Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha
amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Morris Limbe kumlipa fedha
Mkandarasi anayekarabati shule ya sekondari Bukoba ili aweze kuendelea
na kazi na kukamilisha ukarabati huo kwa wakati
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo
mkoani Kagera wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya
elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia ilishapeleka fedha zote za ukarabati huo kiasi cha
shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa mkandarasi huyu amelipwa kiasi
cha shilingi milioni 32 tu.
“Fedha zilishaletwa zote na wizara
shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa Mzinga wamelipwa shilingi milioni
32 tu kati ya milioni mia mbili na zaidi walizotakiwa kuwa wamelipwa
mpaka sasa, hivyo Mkurugenzi wa manispaa dirisha likifunguliwa hakikisha
Mzinga wanapata fedha ambazo wanadai” amesisitiza Ole Nasha.
Ole Nasha amesema ukarabati wa shule hiyo
unaoendelea umechelewa kukamilika kwani licha ya fedha hizo kupelekwa
mapema mkandarasi amechelewa kuanza kufanya ukarabati huo. Hata hivyo
amesema kasi ya ujenzi huo si mbaya kutokana na kuanza mwezi wa tano.
Aidha, Ole Nasha amewataka watendaji wa
manispaa hiyo kufuatilia kwa ukaribu matumizi ya fedha hizo kwani ni
nyingi kutumika kwa ukarabati ukilinganisha na fedha zinazotumika katika
miradi mingine, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa fedha kubaki na kutumika
katika kufanya shughuli nyingine za kuboresha mazingira ya kufundishia
na kujifunzia.
“Nikifananisha fedha ambazo tumetumia
kwenye maeneo mengine na miradi mingine mfano miradi ya afya ambao
wanatumia bilioni 1.5 kujenga hospitali kubwa kwa kujenga majengo mapya
makubwa saba lakini sisi hiyo bilioni 1.4 ambayo inakaribiana na bilioni
1.5 ya afya tunakarabati majengo tu, kuna umuhimu wa kuzisimamia fedha
hizi kwa ukaribu,” alisema Ole Nasha.
Aidha, Naibu Waziri amesema shule hiyo
ina nafasi finyu ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi mia saba
waliopo na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo kuwasiliana na Wakala wa Majengo ya
Serikali (TBA) ambao wana eneo karibu na shule hiyo washaurine juu ya
uwezekano wa kutoa eneo hilo kwa ajili ya upanuzi wa shule hiyo.
Awali Mkuu wa shule ya Sekondari Bukoba,
Raymond Mutakyawa, amemweleza Naibu Waziri kuwa ukarabati wa shule hiyo
ulikuwa ufanyike kwa siku sabini tano na ulipaswa kuwa umekamilika
mwishoni mwa mwezi wa saba lakini ulisimama kutokana na kukosa fedha za
kununua vifaa kwa ajili ya kazi hiyo baada ya mfumo wa malipo kufungwa
kabla ya fedha hizo kulipwa kwa mkandarasi.
Shule ya Sekondari ya Bukoba inafanyiwa
ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kuharibiwa
na tetemeko la ardhi la mwaka 2016 lililoikumba mkoa wa Kagera ambapo
baadhi ya kuta za shule hiyo zilianguka na majengo mengine kupata nyufa
na baadae paa kuezuliwa na upepo mkali.
0 comments:
Post a Comment