Waziri wa Nishati, Dkt.Medard
Kalemani,( kushoto) akizungumza na wanakijiji wa Kijiji cha Makanga(
hawapo pichani) mara baada ya kuwasha umeme wa REA Awamu ya tatu
mzunguko wa kwanza, kulia anayeshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga ,
Ngolo Malenya.
Baadhi ya wanakijiji wa Idunda
wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alipofika kijijini
hapo kuwasha umeme wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard
Kalemani, akipeana mikono na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Idunda
wilayani Ulanga mkoani Morogoro mara baada ya kuwapa kifaa cha Umeme
Tayari ( UMETA).
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard
Kalemani ( kushoto) na akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo
Malenya,Waziri alifika wilayani hapo kuwasha umeme na kukagua
utekelezaji wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza.
Baadhi ya akina mama wa kijiji
cha Makanga wakifurahia jambo, wakati Waziri wa Nishati ,Dkt.Medard
Kalemani ( hayupo pichani)akizungumza kuhusu kuwasha umeme wa REA awamu
ya tatu mzunguko wa kwanza katika kijiji chao.
………………………………………………..
Na Zuena Msuya, Morogoro,
Waziri wa Nishati Dkt. Medard
Kalemani, ameagiza Afisa aliyekuwa akisimimamia Mradi wa Umeme Vijijini
(REA), Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Seif Abdallah, aondolewe kwenye
nafasi hiyo kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Aidha Dkt. Kalemani ametoa siku
20, kwa Kampuni ya Ukandarasi ya State Grid inayotekeleza mradi huo
kuwasha umeme katika vijiji vya Wilaya ya Ulanga la sivyo atakatwa
asilimia kumi ya malipo yake kutokana na kazi hiyo.
Dkt.Kalemani alitoa kauli hiyo
Agosti 31,2019, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya
utekelezaji wa mradi wa REA na kuwasha umeme katika Vijiji vya Makanga
na Idunda wilayani Ulanga, mkoani Morogoro.
Waziri wa Nishati alifikia hatua
hiyo baada ya kutoridhishwa na usimamizi unaofanywa na mhandisi huyo
kutoka Wakala wa Nishati Vijiji ( REA) pamoja na utekelezaji wa mradi
usioridhisha.
“Huyu Mhandisi Seif Abdallah,
utendaji wake wa kazi hauridhishi kabisa, hayupo katika maeneo ya kazi
yanayotekelezwa mradi, anamuacha mkandarasi afanye kazi anavyojitakia
yeye mwenyewe hakuna usimamizi wowote, ninamuagiza Mkurugenzi wa REA
amuondoe huyu mhandisi hafai kuwa msimamizi”,alisisitiza Dkt.Kalemani.
Katika hatua nyingine,
Dkt.Kalemani alitoa siku 20 kuanzia, Septemba 1 hadi 20, 2019 kwa
kampuni ya ukarandari ya State Grid kuwasha umeme katika vitongoji vinne
kabla ya kukamilisha Mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza
unaotarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu nchini kote.
Alifafanua kuwa, utekelezaji
wa Mradi wa REA awamu ya tatu umegawanyika katika mizunguko miwili
ambayo ni mzunguko wa kwanza ulioanza kutekelezwa mwezi Juni, 2019 na
utakamilika Desemba mwaka huu.
Aidha mzunguko wa pili wa REA
awamu ya tatu unatarajiwa kuanza mwezi Januari na kukamilika mwezi Juni
,2020, hivyo alimtaka kila mkandarasi aliyepew kazi ya kutekeleza mradi
huo ahakikishe anakamilisha mzunguko wa kwanza wa kazi yake kwa mujibu
wa makubaliano ya mikataba na sheria.
Alisisitiza kuwa haridhishwi na
hatua ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Morogoro ambao mpaka
sasa umefikia asilimia 56 tu ya utekelezaji wake ambao hauendani na kasi
ya utekelezaji wa mradi huo.
Sambamba na hilo alimtaka
mkandarasi huyo,kuongeza nguvu kazi ya makundi ya vijana ili kuharakisha
shughuli za utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa
kwanza kama ilivyoelekezwa katika mkataba wa kazi hiyo.
“Sitakubali kukwamishwa na ninyi
State Grid katika utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa mnafanya kazi kwa
kusuasua sana kasi yenu hairidhishi kabisa, na nyie ndiyo mko nyuma
kabisa katika kasi ya kutekeleza mradi wa huu REA awamu ya tatu,
mzunguko wa kwanza ikilinganishwa na wakandarasi wote wanaotekeleza
miradi hii nchini, kama hamtatimiza makubaliano ya mkataba, tutawakata
asilimia 10 ya malipo yenu”, alisema Dk.Kalemani.
Hata hivyo, Dkt.Kalemani alirejea
kauli yake ya kuwataka wananchi kuwa wasinunue miundombinu ya umeme
kama vile nguzo, pamoja Luku kwa kuwa vifaa hivyo vinatolewa bure kwa
kila mwananchi aliyepitiwa mradi wa umeme vijijini.
Pia aliwataka wananchi
kutumia umeme kwa faida kama vile kuongeza thamani ya mazao kwa kufanya
usindikaji wa mazao yao ili kujiletea maendeleo zaidi.
Serikali imetenga shilingi
Bilioni 42 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko
wa kwanza kwa Mkoa wa Morogoro.
0 comments:
Post a Comment