METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, August 4, 2019

YANGA YATOKA SARE YA 1-1 NA KARIOBANGI SHARKS,TAIFA YAFURIKA WIKI YA MWANANCHI

Na Asha Kigundula, Dar es Salaam
TIMU Yanga SC imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Kariobangi Sharks ya Kenya katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuhitimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Katika mchezo huo maalum wa Yanga SC kuzindua msimu wake mpya, Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kumeza watu 60,000 ulionekana kusheheni na kupendeza kwa rangi za kijani na njano, huku makundi mengine wakibaki nje kwa kukosa nafasi ya kuingia ndani.

Pamoja na yote, wageni Kariobangi Sharks walitangulia kupata bao dakika ya 50 ya kupitia kwa nyota wake Patrick Otieno aliyemalizia pasi ya Patrick Nguyi.
Lakini Yanga SC iliyotumia mchezo huo kutambulisha kikosi chake kipya na jezi mpya za msimu, ikasawazisha bao hilo kwa penalti dakika ya 57 kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Patrick Sibomana aliyefunga kwa penalti kufuatia mchezaji wa Kariobangi kuunawa mpira.

Huo unakuwa mchezo wa tano mfululizo Yanga SC inacheza katika maandalizi ya msimu mpya, baada ya kushinda zote nne za awali katika kambi ya mjini Morogoro.

Ilishinda 10-1 dhidi ya dhidi ya Tanzanite, 7-0 dhidi ya ATN, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 1-0 dhidi ya Mawenzi Market.
Na yote hayo ni maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC wakianza na Township Rollers ya Botswana kati ya Agosti 9 na 11 mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nao mjini Gaborone kati ya Agosti 23 na 25.
Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza Yanga itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Farouk Shikhalo, Moustafa Selemani, Muhaeami Issa ‘Marcelo’, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Papy Tshishimbi, Mapinduzi Balama, Mohammed Issa ‘Banka’/ Mrisho Ngassa dk65, Sadney Urikhob/ David Molinga ‘Falcao’ dk87, Juma Balinya/ Maybin Kalengo dk82 na Patrick Siebomana.
Kariobangi Sharks: Brian Bwire, Eric Juma/David Simiyu dk82, Samuel Qlwande, Kyara Amani, Nixon Omandi, Yidah Sven, Shaphan Oyugi/James Mazembe dk59, Harrison Mwendwa, Patrick Otieno/ Julius Masaba dk54/Peter Oudo dk88, Patrick Nguyi na Erick Kapato.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com