Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wachimbaji wa madini katika
migodi midogo midogo kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo
linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi na maporomoko migodini katika
kipindi hiki cha mvua za msimu.
Mkurugenzi
Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu utabiri wa mvua za msimu wa Novemba mwaka
huu hadi Aprili mwakani.
Pia
imezitaka mamlaka za miji pamoja na wananchi, kuchukua tahadhari kwa
kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi katika
kiwango cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na
uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.
Akizungumzia
mwelekeo wa mvua za msimu, Dk Kijazi alisema kutakuwa na mvua za
wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi yanayopata msimu moja wa
mvua kwa mwaka, na kwamba mvua kubwa inatarajiwa Januari mwakani.
“Msimu
huu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati,
nyanda za juu Kusini Magharibi, kusini mwa nchi, maeneo ya kusini mwa
mkoa wa Morogoro pamoja na Ukanda wa Pwani ya Kusini.
Mvua
inatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya Novemba na kuisha wiki ya nne ya
Aprili, 2018,” alieleza Dk Kijazi. Alisema Kanda ya Kati kwenye mikoa ya
Singida na Dodoma, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na
ya pili ya Desemba mwaka huu, zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya
wastani katika maeneo mengi.
Kwa
Nyanda za Juu Kusini Magharibi na maeneo ya Kusini mwa nchi, mvua
zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Novemba na wiki ya kwanza ya Desemba.
Alisema Pwani ya Kusini kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara mvua
zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Novemba na wiki ya kwanza ya
Desemba.
Dk
Kijazi aliwataka watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ambao ni
wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyama pori, mamlaka za maji na afya
waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta
husika.
0 comments:
Post a Comment