1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency-IRENA) ni Taasisi iliyoanzishwa tarehe 26 Januari, 2009 na ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mwezi Aprili, 2011. Kwa mujibu wa Mkataba wa IRENA (Statute of the International Renewable Energy Agency-IRENA) ulioanza kutekelezwa mwezi Julai, 2010, lengo la Taasisi hiyo ni kuendeleza na kuhamasisha matumizi endelevu ya aina zote za nishati jadidifu kwa kuzingatia manufaa yatokanayo na nishati hiyo na mchango wake katika kuhifadhi mazingira; kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; kuimarisha upatikanaji wa nishati safi, salama, ya uhakika na gharama nafuu pamoja na kupunguza umaskini na kuleta maendeleo endelevu. Nishati hizo jadidifu ni pamoja na upepo, maporomoko ya maji, jua, tungamotaka, jotoardhi pamoja na mawimbi ya bahari. Aidha, Taasisi hiyo inazingatia haki, usawa na uwezo wa kila mwanachama katika utekelezaji wa majukumu yake. Vilevile, Taasisi hiyo inahamasisha uendelezaji wa teknolojia mbalimbali katika kuzalisha umeme na hivyo kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uwiano wa vyanzo vya nishati (energy mix) nchini. Makao Makuu ya IRENA yapo Abu Dhabi, Falme za Kiarabu na Mji wa Bonn nchini Ujerumani ni Kituo cha Uvumbuzi na Teknolojia cha Taasisi hiyo.
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2011 IRENA ilipoanza kutekeleza majukumu yake, idadi ya nchi zilizoridhia Mtakaba wa Taasisi hiyo imeongezeka kutoka nchi 85 hadi 168 mwaka 2022 ambapo za ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) ni Kenya, Uganda na Rwanda na ukanda wa SADC ni Angola, Botswana, Comoros, Eswatini, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe. Tanzania ilisaini Mkataba huo tarehe 15 Juni, 2009 na kwa mujibu wa Ibara ya 19 ya Mkataba huo, Tanzania itatambuliwa kuwa mwanachama wa Taasisi hiyo siku ya 30 baada ya tarehe ya kuwasilisha Hati ya Kuridhia Mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, vyombo vya usimamizi na uendeshaji wa IRENA vinahusisha Mkutano Mkuu (Assembly) ambacho ndicho chombo cha juu cha maamuzi, Baraza la IRENA linaloundwa na wawakilishi kuanzia 11 hadi 21 kutoka wanachama watakaochaguliwa na Mkutano Mkuu na Sekretarieti inayoongozwa na Mkurugenzi Mkuu na watumishi wengine wa IRENA. Bajeti ya uendeshaji wa Taasisi hiyo inatokana na michango ya lazima kutoka kwa wanachama, michango ya hiari na vyanzo vingine. Aidha, Bajeti hiyo huandaliwa na Sekretarieti na kuwasilishwa katika Baraza la IRENA kwa uchambuzi kisha kujadiliwa na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu. Mkataba wa IRENA unabainisha majukumu mbalimbali ya Taasisi hiyo, yanayolenga kuleta manufaa kwa wanachama wake kupitia nishati jadidifu, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kisera; kuwajengea uwezo kupitia
mafunzo, teknolojia, elimu na kubadilishana ujuzi na utafiti; kuwezesha upatikanaji wa rasimali fedha za kutekeleza miradi ya nishati jadidifu pamoja na kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu za uendelezaji wa nishati jadidifu.
2. MKATABA WA TAASISI YA KIMATAIFA YA NISHATI JADIDIFU (STATUTE OF THE INTERNATIONAL RENEWABLE ENERGY AGENCY – IRENA) WA MWAKA 2009
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati Jadidifu (Statute of the International Renewable Energy Agency – IRENA) wa mwaka 2009 una jumla ya Ibara ishirini (20) kama ifuatavyo:
(i) Ibara ya I - Kuanzishwa kwa Taasisi ya IRENA: Ibara hii inaeleza kuhusu uanzishwaji wa Taasisi hii inayozingatia misingi ya usawa kwa wanachama wote na kuheshimu mamlaka na uwezo wa Wanachama katika kutekeleza majukumu yake.
