Na Agnes Lubuva, Simiyu
Naibu
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde amesema Vyama vya Ushirika
havina budi kuendeleza jitihada za kutoa elimu ya ushirika kwa wanachama wa
vyama vya ushirika na wananchi wote kwakuwa ushirika ni dhana muhimu yenye
mchango mkubwa katika kupambana na umaskini.
Bw.
Malunde ameyasema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa maonesho ya Nanenane Kitaifa
katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. Alieleza kuwa Tume ya Maendeleo ya
Ushirika Tanzania (TCDC) imeshiriki maonesho ya Nanenane kipekee mwaka huu kwa
shughuli mbalimbali hususan kushirikisha vyama vya ushirika kwa lengo la kuongeza
mwamko na elimu ya ushirika miongoni mwa wananchi.
Kutokana
na ushiriki wa vyama hivyo wananchi watapata fursa zaidi ya kuona shughuli za
ushirika, kupata maelezo pamoja na kuuliza maswali mbalimbali kuhusu ushirika.
Aidha, Bw. Malunde amevitaja vyama vinavyoshiriki maonesho hayo mkoani Simiyu mwaka
huu kuwa ni pamoja na Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Usalama wa
Raia (URA SACCOS), Chama cha Umwagiliaji Ruvu (CHAURU), Chama Kikuu cha
Ushirika Kagera (KCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU), Chama Kikuu
cha Ushirika Lindi Mwambao, Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu (SIMCU), Chama
Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA),
na Rungwe & Busokelo Joint Enterprise Tea Corperative (R.B.T.C.J.E).
“Tume
inashiriki maonesho haya kipekee sana mwaka huu kwa kushirikisha vyama vya
ushirika vinavyojihusisha na shughuli mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji
nyuki, mifugo pamoja na vyama vya akiba na mikopo SACCOS. Vyama hivi
vimeshiriki kwaajili ya kuonesha bidhaa na shughuli mbalimbali zinazofanywa na
vyama hivyo. Niwasihi wananchi kuitumia fursa hii kupata elimu ya ushirika.”
Amesema Malunde
Naibu Mrajis amevipongeza vyama vyote vinavyoshiriki
maonesho hayo kwa kushirikiana bega kwa bega na Tume ya Maendeleo ya Ushirika
katika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya ushirika katika maonesho hayo.
Kwa
upande wake Afisa Ugani wa Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KCU), Bw. Godfrey Katiti ameunga
mkono hatua ya Tume kushirikisha vyama vya ushirika katika maonesho hayo kwani
hiyo ni fursa kwao kueleza manufaa ya ushirika na kupata wanachama zaidi. Aidha,
Katiti alieleza kuna faida kubwa kwa wakulima na wazalishaji wa mazao kujiunga
na vyama vya ushirika kwani vyama hivyo vinawapa nguvu ya pamoja katika kupata
mikopo kwa riba nafuu katika Taasisi za fedha pamoja na bei za mazao zenye ushindani na tija kwa
wakulima. Vile vile Katiti alitoa wito kwa wananchi kufika katika banda la KCU
kujifunza kuhusu “Kilimo Hai” ambacho ni kilimo kisichotumia Kemikali.
Pamoja
na mambo mengine katika “Kijiji cha Ushirika” ambacho ni mkusanyiko wa mabanda
mbalimbali ya vyama vya ushirika, taasisi na wadau wa sekta ya ushirika,
wananchi na wanachama wa vyama vya ushirika wanapata fursa ya kujua masuala
mengi kama vile haki na wajibu wao katika vyama, majukumu ya wanachama ikiwa ni
pamoja na kusimamia shughuli za uendeshaji wa chama, kuhakikisha hesabu za
vyama vya ushirika zinaandaliwa kwa wakati, kuchangia mawazo ya uboreshaji wa
utendaji wa vyama, kushiriki mikutano na vikao, kulipa malipo ya hisa,
kiingilio na michango mingine kwa mujibu wa taratibu za vyama vya ushirika.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment