Waziri
wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa NIC Dkt. Elirehema
Doriye, akifuatiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika Dkt.Titus Kamani, kushoto
ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka pamoja na viongozi wengine wa sekta
ya kilimo na Ushirika wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Vyama vya
ushirika waliopata vyeti vya utambuzi
kwa mchango katika Kilimo na Ushirika
Waziri
wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania
kutokana na Uhamasishaji, Usimamizi,
Udhibiti na Ufuatiliaji wa shughuli za Ushirika na kuhakikisha kwamba Vyama vya
Ushirika hapa nchini vinatekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na kuleta
tija kwa wanaushirika na jamii kwa ujumla.
Waziri
Hasunga alikuwa Mgeni Rasmi katika Siku Maalum ya Ushirika kwenye Maonesho ya
Nanenane Kitaifa 2019 ambapo alizindua Bima ya Mazao iliyoandaliwa na Wizara ya
Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Bima ya Taifa (NIC). Bima ambayo
itawezesha mkulima, mfugaji na mvuvi kulindwa kwa kupunguza hasara ambayo
anaweza kuipata.
Akizungumza leo Jumamosi, Agosti 03, 2019
katika uwanja wa Maonesho ya Kilimo Nyakabindi – Simiyu kwenye siku maalumu ya
kuhamasisha ushirika kupitia utekelezaji wa programu ya kuendeleza Sekta ya
kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) iliyotengwa kwa
ajili ya kutangaza shughuli za ushirika, mafanikio yaliyopatikana na
kuhamasisha wazalishaji kupitia sekta za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kujiunga na
ushirika. Kutokana na hatua mbalimbali za uboreshaji wa Sekta ya Ushirika idadi
ya vyama hivyo vimeongezeka.
“Hadi
kufikia mwezi Mei, mwaka 2019, nchi yetu ina jumla ya Vyama vya Ushirika 11,331
vyenye idadi ya wanachama 4,611,804 na wanachama tarajiwa 765,804. Idadi hii
imeongezeka kutoka Vyama vya Ushirika 10,990 vyenye wanachama 2,619,311 kwa
mwaka 2018. Hivyo kwa kipindi cha mwaka mmoja jumla ya Vyama vya Ushirika 341
na Wanachama 1,991,960 wameongezeka katika mtiririko huo.” Alisema Hasunga
Pia
aliongeza kuwa hadi kufikia mwezi Februari 2019, Tume ilifanya ukaguzi wa mara
kwa mara kwa vyama vya ushirika 3,140 sawa na asilimia 54 ya lengo la kukagua
vyama 5,830.
Katika
maadhimisho hayo, Waziri Hasunga alitoa vyeti vya utambuzi kwa Vyama vya Ushirika
na Taasisi zenye mchango katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi. Taasisi hizo zilizopata vyeti
hivyo ni pamoja na; Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU), COASCO, FSDT, Mbozi Coffee
Curing Company Limited, TANESCO SACCOS na URA SACCOS.
Akimkaribisha
Mhe. Waziri, kuongea na wakulima pia kuzindua Bima ya Mazao na
kutoa vyeti vya utambuzi kwa mchango wa Vyama vya Ushirika na Wadau katika
maendeleo ya sekta ya Kilimo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew
Mtigumwe amewashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi kwa juhudi zao kubwa katika
uzalishaji wa mazao mbalimbali na alieleza umuhimu wa wazalishaji wa mazao
mbalimbali kupewa kipaumbele na kuhusishwa kwenye masuala ya kilimo na
ushirika.
“Tukio
hili la uzinduzi wa Bima ya Mazao na utoaji wa vyeti kwa Vyama vya Ushirika ni
dhamira dhahiri ya Serikali katika kuhakikisha mkulima, mfugaji na mvuvi
anahusishwa vyema kuendeleza sekta ya kilimo.”
MWISHO
0 comments:
Post a Comment