Na Dennis Buyekwa,MAELEZO
DAR ES SALAAM
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Job Ndugai ametoa wito kwa Serikali
kuendeleza utalii wa Pwani ya Bahari ya Hindi, hatua itakayosaidia
kuchochea ukuaji wa utalii nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jengo la
tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jana
alhamisi (Agosti Mosi, 2019), Ndugai alisema Tanzania ina kila sababu ya
kuendeleza fukwe hizo kutokana na ukweli kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi za
fukwe na bahari zilizo bora kuliko nchi yoyote ndani ya bara la Afrika.
Spika Ndugai aliongeza kuwa uendelezaji wa
fukwe hizo utasaidia nchi kwa kiasi
kikubwa kupiga hatua na kuifanya
Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Sisi hapa Tanzania tuna pwani ya bahari nzuri
zaidi kuliko pwani zingine popote pale Afrika, hizi ni hifadhi za mwambao wa Pwani
ya Bahari ya Hindi, kuanzia Pangani mpaka Mtwara ambazo hazijatumika vizuri.” Alisema
Spika Ndugai
Aidha Spika Ndugai aliongeza fukwe hizo zikitumika vizuri zitasaidia
kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kuoanishwa vizuri kwa
utalii wa pwani na ule wa bara na hivyo kuifanya sekta ya utalii kuongeza wigo
mwingine wa mtandao wa mapato nchini.
Akizitaja sababu zilizopelekea utalii
kutoonekana vizuri, Spika Ndugai alisema moja ya sababu kubwa inayochangia sekta
ya utalii kutokufanyika vizuri ni kwa kuwa utalii wa
fukwe za bahari bado uko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Aidha katika kuonyesha umuhimu wa kuendeleza
fukwe hizo, Ndugai aliyataja maeneo ya Mombasa, Lamu na Malindi nchini Kenya kama
maeneo ambayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendeleza fukwe katika Pwani zao,
ambapo zimesaidia kuchochea ongezeko la watalii katika maeneo hayo.
“Kwenye Pwani zao kwa sasa kuna utalii maarufu
unaofanyika baharini, unaofahamika kama ‘Marine
Parks tourism’, ndio maana ukiangalia Pwani yao imejaa hotel, na sisi hapa
kwetu tukitumia fukwe zetu vizuri tunaweza kuwa na utalii mzuri zaidi wa namna
hii utakaosaidia kuongeza idadi ya watalii nchini”. Alisema Spika Ndugai.
Pia Spika Ndugai alimshukuru Rais Dkt. John Magufuli
kwa kuamua kuipandisha hadhi iliyokuwa sehemu ya pori la akiba la Selous Game Reserve’
kuwa hifadhi kamili itakayojulikana kama Hifadhi ya Taifa ya Nyerere au ‘Nyerere National Park’.
Akizungumzia kuhusu suala hilo Rais Magufuli
alisema pendekezo la kuendeleza
fukwe za pwani ya Bahari ya Hindi ni moja
ya vipaumbele vya Serikali kwa sasa, na kumuagiza Waziri Mkuu , Kasim
Majaliwa kuangalia jinsi ya kuendeleza fukwe zote kuanzia Moa hadi Msimbati.
0 comments:
Post a Comment