
Na.Alex Sonna,Dodoma
CHAMA cha Mapinduzi(CCM), kimewataka wenyeviti wa mashina na mabalozi kutopanga foleni wanapofika kwenye ofisi za serikali.
Kauli hiyo aliitolewa jana jijini
hapa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Taifa, Dk. Bashiru Ally, wakati wa
uzindua wa gazeti la ‘Uhuru ya kijani’ ambalo linalenga kujenga na
kuimarisha chama hicho.
Alisema kuwa mabalozi hawana kizuizi hata kwenye kugombea wao hawaitwi na hawazuiliwi wanaweza kugombea hata urais.
“Mwenyekiti wa shina au balozi
akipiga simu au kupiga hodi sehemu yeyote zilipo ofisi za viongozi wa
serikali naomba asipange foleni,”alisema.
Aidha, Dk. Bashiru alieleza kuwa,
wamepanga kuwapatia vitambulisho viongozi hao kwa sababu ndio njia
pekee ya kutambua mchango wao kwa kuwa, viongozi hao katika ngazi ya
chini ya chama wamekuwa wakijitolea Zaidi kuliko wanachama wengine.
“Chama chetu kitaendelezwa kwa
njia ya kujitolea na nitumie fursa hii wabunge wetu na wabunge wa baraza
la wawakilishi mfanye kazi kwa kujitolea ili kuimarisha chama
chetu,”alisema.
Dk.Bashiru alisema kazi
wanayoifanya ni kuwalinda wabunge dhidi ya wanaowasumbua na watu
wasiofuata taratibu hivyo nao wasaidie kuimarisha chama.
Akizungumzia mkakati wa Umoja wa
Vijana wa CCM(UVCCM) wa ‘Tanzania ya kijani’, Dk.Bashiru alisema mkakati
huo umepokelewa vizuri na kuwataka usitumike kama makongamano ya
kuonekana kwenye TV na mitandao ya kijamii ikiwemo ‘You tube’
“Sasa nataka vijana wabadilike
kutoka kwenye hamasa waende kwenye kazi ya siasa ya kuimarisha chama ili
shughuli ipimike, vinginevyo huu mkakati nitausimamisha nimeshaongea na
katibu ni mkakati mzuri tusiposimamia unaweza kuzaa jambo ambalo
hatujalitarajia,”alisema.
Alieleza kuwa vijana wawe na mvuto
wa kukilinda chama na inapotokea mtu anakichokoza chama ahame chama
aonekane ni jasiri na sio legelege.
Kuhusu gazeti hilo, Dk.Bashiru
alisema litatumika kujenga na kuimarisha chama nay eye atakuwa na
ukurasa wake ambao atakuwa anazungumzia kuhusu urithi.
Alisema katika ukurasa huo kutakuwa na mambo matano ikiwemo haki, tunu za taifa.
“Kuna mjadala kuhusu tunu za Taifa
kulikuwa na mjadala hata kwenye Bunge la Katiba ambapo moja ya tunu ni
lugha ya Kiswahili, na gazeti hili litatumika kukuza Kiswahili,”alisema.
Alisema kati ya mambo ambayo
yamefanyika chini ya uongozi wa Spika Job Ndugai ambayo ni kubwa kuliko
yote ni uamuzi wa kimapinduzi wa kulinda rasilimali kwa kutunga sheria
ambayo inaonesha nchi imegoma kugeuzwa shamba la bibi.
Aidha alisema katika mikakati ya
kisiasa ya kuimarisha uhai wa chama ipo minne ambapo ni pamoja na
kukomaza demokrasia mashinani kupitia kwa wenyeviti wa mashina na
mabalozi ili kukifanya kuwa karibu na wananchi na wanachama.
Awali, Spika wa Bunge Job Ndugai,
alipongeza kuanzishwa kwa gazeti hilo na kudai kuwa kukosekana kwa
habari kwenye matawi kumekuwa ni unyonge mkubwa.
“Gazeti lina habari za kuelimisha
jambo hili ni jema nakuahidi sisi wabunge tutatoa kila aina ya
ushirikiano, tutachukua nakala kwa idadi ya matawi, kata, na wilaya na
limekuja wakati muafaka maana tunaelekea kwenye uchaguzi,”alisema.
Alisema chama kina nguvu kubwa ya kuvitumia vyombo vyake vya habari ili kukabiliana na vitendo vya upotoshaji.
0 comments:
Post a Comment