya kuuza na kununua kipande itakuwa sawa na thamani halisi
ya kipande bila gharama yoyote.
Kiwango
cha chini kitakuwa sh. 50,000 na hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu, hiyo ni
fursa kwa kila Mtanzania ambapo baada ya muda wa mauzo ya awali, mwekezaji
anaweza kuwekeza kuanzia sh. 5000, mara nyingi kadri awezavyo.
Malipo ya mauzo ya vipande yanaweza kufanywa kwa
fedha taslimu au hundi ya benki itakayolipwa kwenye akaunti ya Mfuko wa Hati
Fungani iliyopo Benki ya CRDB.
“Wawekezaji wanaweza kwenda kwenye tawi lolote la
Benki ya CRDB na kufanya malipo. Pia malipo yanaweza kufanyika kwa kupitia M-Pesa,
Tigo Pesa, Airtel Money,” alisema.
Mbaga alisema kiwango
cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa Kukuza Mtaji ni
vipande 500. Kwa kuwa thamani ya mwanzo ya kipande ni sh. 100, thamani ya chini
ya vipande, mauzo itakuwa sh. 50,000.
Kuhusu
mpango wa gawio kila mwezi, kiwango cha chini cha uwekezaji wakati wa mauzo ya
mwanzo kwa mpango wa gawio kila mwezi ni vipande 100,000, thamani ya mwanzo ya
kipande sh. 100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh.
10,000,000.
Mpango wa gawio kila miezi sita, kiwango cha chini cha uwekezaji
wakati wa mauzo ya mwanzo kwa Mpango wa gawio kila miezi sita ni vipande
50,000, thamani ya mwanzo kwa kipande sh.
100, thamani ya chini ya vipande katika mauzo itakuwa sh. 5,000,000.
Alitoa
wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi akiwahimiza wawe sehemu ya
uwekezaji katika mfuko huo mpya kwani una faida nyingi, hawapaswi kuwa na hofu.
0 comments:
Post a Comment