METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 5, 2019

TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA YAPONGEZWA KWA JUHUDI ZA UELIMISHAJI




 Afisa Ushirika Bw. Boniface Moshi akitoa mada ya masuala ya ushirika katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu wakati wa maonesho ya Nanenane


 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa vyama vya Ushirika Bw. Zavery Mkingule akieleza masuala ya ukaguzi wa mahesabu ya vyama vya Ushirika katika maonesho ya Nanenane Kitaifa mkoani Simiyu
 ........................
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara Mhandisi Stella Manyanya amepongeza hatua ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuendesha mafunzo ya ushirika wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.  Mafunzo yanayoendeshwa katika “Kijiji cha Ushirika” ambacho kinaundwa na mabanda ya Tume, vyama vya ushirika, pamoja na wadau wa ushirika. 
Pongezi hizo zimetolewa wakati Mhandisi Manyanya alipotembelea mabanda ya Tume ya Ushirika kwa lengo la kuona na kupata maelezo ya shughuli mbalimbali za sekta ya ushirika nchini. Mafunzo hayo yanatolewa kwa wajumbe wa Bodi za mazao ya kilimo, na watendaji wa vyama vya ushirika.
Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri Manyanya amewasihi wanaushirika kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuongeza wigo wa ajira zinazoweza kuzalishwa kutokana na vyama vya ushirika kama vile ufundi, biashara na viwanda hususan wakati ambapo Serikali ina dhamira ya kuelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025. 
Aidha, Mheshimiwa Manyanya ameshauri umuhimu kwa Bodi na Watendaji kujifunza masuala ya ushirika ili kuendesha vyama hivyo kwa weledi na viwango bora.
“Elimu hii ikalete mabadiliko chanya katika ushirika na niwaombe elimu hii isiishie kwa viongozi tu bali ifike kwa wanachama,” alisema Mhandisi Manyanya.    
Awali akizungumzia ratiba ya mafunzo kwenye maonesho hayo, Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Bw. Charles Malunde amesema Tume inatumia fursa hiyo kutoa mafunzo katika siku zote za maonesho kwa watendaji na viongozi wa vyama vya ushirika kutoka maeneo mbalimbali. 
“Mafunzo haya yanatoa fursa ya  kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa vyama kwa kuwakutanisha vyama vya ushirika,  taasisi na wadau wa ushirika kama vile Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa vyama vya Ushirika (COASCO) pamoja na Shirikisho la vyama vya Ushirika (TFC),”alisema Bwana Malunde.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ukaguzi wa vyama vya ushirika (COASCO), Bwana Zavery Mkingule alitoa mada katika mafunzo hayo huku akieleza masuala mbalimbali kama vile majukumu ya COASCO, uandaaji wa taarifa za fedha, Utawala Bora na taratibu za uongozi ndani ya vyama vya ushirika. Mkengule alifafanua kwamba ni muhimu vyama vya ushirika kufanyiwa ukaguzi na kupata hati ya ukaguzi.
“Hati ya ukaguzi ni maoni ya mkaguzi yanayotoa picha juu ya taarifa za fedha alizokagua kama zinaonesha hali halisi au sivyo. Kuonesha hali halisi maana yake ni kwamba taarifa za fedha zimeandaliwa kulingana na viwango vya uhasibu vilivyokubalika na pia taarifa hizo hazina makossa yoyote makubwa au ubadhilifu na hivyo kutopotosha picha halisi,” alisema Bwana Mkingule.
Bwana Mkingule alibainisha kuwa zipo aina nne za hati zinazotolewa na mkaguzi kulingana na taarifa za fedha kuwa hali halisi au sivyo kulingana na ukubwa wa tatizo atakalokuwaamelibaini Mkaguzi, akizitaja hati hizo ni hati inayoridhisha, hati yenye shaka, hati isiyoridhisha na hati mbaya.
Aakitoa mada kwa Wajumbe wa Bodi na watendaji wa vyama vya ushirika kutoka Simiyu, Mwanza na Shinyanga, Afisa Ushirika, Bwana Boniface Moshi, alibainisha masuala mengi pamoja na mihimili muhimu ya vyama vya ushirika kuwa ni Wanachama, Bodi za vyama na Watendaji. Masuala mengine yaliyojadiliwa katika mada hiyo ni Utawala Bora, uandishi wa taarifa za fedha, majukumu ya Bodi, haki na wajibu wa mwanachama. na kusisitiza kuwa ni muhimu wanachama kufuatilia vyama vyao kwakuwa maamuzi ya chama ni ya wanachama wenyewe.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mjumbe wa Bodi kutoka chama cha Jojababi Shinyanga, Bi. Amina Malale alisema kuwa mafunzo hayo yamemuongezea maarifa hususani katika masuala ya utendaji na uongozi katika chama cha ushirika. Hivyo, mafunzo hayo yamemuhamasisha kwenda kufanya kazi kwa tija zaidi na kuhamasisha wakulima na wazalishaji ambao bado si wanaushirika kujiunga na vyama vya ushirika ili kunufaika na kupambana na umaskini kupitia nguvu ya pamoja ya vyama vya ushirika.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com