(ii) Ibara ya II - Malengo ya Taasisi: Ibara hii inahusu malengo ya kuundwa kwa IRENA ambapo lengo kuu ni kuhamasisha, kupanua na kuongeza matumizi endelevu ya vyanzo vyote vya nishati jadidifu kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa na manufaa yatokanayo na mikakati ya kukuza nishati hiyo, pamoja na mchango wake katika kuhifadhi mazingira hususan kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi; kukuza uchumi na kupunguza umaskini pamoja na usalama katika upatikanaji wa nishati.
(iii) Ibara ya III - Tafsiri: Ibara hii inahusu tafsiri ya vyanzo mbalimbali vya nishati jadidifu ikiwemo nishati za tungamotaka, jotoardhi, maporomoko ya maji, jua, upepo na mawimbi ya bahari.
(iv) Ibara ya IV – Majukumu ya IRENA: Ibara hii inafafanua kuhusu majukumu ya IRENA. Majukumu hayo ni pamoja na kufanya uchambuzi wa masuala ya kisera, uwekezaji, uzoefu na teknolojia kwa lengo la kutoa ushauri mahsusi kwa Wanachama katika kuendeleza nishati jadidifu katika nchi zao; kuwajengea uwezo wanachama katika usimamizi na uendelezaji wa nishati jadidifu kupitia elimu na mafunzo, teknolojia, masuala ya ubora, kubadilishana ujuzi na utafiti; kusaidia upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya nishati jadidifu; na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za nishati jadidifu kwa viwango vya kimataifa. Ibara hii inaielekeza IRENA kuwasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu yake kwa wanachama.
(v) Ibara ya V - Mpango Kazi na Miradi: Ibara hii inaelezea pamoja na mambo mengine, Mpango Kazi na miradi itakayotekelezwa na IRENA ambapo shughuli za Taasisi zitatekelezwa kwa kufuata Mpango Kazi wa mwaka utakaoandaliwa na Sekretarieti, kupitishwa na Baraza na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu. Pia Taasisi kwa kushauriana na nchi wanachama inaweza kutekeleza miradi iliyobuniwa na wanachama kutegemeana na upatikanaji wa fedha na rasilimali nyingine.
(vi) Ibara ya VI – Uanachama wa IRENA: Ibara hii inaelezea taratibu na kanuni za kuwa mwanachama wa IRENA ambapo ili nchi iwe mwanachama inapaswa kuwa ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa au Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda. Nchi au taasisi hizo zitakuwa mwanachama wa IRENA kwa kusaini mkataba wa kuanzishwa kwa IRENA; na kuwasilisha kwa mhifadhi Hati ya Kuridhia mkataba huo au kwa wanachama wapya kuwasilisha hati ya kuridhia mkataba baada ya maombi ya kujiunga uanachama kukubaliwa. Jumuiya za ushirikiano wa kikanda kama SADC, EAC, ECOWAS, EU zinaweza kupatiwa uanachama kwa kutambua kazi zao kuhusiana na malengo ya IRENA.
(vii) Ibara ya VII - Wanachama wasio na Turufu (Observers): Ibara hii inaelezea nchi au Taasisi ambazo sio wanachama zinavyoweza kushiriki katika masuala ya IRENA. Aidha, Taasisi zinapaswa kuwa ni Asasi za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya nishati jadidifu; nchi iliyosaini mkataba wa kuanzishwa kwa IRENA lakini bado haijaridhia mkataba huo na nchi inayosubiri kupatiwa uanachama baada ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na IRENA. Aina hii ya wanachama wanaweza kushiriki katika vikao vya IRENA ikiwemo Mkutano Mkuu bila haki ya kupiga kura.
(viii) Ibara ya VIII – Muundo wa IRENA: Ibara hii inaelezea vyombo (organs) muhimu vya IRENA ambavyo ni Mkutano Mkuu, Baraza na Sekretarieti. Mkutano Mkuu na Baraza vinaweza kuunda chombo mahsusi cha kutekeleza kazi zao kulingana na mkataba na kwa ridhaa ya Mkutano Mkuu.
