WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Serikali ya
Afrika Kusini katika kutimiza azma yake ya kukuza uchumi na kufikia
uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.
Amesema Tanzania inahitaji
uungwaji mkono na Serikali ya Afrika Kusini hususan katika kipindi hiki
ambacho imedhamiria kuimarisha shughuli za uzalishaji kupitia viwanda
kwa lengo la kufikia uchumi wa kati.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Ijumaa, Agosti 16, 2019) wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais wa
Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha
Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro.
Ameyasema kwa kuwa changamoto
zinazoikabili Tanzania katika nyanja mbalimbali zinafanana kwa kiasi
fulani na zile za Afrika Kusini kwani historia za nchi hiyo na jiografia
vinafana na Serikali ya Tanzania.
Akizungumzia kuhusu eneo la
Mazimbu, Waziri Mkuu amesema kuwa lina uhusiano mkubwa na historia ya
nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea vizuri uhusiano kati ya
Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.
Waziri Mkuu amesema eneo la
Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya vuguvugu la ukombozi
wa nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na mapambano dhidi ya ubaguzi wa
rangi nchini Afrika Kusini.
“Mheshimiwa Rais, Tanzania
ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele
(Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana
katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa
rangi nchini Afrika Kusini”.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
kuwa sera za ubaguzi wa rangi zilikoma mwezi Februari 1994 na kufuatiwa
na uchaguzi huru na wa haki uliopelekea kupatikana kwa Rais wa kwanza
mzalendo wa nchi hiyo, Hayati Mzee Nelson Mandela mwezi Mei 1994.
“Tunapoongelea kukoma kwa sera
za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, siku zote tutawakumbuka
Hayati Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyerere na Hayati Mzee Nelson Mandela
kwa utumishi wao uliotukuka kwa kujenga misingi imara ya umoja katika
mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini”.
Amesema misingi imara
iliyojengwa na wazee wetu hao, imekuwa chachu ya ushirikiano kwenye
majukwaa ya Kimataifa hususani katika kupambana na ubaguzi wa kiuchumi
na unyanyasaji wa aina mbalimbali.
Waziri Mkuu amesema namna
pekee ya kuwaenzi viongozi wetu hao ni kuendelea kujenga umoja na
kushirikiana katika kuimarisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC) kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake, Rais
Ramaphosa amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa
ulioutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za kupigania uhuru
wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.
Rais huyo wa Afrika Kusini
amesema Serikali yake ipo tayari kushirikiana na Serikali Tanzania
katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kubadilishana
uzoefu katika maeneo mbalimbali na kukuza teknolojia.
Pia amesema watairisha chuo
cha SUA kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ili kulifanya eneo hilo
kuwa la kisasa. “Tutaboresha na shule katika eneo hili na kuweka
utaratibu wa walimu wake kutembeleana na wa Afrika Kusini kwa ajili ya
kubadilishana uzoefu.”
Rais Ramaphosa aliwasili
katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi na kupokelewa na
Waziri Mkuu. Kisha alitembelea campus ya Solomon Mahlangu na kujionea
maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakikutana na
kupanga mipango mbalimbali.
Pia kiongozi huyo ambaye kwa
mara ya kwanza amefika mkoani Morogoro leo alitembelea campus ya Mazimbu
na kujionea sehemu ambazo waliishi wapigania uhuru wa nchi yake na
kisha aliweka shada la maua kwenye makaburi ya wapigania uhuru.
Ameondoka uwanja wa ndege wa Morogoro na kuelekea jijini Dar es Salaam
saa 1.59 mchana.
0 comments:
Post a Comment