Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, William Ole Nasha amemtaka Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani (NECTA) kushirikiana na TAMISEMI pamoja na viongozi wa Mkoa wa
Tanga kufanya uchunguzi wa wizi wa mitihani ambao umefanyika katika
miaka ya nyuma wilayani Kilindi.
Naibu Waziri ametoa agizo hilo
alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu
wilayani humo ambapo amesema uchunguzi huo ufanywe ili kujiridhisha
kwamba wizi huo wa mitihani hauendelei kwani haipendezi kuwa na vijana
wasomi wazuri ambao wamefaulu kwa njia za udanganyifu.
Ole Nasha amesema yeye kama
msimamizi wa sera na sheria, suala la uvunjifu wa sheria na wizi wa
mitihani haliwezi kumfurahisha kwani jambo hilo ni kosa. Amesema
inasikitisha kuona wizi huo umefanyika na viongozi wanafahamu lakini
hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wa wizi huo wa
mitihani.
Aidha, Naibu Waziri amesema wilaya
hiyo haijakaa vizuri kitaaluma kwani katika matokeo ya mitihani ya
kidato cha nne ya mwaka 2017 kuelekea 2018 ufaulu ulishuka kutoka
asilimia 85 mpaka 55. Amesema anguko hilo ni kubwa ambalo kama ukiwa
msimamizi wa elimu linashtua na hivyo kuhitaji kujua sababu ya anguko
hilo ili kuweza kuchukua hatua za kusaidia kutoka katika hali hiyo.
“Kwa bahati mbaya sababu ambazo
mmezitoa si nzuri, ukisikia kwamba sababu tumezuia walimu wasitoe majibu
kwa wanafunzi hiyo sio sababu kwani hilo ni kosa katika sheria hii.
Inamaanisha kwamba Kilindi mitihani imekuwa ikiibiwa, viongozi wanajua
na hakuna hatua zinazochukuliwa,” amesema Ole Nasha.
Amesema usimamizi wa elimu katika
wilaya ya Kilindi si mzuri na amemtaka Afisa Elimu wa Mkoa wa Tanga
kuhakikisha anaangalia changamoto zilizopo katika wilaya hiyo na kuona
namna ya kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo.
Aidha, Ole Nasha amesema Serikali
imepeleka fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya ujenzi wa mindombinu
katika wilaya hiyo na amesisitiza kuwepo na usimamizi mzuri wa fedha
hizo na kusisitiza kwamba fedha hizo zinapelekwa katika wilaya kwa ajili
ya kuboresha elimu hivyo haipendezi zisitumike kufanyia kazi
iliyokusudiwa ama kuchelewesha kutekeleza miradi.
Naibu Waziri huyo ameonyesha
wasiwasi wa kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya
kuanzishwa kidato cha tano katika shule za Mafisa na Kikunde ambao fedha
zake zilitumwa toka mwezi wa kwanza na kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo,
Sauda Mtondoo kufuatilia sababu za ucheleweshaji wa mradi huo pamoja na
kujihakikishia ukweli wa taarifa iliyotolewa kuhusu ujenzi huo ili
kujiridhisha.
Naye Mtondoo akitoa taarifa ya
Sekta ya Elimu katika wilaya hiyo iliyoonesha kushuka kwa kwa ufaulu
katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2017 kuelekea
2018, amesema kushuka huko kulitokana na kuzibwa mianya ya udanganyifu
na wizi wa mitihani uliokuwa ukiendelea katika wilaya hiyo kwa miaka
mingi.
Mtondoo amesema sababu nyingine ni
kuwepo kwa mgomo baridi uliokuwa ukifanywa na walimu wa wilaya hiyo
kutokana na kutotekelezewa madai yao ikiwemo kutopandishwa madaraja
jambo ambalo wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi
wamelitatua na walimu sasa wameacha mgomo huo.
Aidha, Mbunge wa Kilindi, Omari
Kigua amekiri kuwepo kwa tabia ya walimu kuwapa wanafunzi majibu ya
mitihani na kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye baada ya
kufika Kilindi na kuona tatizo hizo la wizi wa mitihani aliweka mikakati
ya kuhakikisha mianya hiyo inazibwa ili kuzuia wizi huo.
“Ni ukweli usiopingika kwamba wizi
wa mitihani ulikuwepo, Kilindi tunataka kupata wasomi wazuri na si
wasomi wa wizi wa mitihani, hatuwezi kuficha ukweli kwamba walimu
walikuwa na tabia hiyo. Ni ngumu kuamini kwamba kuongeza usimamizi wa
mitihani ndo sababu ya kufeli kwa wanafunzi,” amesisitiza Kigua.
0 comments:
Post a Comment