WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza
Wizara za Kilimo, Viwanda na Biashara, Uvuvi na Mifugo kushirikiana na
Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji
kutengeneza mkakati wa kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo,
mifugo na uvuvi nchini.
Amevitaja viwanda kuwa ni pamoja na vya
nyuzi, nguo, ngozi, maziwa, minofu, nyama, kubangua korosho, kutengeneza
unga, mafuta ya kula, sabuni, usindikaji wa matunda na mbogamboga,
“Kwani ndiyo msingi wa kauli mbiu yetu ya kufikia uchumi wa viwanda
2025”.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Alhamisi, Agosti 8, 2019) katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya
wakulima nane nane Kitaifa kwenye viwanja vya maonesho Nyakabindi mkoani
Simiyu kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu amsema sambamba na mkakati
huo, pia ameagiza kuimarishwa kwa vyama vya ushirika ili kumwezesha
mkulima kuendelea kumiliki zao lake mpaka hatua ya kuuza sokoni. “Vyama
vya ushirika vikiweza kuchakata mazao na kuyaongeza thamani
vitamuwezesha mkulima kuwa na umiliki na kufaidika na bei ya soko”.
Amesema mfano uliooneshwa katika zao la
Kahawa kupitia Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KCU) ni mzuri ambapo
wanamiliki asilimia 100 ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa (BUCOP), pamoja na
asilimia 54 ya Kiwanda cha Kuzalisha Kahawa – Tanganyika Instant Coffee
(TANICA).
“Kwa upande wa Pamba, Nyanza Cooperative
Union (NCU) walianza vizuri kwa kumiliki viwanda vinane vya kuchambulia
pamba. Tunataka jitihada za namna hii zianzishwe katika shughuli za
wakulima wetu na zilizopo ziimarishwe”.
Hivyo, ameitaka Tume ya Maendeleo ya
Ushirika kwa kushirikiana na wadau, ifanye tathmini kwenye vyama vya
ushirika vinavyomiliki viwanda ili kubaini hali ilivyo kwa sasa na
kuweka mikakati ya kuvifufua na kuviongezea uwezo.
Amesema safari ya kujenga uchumi wa
viwanda itaiwezesha Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati imeanza na
inaendelea vizuri na matarajio yake ni kuona wananchi wote bila kujali
tofauti za kiitikadi, wataendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuwa
maendeleo wanayoyapigania ni kwa manufaa ya wote waliopo leo na vizazi
vijavyo.
Waziri Mkuu amesema kwa mantiki hiyo,
kila Mtanzania hanabudi kuongeza bidii katika kufanya kazi, kupiga vita
rushwa, kulipa kodi ya Serikali na kulinda rasilimali za Taifa ili
ziweze kutumika sasa na kwa faida ya vizazi vyetu vijavyo.
“Niwaombe muendelee kuiunga mkono
Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imeamua kwa makusudi
kuanzisha miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi
inayoendelea kujengwa nchini ikiwemo reli ya kisasa ya mwendokasi, mradi
mkubwa wa umeme wa Mto Rufiji, upanuzi wa viwanja vya ndege, bandari na
ununuzi wa ndege kubwa”.
Amesema kuboreshwa kwa miundombinu hiyo,
pamoja na mambo mengine kutachochea uwekezaji mkubwa katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi, kurahisisha usafirishaji wa mazao, mifugo,
samaki, na kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuwezesha viwanda
vya ndani kushindana kibiashara na bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya
nje ya nchi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kutoawito kwa viongozi wa Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga
kuendelea kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo kuhakikisha viwanja
hivyo vya Nyakabindi, vinakuwa kituo cha mafunzo ya wakulima, wafugaji
na wavuvi.
“Kumbukeni kuwa kila mmoja wetu akitimiza
wajibu wake ipasavyo, maendeleo ya viwanda yanawezekana, ajira
zitapatikana, uhakika wa chakula na lishe bora itakuwepo na sote kwa
pamoja tutasonga mbele kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025”.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Nane Nane ya
mwaka huu inasema: – “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa
Nchi”.Kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya kukuza uchumi wa viwanda na biashara, ikilenga kukuza uchumi wa
mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa na wakati huo huo kupunguza umaskini.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea na kukagua
mabanda mbalimbali katika maoneosho hayo. Miongoni mwa mabanda
aliyoyatembelea ni pamoja na banda la EPZA, NMB, CRDB, NBC, BOT kitengo
cha mifumo ya malipo ya Kielektroniki ya Serikali, Wizara ya Kilimo,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na JKT.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu
Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi,
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina,
Naibu Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nchi
OR-TAMISEMI, Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Madini, Stansalaus
Nyongo pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment