Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipiga Push Up na wasanii wa Tanzania
One Theatre (TOT) wakati wa sherehe ya ufunguzi rasmi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Alhamisi
Agosti 1, 2019
………………………………………………..
RAIS Dkt. John Magufuli amesema
Tanzania imeamua na ina uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya
maendeleo nchini pasipo kutegemea fedha zenye masharti zinazotolewa
kutoka kwa wafadhili na wadau wa kimataifa wa maendeleo.
Akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa Jengo la 3 la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi (Agosti 1, 2019), Rais Magufuli
alisema uzinduzi wa Jengo la Uwanja huo ni ushahidi wa wazi wa usimamizi
na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali zinazotokana na kodi ya
wananchi.
Aliongeza Jengo la Uwanja huo
limejengwa kwa asilimia 100 kutokana na kodi za Watanzania, na hivyo
kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala wa
Barabara Nchini (TANROAD) kusimamia vyema miundombinu ya Uwanja huo kwa
kuhakikisha kuwa inatunzwa ili kuakisi vyema taswira ya Jiji la Dar es
Salaam na Watanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli
alisema jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia jumla ya abiria
Milioni 6 kwa mwaka limeigharimu Serikali kiasi cha Tsh Bilioni 722
ambazo ni fedha zilizotolewa na Serikali, limeweza kuifanya Serikali
kuaminika na kuwa na udhubutu wa kutekeleza miradi ya Maendeleo kupitia
fedha za ndani.
“Ipo miradi mingi ya Maendeleo
tunayoisimamia kwa fedha zetu za ndani ikiwemo Ujenzi wa reli ya kisasa,
mradi wa kufua umeme Mto Rufiji, Barabara za Juu Ubungo, Daraja la
Kigongo-Busisi, Daraja la Salender, Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya
ndege 15, kujenga rada 4 katika Viwanja vya Ndege vya Dar Salaam,
Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, huu ni ushahidi wa usimamizi imara wa
fedha zetu za ndani” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema
kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya anga nchini,
kwa kuwa sekta hiyo imekuwa kiungo muhimu katika maendeleo ya sekta ya
Utalii, kwani kila siku takribani watu Milioni 12 duniani hutumia
usafiri wa anga kutokana na kuwa njia ya haraka na ya uhakika kwa ajili
ya usafirishaji wa abiria na mizigo.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli
aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutoa kipaumbele kwa
makampuni ya kitanzania yanapewa nafasi katika maduka yatakayofunguliwa
ndani ya Uwanja huo ili kuwawezesha kufaidi matunda ya kodi yao sambamba
na kuweza kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa
mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema
tangu mwaka 2004-2011 Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa ajili ya
kuimarisha miundombinu ya majengo ya Uwanja wa ndege vyaJulius Nyerere
ikiwemo ujenzi wa Jengo jipya la tatu la abiria katika uwanja huo,
kutokana na majengo ya sasa ya jengo la I na II kukabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo uwezo mdogo wa kuhudumia abiria.
Anaongeza kuwa ujenzi wa Jengo
hilo la tatu la abiria lilisimama ujenzi wake mwaka 2016 kutokana na
mkandarasi kudai Tsh Bilioni 29, ambapo awali alishapokea kiasi cha Tsh
Bilioni 380 kati ya Tsh Bilioni 560 zilizohitajika kwa ajili ya
ukamlishaji wa jengo hilo hapo awali, lakini mwaka 2017 Serikali ilitoa
zabuni ya ujenzi wa mradi huo kwa mkandarasi mwingine kutokana
mkandarasi aliyepita kuwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mfugale
alisema kutokana na kasoro zilizojitokeza, shughuli za ujenzi wa jengo
hilo zilipelekwa kwa kampuni ya TECU na mshauri mwelekezi kampuni ya
Arab Contractor ambapo hadi kufikia Mei 29 mwaka huu zilikamilisha
ujenzi wa jengo hilo na kusubiri kukabidhiwa kwa Serikali kwa ajili ya
kuanza kutumika kwake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama alisema
hadi kufikia sasa jumla ya makampuni 18 kati ya 23 ya kimataifa tayari
yamehamishia shughuli zao katika Uwanja huo kwa ajili ya kuanza kutoa
huduma za usafiri kwa abiria wanaosafiri kwenda nje ya nchi.
Aliongeza kuwa katika kuimarisha
usimamizi bora wa Jengo la Uwanja huo, Mamlaka hiyo pia imewapatia
mafunzo watumishi wake kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja wa namna
bora ya kulinda miundombinu ya Uwanja huo na hadi sasa imepokea Tsh
Milioni 500 kutoka Serikalini ilizozilipa kwa mkandarasi wa ujenzi wa
mradi huo kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.
0 comments:
Post a Comment