METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, August 15, 2019

TUTAIMARISHA BIASHARA ZA MAZAO KATIKA NCHI ZA SADC-WAZIRI HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Serikali imesema kuwa imejipanga kuimarisha biashara ya mazao ya Kilimo na mengineyo kwa nchi wanachama wa SADC ili kuwanufaisha wakulima katika nchi hizo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo Leo tarehe 15 Agosti 2019 wakati akizungumza Mubashara (Live) kwenye kipindi cha Clouds 360 kilichorushwa na Clouds TV wakati wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi 16 wanachama wa SADC katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Center.

Amesema kuwa zaidi ya watanzania Milioni 50 nchini wanategemea chakula hivyo lazima kubadili mbinu za uzalishaji katika mazao ya kilimo kwa kuongeza tija kupitia teknolojia mpya ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija.

Mhe Hasunga alisema kuwa Malighafi zinazohitajika zaidi ya Asilimia 66 zinatokana na mazao ya Kilimo hivyo ukamilisho wa serikali ya viwanda unaungwanishwa kwa ukaribu na sekta ya kilimo.

Waziri huyo wa Kilimo Mhe Hasunga, alisema Mkutano wa SADC ni fursa kwa wakulima wa Tanzania kwa kuwa wageni wote waliowasili na watakaoendelea kuwasili watahitaji kula vizuri hivyo mkutano huo ni sehemu ya kuimarisha na kutangaza masoko ya mazao mbalimbali hususani vyakula vya asili.

Aidha, Utoshelevu wa chakula nchini ni asilimia 119 ukilinganisha na mwaka jana ambapo ilikuwa asilimia 124 hivyo serikali imefungua mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi lakini pia ni lazima kuwa na kumbukumbu muhimu za taarifa zote za usafirishaji wa mazao.

Mhe Hasunga alisema kuwa ni wakati wa nchi za Afrika Mashariki na nchi zote za SADC kuanza kutumia masoko ya ndani ya nchi katika mazao ya Kilimo na mengineyo kuliko kutegemea kuagiza katika nchi zingine nje ya Afrika.

Alisema kuwa kufanya hivyo kutaimarisha masoko ya mazao mbalimbali nchini hivyo kuwaimarisha wakulima katika Kilimo chao na kuwa na kipato kikubwa kinachokidhi mahitaji ya kula mkulima ikiwa ni pamoja na uimara wa ucumi wa nchi.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com