***************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Bw. Geoffrey
Mwangulumbi pamoja na Mwekahazina wa Manispaa hiyo, Bw. Pascal Makoye
kuwa anawataka wabadilike na waache kugombana na badala yake watekeleze
majukumu yao ipasavyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bibi Zainab Telack azisimamishe
kazi kampuni zote zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato katika Manispaa
hiyo kwa kuwa zimeshindwa kufanya kazi vizuri na zina madeni.
Waziri Mkuu ametoa maagizo
hayo leo (Ijumaa, Agosti 9, 2019) wakati alipozindua nyumba 10 za Askari
Polisi katika Manispaa ya Shinyanga eneo la Kambarage. Mradi huo
umetokana na fedha kiasi cha sh. milioni 225 zilizotolewa na Rais Dkt.
John Magufuli.
Amesema viongozi hao
wameshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia kikamilifu zoezi
la ukusanyaji wa mapato na kutoa kazi hiyo kwa kampuni zisizokuwa na
uwezo. Amesema mwaka jana walikadiria kukusanya sh. milioni 800 na
badala yake walikusanya sh. milioni 500.
Waziri Mkuu amesema Manispaa
hiyo haiwezi kusonga mbele kimaendeleo iwapo viongozi wake hawaelewani
wanagombana kila siku. “Mkurugenzi na wenzako nawaonya kwa mara ya
mwisho badilikeni na hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo
yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato.”
Akizungumzia kuhusu nyumba za
Askari Polisi, Waziri Mkuu amesema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni
kuhakikisha askari wanaishi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha
kutekeleza vizuri majukumu yao. “Ili waweze kutekeleza vizuri majukumu
yao lazima wawe na makazi mazuri”.
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito
kwa askari waliopewa funguo kwa ajili ya kuishi katika nyumba hizo
wahakikishe wanazitunza vizuri na hata inapotokea wamehamishiwa kwenda
katika vituo vingine, wale watakaohamia wakute nyumba hizo zikiwa katika
mazingira mazuri.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
amesema ujenzi wa nyumba hizo ni endelevu, ambapo pia amezitaka idara
mbalimbali za Serikali ziendelee na mchakato wa ujenzi wa nyumba zake
kwani wakiwa na nyumba nyingi itasaidia kupunguza idadi kubwa ya askari
wanaoishi uraiani.
Awali, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao alisema awali fedha zilizotolewa
zilikuwa zijenge nyumba tisa za vyumba viwili lakini kutokana na ubunifu
waliweza kuboresha mradi huo kwa kuongeza nyumba moja sambamba na
kuongeza chumba kimoja, hivyo kuufanya mradi huo kuwa na nyumba 10 zenye
vyumba vitatu vya kulala.
Pia alimshukuru Rais Dkt.
Magufuli kwa upendo wake mkubwa kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa
kulipatia fedha za kuboresha makazi ya askari. Mradi huo umekamilika kwa
gharama ya sh. milioni 278, 565, 500 wastani wa gharama za ujenzi kwa
nyumba moja ni sh. milioni 27, 856, 550. Alisema kiasi cha nyongeza cha
sh. milioni 53, 565,500 zilitolewa na wadau mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment