Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akiangalia namna dhahabu inavyochenjuliwa kwa kutumia zebaki katika eneo la
wachimbaji wadogo Mugusu Mkoani Geita. Serikali imeazimia kupunguza matumizi
ya zebaki kwa wachimbaji wadogo kutokana na athari kwa binadamu na
mazingira.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akikagua chanzo cha maji cha Mto Mabubi kilichopo katika Kata ya Mugusu Mkoani
Geita. Naibu Waziri Sima amewaagiza wakazi wa eneo hilo kulinda chanzo hicho kwa
kutofanya shughuli za kibinadamu kandokando, sambamba na kupunguza matumizi ya
zebaki ili kulinda afya za wanachi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akizungumza na wakazi wa Kata ya Mugusu Mkoa wa Geita ambao
wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji madini na kuchenjua dhahabu kwa
kutumia zebaki. Naibu Waziri amewaeleza athari za matumizi ya zebaki na
kuwataka kujiunga na vikundi rasmi ili waweze kunufaika na mikopo itolewayo na
Serikali.
Afisa Madini Mkoa wa Geita Bw. Ernest Maganga (kushoto) akifafanua jambo kwa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
mara baada ya kutembelea mtambo maalumu wa kuchenjua dhahabu wa Jambo Africa– Geita.
*************
Na Lulu Mussa
GEITA
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kata ya Mugusu Mkoani Geita
wametakiwa kufuata taratibu za hifadhi ya mazingira ili kunusuru afya zao na
kuchukua tahadhari ya kukabiliana na uwezekano wa milipuko ya magonjwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi kutembelea
eneo la Mgusu, kuona uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya
Mwaka 2004.
Akiwa katika eneo la Mugusu Naibu Waziri Sima amesema bado kuna tatizo la
usafi wa mazingira katika maeneo wanayoyatumia kuchenjua dhahabu kwa
kutumia zebaki, na kuna haja wachimbaji hao kukaa na halmashauri ya Geita
Vijijini ili kuhakikisha wanakuwa na vyoo bora.
Akitoa kauli ya Serikali kuhusu mpango kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya
zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika shughuli za uchenjuaji, Sima
amewataka wakazi wa Mgusu kuendelea na shughuli za uzalishaji wa dhahabu
bila kuathiri sekta ya mazingira kwa kupunguza matumizi ya zebaki inayoharibu
mazingira na afya za binadamu.
“Nimeona namna vijana wanavyojishughulisha kwa ajili ya kujipatia kipato, hili ni
jambo jema kwenye Taifa letu, lakini nimetembea hadi chini kwenye ule mto wa
Nyamasenge hakuna vyoo, watu wanatumia pori na mto kwa ajili ya haja ndogo
na kubwa.
“Kwa mazingira yetu ni hatari sana, tunaweza kufanya kazi nzuri lakini ugonjwa
utasitisha shughuli zetu. Nawasisitiza kuwa Usafi ni jambo la kwanza katika
kufanya kazi, huwezi kuwa na nguvu isiyojali usafi,” alisema Sima.
Awali, Naibu Waziri Sima alitembelea chanzo cha maji cha maji cha Mto Mabubi
na kujionea hali mbaya inayotishia kutoweka kwa chanzo hicho kutokana na
shughuli za kibinadamu zinazoendelea kandokando ya eneo hilo.
“Chanzo cha maji cha mto Mabubi, hakitadumu na maji hayatakuwa salama kwa
matumizi ya binadamu endapo kitaendelea kuingia kemikali ya zebaki nanyi
wachimbaji kujisaidia katika eneo hilo” Sima alisisitiza.
Diwani wa Kata ya Mgusu Bw. Pastory Ruhusa amesema kuwa ataitisha
mkutano wa wananchi mapema iwezekanavyo ili kuweka mikakati ya haraka kutokomeza hali hiyo ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira na kupunguza
matumizi ya zebaki.
Naibu Waziri Sima yuko katika ziara ya kikazi Kanda ya Ziwa kukagua uzingatiaji
na usimamizi wa Sheria ya Mazingira pamoja na uwaelimisha wananchi mpango wa Serikali wa kupunguza matumizi ya zebaki nchini.
0 comments:
Post a Comment