………………….
Na Munir Shemweta, WANMM MKINGA
Serikali
imefuta miliki ya Mashamba matatu ya Mkomazi Plantantions maarufu MOA
yaliyopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya
uendelezaji ikiwemo kutelekezwa bila kufanyiwa maendelezo yaliyokusudiwa na kutolipiwa kodi ya pango la ardhi.
Uamuzi
huo umetangazwa leo tarehe 30 Agosti 2019 na Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipozungumza na wananchi wa
Mayomboni wilayani Mkinga mkoani Tanga alipokwenda kutatua mgogoro wa
muda mrefu katika eneo hilo.
Mashamba yaliyofutiwa ni lenye hati Na 9780 na ukubwa wa ekari 14,688, shamba Na 4268 ekari 804 na Shamba lenye Hati Na 9781 ekari 246 ambapo mashamba yote matatu yana ukubwa wa ekari 15,738.
Kufuatia
uamuzi huo, jumla ya vijiji kumi vyenye kaya 3,236 zilizo na wakazi
16,450 zitanufaika na uamuzi wa serikali kutokana na wananchi wake
kuvamia mashamba hayo na kufanya maendelezo ya kujenga makazi, shule
pamoja na kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya kudumu na ya muda
mfupi.
Vijiji
vilivyonufaika ni uamuzi wa Serikali kufuta mashamba ya Mkomazi
Plantations ni kijiji cha Kilulu-Dunga, Zingibari, Mwaboza, Mwakikoya,
Mhandakini, Nkanyeni, Sigaya, Mayomboni, Ndumbani pamona na kijiji cha
Moa
Akizugumza
wakati wa kutangaza uamuzi huo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi amesema uamuzi wa kufuta mashamba hayo matatu
unafuatia maombi yaliyotumwa kwa Raisi John Pombe Magufuli ya kutaka
kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa
muda mrefu.
Alisema,
Rais ameridhia maombi hayo kwa kuwa serikali imekuwa ikisisitiza
utekelezwaji wa sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 ikiwemo uendelezaji
wa mashamba ambayo yamemilikishwa sehemu mbalimbali nchini.
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza kufanyika upimaji
katika vijiji vyote kumi vilivyopo ndani ya shamba hilo sambamba na
kuanishwa miapaka ya vijiji hivyo na kupatiwa hati ambapo alitaka
wananchi wanaishi kwenye vijiji hivyo kutobughudhiwa.
Aidha,
Waziri Lukuvi alitaka maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya uwekezaji katika
shamba yaliyofutwa kuachwa kwa ajili ya shughuli hiyo ikiwemo
muwekezaji wa Katani Azka International Tanzania mwenye ekari mia tano
pamoja na maeneo ya viwanda kama kile cha kuzalisha chumvi na kusisitiza
kuwa serikali inataka uwekezaji utakaotoa ajira kwa vijana na wakati
huo kupata mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.
Katika hatua nyingine
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza
kufanyika uhakiki wa mashamba mengine ya Kwa Mtili Estates Co Ltd
yaliyopo Mkinga mkoani Tanga ambapo ekari 58 pekee ndizo zilizoombwa
kufutwa kwa Rais kutokana na kutoendelezwa huku mmili wake ikidaiwa
kumiliki ekari 2,841.
Hatua
hiyo inafuatia Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika halmashauri
ya wilaya ya Mkainga Obed Katonge kueleza kuwa, Kwa Mtili Estates Co Ltd
inalo shamba la lenye ukubwa wa ekari 2,841 tofauti na inavyoonekana
katika kumbukumbu za ofisi ya Msajili wa Hati Kanda ya Kaskazini ambazo
ni 58.
Lukuvi
aliagiza wataalamu wa ardhi kutoka Kanda ya Kaskazini kufanya uhakiki
huo katika kipindi cha mwezi mmoja na kumpa taarifa ya uhakiki huo
mwisho wa mwezi Septemba 2019 na kufafanua kuwa pale itakapothibitika
kuna ujannja uliofanyika wa kumuongeza mmiliki wa shamba hilo hatua kali
zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Mbunge
wa Jimbo la Mkinga mkoani Tanga Dustan Kitandula aliishukuru serikali
ya awamu ya tano kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi
wanaoishi eneo la shamba lililofutwa la kutaka kurejeshewa ardhi yao
waliyokuwa wakiutumia kwa shughuli mbalimbali.
Alisema,
mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa mkinga na wamiliki wa mashamba ya
Mkomazi Plantantions Co Ltd umekaa kwa muda mrefu na kuwafanya wananchi
kuwa na ndoto isiyokuwa na majibu lakini uamuzi uliotolewa na Serikali
umewafanya kuishi kwa furaha na amani .
0 comments:
Post a Comment