(ix) Ibara ya IX - Mkutano Mkuu: Ibara hii inaelezea kuwa Mkutano Mkuu ndicho chombo cha juu cha maamuzi cha IRENA ambacho majukumu yake ni pamoja na kujadili na kufanya maamuzi kuhusu masuala yoyote yanayohusiana na Mkataba wa IRENA au majukumu ya vyombo vya Taasisi hiyo; kutoa mapendekezo mbalimbali kwa wanachama, Baraza na Sekretarieti; kuchagua wanachama wa Baraza na kuidhinisha marekebisho katika Mkataba wa IRENA. Majukumu mengine ni kupitisha bajeti na mpango kazi wa mwaka;
kuamua kuhusu maombi ya uanachama yaliyowasilishwa; kuidhinisha Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Mkutano Mkuu na Baraza pamoja na shughuli nyingine zinazohusiana na Sera na Kanuni za kifedha; kuteua Mkurugenzi Mkuu wa IRENA pamoja na Mkaguzi wa Hesabu za Taasisi.
Mkutano Mkuu unaundwa na wanachama wote wa IRENA na unafanyika mara moja kwa mwaka. Rais na Maafisa wa Mkutano Mkuu wanachaguliwa na wajumbe wa Mkutano huo kwa kuzingatia uwakilishi wa kijiografia.
Nchi wanachama zinapaswa kujigharamia kushiriki katika Mkutano Mkuu wa IRENA. Aidha, kila mwanachama ana kura moja katika Mkutano Mkuu na maamuzi makubwa katika Mkutano huo yanafanyika kupitia makubaliano ya wote (consensus) waliohudhuria Mkutano.
Endapo makubalinao ya wote hayatafikiwa katika jambo linalojadiliwa, consensus itatambulika kufikiwa endapo hakuna zaidi ya nchi mbili wanachama zilizopinga uamuzi unaokusudiwa kufanyika. Utaratibu wa idadi iliyozidi nusu (simple majority) unatumika kufanya maamuzi kwa upande wa masuala ya kiutaratibu (questions of procedure).
(x) Ibara ya X - Baraza: Linaundwa na wajumbe wasiopungua 11 na wasiozidi 21 wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu kwa utaratibu wa mzunguko kwa lengo la kuhakikisha ushiriki wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea, usawa wa kijiografia na ufanisi wa Baraza. Wajumbe wanachaguliwa kwa kipindi cha miaka miwili na kila mjumbe ana kura moja katika maamuzi yanayofanywa na chombo hicho. Aidha, maamuzi kwa masuala makubwa yanafanyika kwa urataratibu wa theluthi mbili na kwa upande wa masuala ya kiutaratibu simple majority inatumika. Majukumu ya Baraza hili ni pamoja na kuchambua na kuwasilisha katika Mkutano Mkuu rasimu ya Mpango Kazi, Bajeti na Taarifa ya Mwaka ya Utekelezaji wa majukumu ya IRENA; kuidhinisha Agenda za Mkutano Mkuu na kuandaa Mikataba mbalimbali.
(xi) Ibara ya XI - Sekretarieti: Ibara hii inaelezea muundo na majukumu ya Sekretarieti ya IRENA ambapo Mkurugenzi Mkuu ndiye msimamizi mkuu wa masuala ya utawala, rasilimaliwatu na shughuli za kila siku za Taasisi. Sekretarieti pamoja na mambo mengine, ina jukumu la kuandaa na kuwasilisha kwenye Baraza rasimu ya Mpango Kazi na Bajeti ya Taasisi, kutekeleza Mpango Kazi na maamuzi, kuandaa na kuwasilisha kwenye Baraza rasimu ya taarifa za shughuli za Taasisi na kuratibu mawasiliano kati ya Taasisi na wanachama wake.
(xii) Ibara ya XII - Bajeti: Ibara hii inaelezea vyanzo vya fedha za kugharamia utekelezaji wa majukumu ya IRENA. Vyanzo hivyo vinajumuisha michango ya Wanachama kulingana na kikokotoo cha Umoja wa Mataifa, michango ya hiari na vyanzo vingine. Rasimu ya bajeti itaandaliwa na Sekretarieti na kuwasilishwa kwenye Baraza la IRENA kwa uchambuzi kabla ya kuwasilishwa na Baraza katika Mkutano Mkuu kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa.
(xiii) Ibara ya XIII - Utu wa Kisheria, Haki na Kinga: Ibara hii inaelezea utu wa kisheria, haki na kinga kwa Taasisi kwa kutumia sheria za ndani za nchi wanachama wakati wa utekelezaji wa shughuli za Taasisi.
(xiv) Ibara ya XIV - Uhusiano na Taasisi Nyingine: Ibara hii inaelezea taratibu za IRENA kushirikiana na Taasisi nyingine ambapo mapendekezo ya Baraza kuhusu uhusiano na Umoja wa Mataifa na Taasisi yoyote inayojishughulisha na masuala yanayoendana na malengo ya IRENA yataridhiwa na Mkutano Mkuu. Aidha mkataba wa IRENA hautoathiri haki na majukumu ya mwanachama katika mikataba mingine ya kimataifa.
(xv) Ibara ya XV - Marekebisho, Kujitoa na Mapitio: Ibara hii inaelezea taratibu za kufanya marekebisho, mapitio na kujitoa katika Mkataba wa IRENA. Marekebisho ya mkataba yanaweza kupendekezwa na mwanachama yeyote na Mkurugenzi Mkuu atawasilisha mapendekezo ya marekebisho yaliyowasilishwa kwa wanachama angalau siku 90 kabla ya kujadiliwa kwenye Mkutano Mkuu. Mwanachama yeyote anaweza kujitoa uanachama kwa kutoa Notisi ya maandishi kwa Mhifadhi wa Hati ya Mkataba ambaye atalitaarifu Baraza la IRENA na wanachama wote kuhusu kusudio hilo.
(xvi) Ibara ya XVI- Usuluhishaji wa Migogoro: Ibara hii inaelezea namna ambavyo wanachama watakavyosuluhisha migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa Mkataba wa IRENA. Katika ibara hii inaeleza kuwa mgogoro wowote utakaohusu tafsiri ya mkataba utasuluhishwa kwa njia ya amani kulingana na kanuni na taratibu za Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Aidha, Baraza la IRENA linaweza kuhusika katika utatuzi wa mgogoro baina ya wanachama wake.
(xvii) Ibara ya XVII - Kusitisha Haki kwa Muda: Ibara hii inaelezea masuala ambayo yanaweza kusababisha usitishwaji wa haki ya mwanachama kupiga kura katika maamuzi ya IRENA. Mwanachama atakayekuwa na malimbikizo ya mchango wa uanachama hatakua na haki ya kupiga kura endapo malimbikizo hayo yatafikia au kuzidi kiasi
alichopaswa kuchangia kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Aidha, Ibara hii inaeleza kuwa, Mkutano Mkuu unaweza kumruhusu mwanachama kuwa na haki ya kupiga kura baada ya kujiridhisha kuwa malimbikizo hayo yako nje ya uwezo wa mwanachama husika. Pia, mwanachama yeyote atakayeendelea kukiuka matakwa ya mkataba au makubaliano yoyote anaweza kusitishiwa haki ya uanachama na Mkutano Mkuu kwa kupigiwa kura na theluthi mbili ya wajumbe wa mkutano kulingana na mapendekezo ya Baraza.
(xviii) Ibara ya XVIII - Makao Makuu ya Taasisi: Ibara hii inaelezea mahali patakapokuwa Makao Makuu ya IRENA ambapo Mkutano Mkuu wa Kwanza utaamua mahali Makao Makuu yatakapokuwa.
(xix) Ibara ya XIX – Kujiunga na Kuridhia Mkataba wa IRENA: Ibara hii inaelezea utiaji saini, kuridhiwa na kuanza kutumika kwa mkataba. Mkataba huu upo wazi kwa nchi wanachama ambao ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na taasisi za ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda. Nchi nyingine na taasisi za ushirikiano wa kiuchumi za kikanda ambazo hazijajiunga na Taasisi hiyo, zitaridhia mkataba huu baada ya maombi ya uanachama kuidhinishwa na Mkutano Mkuu.
Utekelezaji wa Mkataba utaanza siku ya 30 baada ya nchi mwanachama wa 25 kuwasilisha Mkataba ulioridhiwa. Kwa nchi au taasisi za ushirikiano wa kikanda zitakazoridhia mkataba baada ya kuanza kwa utekelezaji wa Mkataba, Mkataba utaanza kutumika baada ya siku ya thelathini ya kuwasilisha hati ya kuridhia mkataba kwa Mhifadhi.
