Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa darasa la saba kutoka katika Kata ya Lamadi wilayani Busega Septemba 09, 2019 katika Shule ya Msingi Mwabasabi kwa niaba ya wenzao wa Mkoa wa Simiyu, kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani wa Taifa wanaotarajia kufanya kuanzia Septemba 11-12, 2019.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Njiginya akitoa taarifa ya Ufaulu ya wanafunzi wa darasa la saba katika Halmashauri wakati Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa darasa la saba kata ya Lamadi Septemba 09, 2019 katika Shule ya Msingi Mwabasabi kwa niaba ya wenzao wa Mkoa wa Simiyu, kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani wa Taifa wanaotarajia kufanya kuanzia Septemba 11-12, 2019.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba katika kata ya Lamadi wilayani Busega Mkoani Simiyu wakiwa wamenyoosha mikono yao kama ishara ya kuwa tayari kujibu swali waliloulizwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati akizungumza nao Septemba 09, 2019 katika Shule ya Msingi Mwabasabi kwa niaba ya wenzao wa Mkoa wa Simiyu, kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani wa Taifa wanaotarajia kufanya kuanzia Septemba 11-12, 2019.
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Kuelekea
katika Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu elimu ya Msingi Darasa la saba Septemba
11-12, 2019 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewaonya wanafunzi wa
darasa la saba mkoani hapa kujiepusha na udanganyifu katika mtihani
huo badala yake wazingatie waliyofundishwa na kufanya mtihani huo
kwa utulivu na kujiamini.
Mtaka ameyasema hayo Septemba 09, 2019 wakati
akizungumza na wanafunzi wa darasa la saba kutoka katika Kata ya Lamadi
wilayani Busega Septemba 09, 2019 katika Shule ya Msingi Mwabasabi, kwa niaba
ya wenzao wa Mkoa wa Simiyu, kwa lengo la kuwatakia heri katika mtihani
wa Taifa wanaotarajia kuufanya kuanzia Septemba 11-12, 2019.
Mtaka amesema anaamini walimu wamefanya kazi yao
vizuri ya kuwafundisha na kuwaandaa wanafunzi hao hivyo ni vema wakafanya
mtihani huo wakiwa na ujasiri huku wakipuuza taarifa zozote za kuwepo kwa
majibu ya mitihani mahali popote.
“Ninawatakia kila la heri kwenye mtihani wenu,
nashukuru kwa kazi nzuri iliyofanywa na walimu katika kuwafundisha na kuwaandaa
kwa kutoa majaribio ya mara kwa mara, kambi kambi za kitaaluma; niwaombe
mkaufanye mtihani huu kwa utulivu na ujasiri; asiwadanganye mtu kuwa kuna
majibu ya mtihani au mtihani umevuja sehemu fuulani, mkazingatie
mlichofundishwa” alisema Mtaka.
Katika hatua nyingine Mtaka amewashukuru walimu kwa
namna wanavyojituma katika kuwafundisha wanafunzi na kutoa wito kwa walimu hao
kuanzisha madarasa ya maandalizi ya kidato cha kwanza (pre- form one) kwa
wanafunzi hao wanaohitimu ili wasaidie kuwaandaa wanafunzi hao na masomo
ya kidato cha kwanza na waweze kupata kipato cha ziada kupitia malipo
yatakayotolewa na wazazi watakaokuwa tayari kugharamia masomo hayo.
Kwa upande wake Afisa Taaluma Mkoa wa Simiyu , Mwl.
Onesmo Simime amesema Mkoa wa Simiyu uliweka mikakati mbalimbali ya maandalizi
ya wanafunzi wa darasa la saba ikiwemo walimu kumaliza mada zote mwezi Juni
2019 na kuwepo kwa kambi za kitaaluma kwa kila shule, hivyo wanafunzi
wameandaliwa vizuri na kwa mikakati hiyo matarajio ya mkoa ni ufaulu kuongezeka
zaidi ya mwaka jana 2018.
Akizungumza
kwa niaba ya walimu, Mwalimu Beatrice Ernest kutoka Shule ya Msingi Mwabasabi
amesema wana uhakika na maandalizi waliyofanya kwa wanafunzi wao hivyo
ufaulu utaongezeka, huku akimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwaruhusu
kuanzisha vituo vya ‘pre-form one’ na kuahidi kuwa walimu watajiunga kuanzisha
madarasa hayo ili kuboresha taaluma ya wanafunzi wao na kuboresha vipato vyao.
Nao baadhi ya
wanafunzi wakizungumza kwa niaba ya wenzao wamesema wamejiandaa vizuri na
wamejipanga kufanya vizuri ili waweze kutimiza malengo yao ikiwa ni
pamoja na kujiunga na elimu ya sekondari na hatimaye kuendelea na elimu
juu ili waweze kufikia ndoto zao.
“Mimi na
wenzangu wote tumejiandaa vizuri nina uhakika tutafanya vizuri na wote tutaenda
sekondari, ushauri tuliopewa na Mkuu wa Mkoa tutauzingatia naamini tutashinda
tu” Eric Malimi kutoka Shule ya Msingi Lamadi.
“Sisi
tumejiandaa vizuri na tunaweza kuendelea mbali kimasomo, tunamshukuru Mkuu wa
Mkoa kwa kutupa mawaidha na tutayatekeleza ili tuweze kufaulu mtihani wa Taifa
na tufikie tunapotaka” alisema Glorymary Samwel kutoka Shule ya Msingi
Itongo.
Mkoa wa
Simiyu una jumla ya wanafunzi 29,248 wa darasa la saba wanaotarajia
kufanya mtihani wa Taifa Septemba 11-12, mwaka huu, ambao kati yao
wavulana ni 13, 594 na wasichana 15.654.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment