Mhandisi Din Fu Bin wa Kampuni ya
China Railway inayotengeneza barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga
(wa pili toka kulia) akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa barabara
hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo (wa kwanza Kushoto)
muda mfupi kabla ya ukaguzi wa barabara hiyo uliofanywa na Kamati ya
ulinzi na Usalama ya mkoa pamoja na Viongozi na Wataalamu wa Wilaya ya
Kalambo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (wa pili toka kushoto) pamoja na wataalamu wengine wakiteremka
kuelekea chini ya daraja la Mto Momba lililopo mpakani mwa Mkoa wa Rukwa
na Songwe ili kujionea ubora wa daraja hilo.
………………….
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanafanya
msako kwa wale wote waliohusika kuharibu na kung’oa ‘reflectors’
zilizowekwa kwenye vyuma vya kingo za barabara katika darala la Momba
lililopo mpakani mwa Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe katika Bonde la
Ziwa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga.
Amesema kuwa ung’oaji huo wa
‘reflectors’ hizo unaweza kusababisha ajali itakayopelekea kupoteza
maisha ya watu nyakati za usiku na kupoteza malengo ya ujenzi wa daraja
hilo na kuonya kutoendelea kwa uharibifu huo wenye lengo la kurudisha
nyuma maendeleo ya wananchi, mkoa na nchi kwa ujumla.
“Jeshi la Polisi mzisake bodaboda
zote ambazo zikikutwa zina ‘reflector’ hizi, kwasababu zinafahamika kama
hamjui, iwe kwenye bodaboda, iwe kwenye baiskeli, kamata na fikisha
mahakamani, hatuwezi kufumbia macho uharibifu huu, utakuja kesho utakuwa
wameng’oa kila kitu wataharibu. Kumbukeni kwamba bilioni 17.7 zimelala
hapa, na manufaa yote mmeyasikia na ninyi mnajua zaidi, sasa mnataka
kuturudisha wapi, hatutakubali uharibifu wa aina yoyote ile,”
Alisisitiza.
Mh. Wangabo aliyasema hayo tarehe
28.8.2019 alipotembelea daraja la Mto Momba kuona maendeleo ya daraja
hilo lililojengwa na mkandarasi Jianxi Geo – Engineering (Group)
Corporation kutoka China na kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) kupitia kitengo chake cha ushauri wa miradi TANROADS
Engineering Consulting Unit (TECU) ambapo hadi sasa daraja hilo
limeshakamilika kwa asilimia 100.
Wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa
Daraja hilo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa
Mhandisi Jetrovas August alisema kuwa kazi ya nyongeza ambayo ilikuwa
nje ya mkataba ni kuweka taa katika barabara ya km 1.125 ambayo ni
kiunganisho cha mikoa ya Songwe na Rukwa na kuongeza kuwamiongoni mwa
changamoto ni un’goaji wa ‘reflector’ katika barabara hiyo.
“Pamoja na Mkandarasi kumaliza na
kukabidhi mradi kwa serikali kumeanza kujitokeza uharibifu wa baadhi ya
miundombinu ya barabara, moja ya uharibifu ambao tayari umeanza
kujitokeza ni ung’oaji wa ‘reflector’ zilizowekwa kwenye vyuma
(guardrail) vya kingo la tuta la barabara kwaajili ya kuongozea magari
na vyombo vingine vya usafiri wakati wa usiku,” Alisema.
Katika Hatua nyingine, Mh. Wangabo
amewapongeza wakandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri wa ya ujenzi wa
barabara ya kutoka Sumbawanga – Matai – Kasanga yenye urefu wa Km 107
ambayo imefikia asilimia 91 ya ujenzina kubainisha kuwa barabara hiyo
imetimiza miaka tisa tangua kuanza kwa ujenzi wake lakini pamoja na
mambo mengine yaliyosababisha hayo ni maelewano mabovu yaliyokuwepo
baina ya Mkandarasi na Mshauri jambo ambalo hivi sasa limemalizika na
kazi inakwenda vizuri.
“Mkandarasi pamoja na ‘Consultant’
hay ani matokeo ya kuelewana, ‘Consultant’ na Mkandarasi wameelewana na
wanafanya kazi usiku na mchana na matokeo yake mnayaona kazi imefanyika
vizuri sana mimi nawapa pongezi sana, kwahiyo mimi nategemea kama
mlivyoniambi kwenye taarifa yenu kwamba kufikia tarehe 30 mwezi Septemba
barabara hii itakuwa imekwishafika bandarini kasanga na tutakuwa
tumemaliza mchezo lambda marekebisho ya hapa na pale,” Alieleza.
Mradi huo wa barabara ya
Sumbawanga – Matai – Kasanga unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania na
kugharimu Shilingi Bilioni 133.2 ambapo ujenzi wake unategemewa
kumalizika mwezi Septemba mwaka 2019 chini ya Mkandarasi Joint Venture
of China Railway 15G/New Century Company Ltd.
0 comments:
Post a Comment