(xx) Ibara ya XX - Mhifadhi, Usajili na Uhalali wa Nyaraka: Ibara hii inaelezea pamoja na mambo mengine, kuhusu nchi itakayokuwa Mhifadhi wa mkataba, taratibu za kuusajili na masuala mengine yanayohusiana na Mkataba. Ibara hii inaeleza kuwa nchi ya Ujerumani ndiyo itakuwa Mhifadhi wa Mkataba na utasajiliwa na Serikali ya nchi Mhifadhi kulingana na kifungu cha 102 cha Mkataba wa Kimataifa. Lugha ya Mkataba itakuwa ni Kingereza na nyaraka zitahifadhiwa katika Ofisi za Utunzaji nyaraka za kumbukumbu.
Kiambatisho Na. 1 ni Mkataba wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati Jadidifu
(Statute of the International Renewable Energy Agency – IRENA).
3. WAJIBU WA NCHI BAADA YA KUJIUNGA
Mheshimiwa Spika, endapo Mkataba wa IRENA utaridhiwa, wajibu wa nchi utakuwa ni pamoja na kulipa michango ya ada ya uanachama ya kila
mwaka ambayo ni midogo na inayozingatia uwezo wa kiuchumi wa nchi mwanachama, pamoja na kushiriki katika utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo, ikiwemo mikutano mbalimbali.
4. SERA, SHERIA NA MIPANGO MBALIMBALI KUHUSU UENDELEZAJI WA NISHATI JADIDIFU NCHINI
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 inatambua rasilimali kubwa ya nishati jadidifu iliyopo nchini ikiwemo upepo, jua, tungamotaka, maporomoko madogo ya maji, jotoardhi, na mawimbi ya bahari. Sera inafafanua kuhusu changamoto zinazokabili uendelezaji wa rasilimali hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji kwa kuzingatia gharama kubwa za uwekezaji zinazohitajika, uhaba wa takwimu, teknolojia, vihatarishi na utaalamu. Sera imeweka lengo linalojikita katika kuimarisha mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme (enhancing utilisation of renewable energy resources so as to increase its contribution in electricity generation mix). Aidha, Sheria ya Umeme ya Mwaka 2008 inatoa mwongozo wa kisheria wa uwekezaji katika nishati jadidifu na kwa upande wa Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Sekta Ndogo ya Umeme [Power System Master Plan, 2012 (2020 update)], Mpango huo umelenga kuzalisha megawati 800 (3.96%) kutokana na upepo; megawati 715 (3.54%) kutokana na umeme jua na megawati 995 (4.93%) kutokana na jotoardhi ifikapo mwaka 2044.
Vilevile, kwa sasa unaandaliwa Mkakati wa Taifa wa Nishati Jadidifu (National Renewable Energy Stratergy) unaolenga kuimarisha uendelezaji wa nishati jadidifu nchini ili zichangie ipasavyo katika uzalishaji wa umeme. Pia, kutokana na hali ya mabadiliko ya tabia nchi inayoendelea duniani pamoja na uharibifu wa mazingira, mwelekeo wa dunia kwa sasa ni kuimarisha matumizi ya nishati jadidifu kama chanzo cha nishati. Kuridhiwa kwa Mkataba wa IRENA kutachangia katika kufikiwa kwa malengo ya kisera, mikakati na mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia malengo na majukumu ya Taasisi hiyo. Aidha, mkataba huu hauzuii nchi kuendeleza vyanzo vyake vingine vya nishati ikiwemo mafuta, gesi asilia na makaa ya mawe, bali unahimiza kuwepo kwa vyanzo mchanganyiko (energy mix) kwa lengo la kuwezesha uhakika na uendelevu wa upatikanaji wa nishati kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
5. RASILIMALI ZA NISHATI JADIDIFU ZILIZOPO NCHINI NA UENDELEZAJI WAKE
Mheshimiwa Spika, nishati jadidifu inapatikana katika maeneo mbalimbali nchini. Maeneo yaliyobainishwa kuwa na fursa ya uzalishaji wa umeme jua ni pamoja na Zuzu, Dodoma (MW 50); Manyoni, Singida (MW 100); Same,
Kilimanjaro (MW 50) na Kishapu, Shinyanga (MW 150). Aidha, Tanzania inakadiriwa kuweza kuzalisha hadi MW 1,000 za umeme wa upepo. Maeneo yaliyofanyiwa tathmini na kuonekana kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa upepo ni pamoja na Litembe, Mtwara; Karatu, Manyara; Kititimo, Singida na Makambako, Njombe. Vilevile, Tanzania ina rasilimali ya jotoardhi inayoweza kuzalisha MW 5,000 za umeme.
Mheshimiwa Spika, maeneo yenye viashiria vya jotoardhi nchini ni pamoja na Ukanda wa Volkano wa Kusini Magharibi unaojumuisha maeneo ya Songwe (Songwe); Ngozi, Kiejo-Mbaka, Mbarali, Kasumulu na Mampulo (Mbeya) – MW 1,000; Ukanda wa Volkano wa Kaskazini unaojumuisha maeneo ya Mlima Meru, Natron, Eyasi (Arusha), Rundugai (Kilimanjaro), Manyara na Masware (Manyara) – MW 1,000; Kanda ya Pwani inayojumuisha maeneo ya Luhoi na Utete (Pwani) na Amboni na Bombo (Tanga) - MW 600; Kanda ya Kati yenye maeneo ya Ibadakuli (Shinyanga); Kondoa, Takwa (Dodoma); Isanja, Msule (Singida) na Balangidalalu (Manyara) - MW 500; mkondo wa Magharibi wa Bonde la Ufa unaojumuisha maeneo ya Mtagata (Kagera); Kanazi, Rock of Hades na Majimoto (Katavi) na Ruaha Mkuu (Iringa) - MW 900; na maeneo mengine yanayojumuisha Kisaki, Tagalala na Mtende (Morogoro); Majimoto, Monanka na Nyamosi (Mara) - MW 1,000.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza rasilimali za nishati jadidifu zilizopo nchini, hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwemo kuanzisha Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (Tanzania Geothermal Development Company Limited-TGDC), kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji umeme kutokana na maporomoko madogo ya maji (small hydro) ili kuhakikisha bei ya wazalishaji wa umeme huo inavutia uwekezaji, kuhamasisha viwanda vinavyozalisha taka kama vile vya sukari kuwekeza kwenye uzalishaji wa umeme, kufanya Upembuzi Yakinifu na tathmini kwa ajili ya uzalishaji umeme wa jua na upepo, kuweka mfumo wa utaratibu wa kushindanisha upatikanaji wa waendelezaji wa miradi na kutangaza miradi ya nishati jadidifu kwa wawekezaji kupitia majukwaa mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa sasa, kuna wazalishaji mbalimbali wa umeme wa nishati jadidifu wenye leseni za kuzalisha umeme huo ikiwemo kiwanda cha TPC, Moshi (Tungamotaka)-MW 20; NextGen Solawazi, Kigoma (Umeme Jua)-MW 5, Mwenga, Mufindi (upepo)-MW 2.4, Bagamoyo Sugar Limited, Bagamoyo (Tungamotaka)-MW 5; TANWAT, Njombe (Tungamotaka)-MW 1.50; SSI Energy(T) Limited, Kahama (umeme jua)-MW 10 na Suma Hydro Limited, Rungwe (maji)-MW 4.
6. MANUFAA YA KURIDHIA MKATABA
Mheshimiwa Spika, kuridhiwa kwa Mkataba wa IRENA kutakiwa na manufaa yafuatayo:
a) Kuimarika kwa mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini na kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii na kutatua changamoto ya vyanzo vya umeme visivyo endelevu na uhakika;
b) Nchi kupata taarifa na takwimu sahihi kuhusu masuala ya nishati jadidifu na pia fursa za uwekezaji katika nishati hiyo zilizopo;
c) Kuimarika kwa utaalamu, teknolojia, utafiti na uelewa kuhusu nishati jadidifu kwa watoa maamuzi na wadau mbalimbali wa nishati;
d) Kuimarika kwa uwekezaji, mitaji na upatikanaji wa ushauri wa kiufundi katika uendelezaji wa nishati jadidifu nchini;
e) Kupungua kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji na matumizi ya nishati isiyo rafiki wa mazingira na pia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi;
f) Kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu na rafiki wa mazingira ambayo ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini;
g) Kuchochea kasi ya kufikiwa kwa malengo na shabaha ya Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015, maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020, Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme wa Mwaka 2020 na Shabaha za Lengo Na. 7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030 linalozitaka nchi kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, endelevu, ya kisasa na gharama nafuu kwa wote; na
h) Kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mwelekeo wa dunia kwa sasa kuhusu matumizi ya vyanzo vya nishati visivyoathari mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
7. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, naomba sasa niwasilishe Azimio la Tanzania kuridhia mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (Statute of the International Renewable Energy Agency- IRENA).
0 comments:
Post a Comment