Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),
Dkt. James Mataragio (kushoto) akikagua maendeleo ya ujenzi wa
miundombinu ya gesi asilia kuwaunganishia wateja wa viwanda maeneo ya Mkuranga,
Mkoa wa Pwani, hivi karibuni.
....................
Na Veronica Simba – Dodoma
Serikali imebainisha kuwa matumizi ya gesi asilia katika magari nchini
yamezidi kukua ambapo kwa sasa idadi imefikia 210 kutoka 65 yaliyokuwa
yakitumia nishati hiyo, mwaka 2017.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio, jijini Dodoma, leo Agosti 21,
2019 wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini, kuhusu hatua zilizofikiwa katika kuandaa moduli ya miradi ya bei ya
gesi asilia, uuzaji na usambazaji wake majumbani na viwandani.
Akieleza zaidi, Dkt. Mataragio alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo,
kituo cha majaribio kilichopo Ubungo Dar es Salaam, kinashindwa kuhimili
matakwa ya matumizi hivyo shirika limejipanga kujenga kituo kikubwa eneo la Sam
Nuyoma jijini humo, ili kuondoa changamoto husika.
“Kituo hicho kinachotarajiwa kukamilika Oktoba 2020, kitatumika kujazia
gesi katika magari pamoja na kupeleka gesi maeneo ambayo miundombinu ya mabomba
ya gesi bado haijafika, yakiwemo maeneo ya viwanda Kigamboni na Kibaha pamoja
na maeneo ya Feri na Muhimbili.”
Aidha, alieleza kuwa, sambamba na ujenzi wa kituo husika, shirika
limetangaza fursa kwa kampuni binafsi kuuza gesi kwa rejareja kwa watumiaji wa
nishati hiyo katika magari nchini. Aliongeza kuwa, jumla ya shilingi bilioni
16.6 zimetengwa kwa ajili ya vituo vya kuongeza mgandamizo wa gesi (CNG) na
kujazia gesi katika magari.
Ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za uwezeshaji matumizi ya gesi katika
magari nchini, Dkt. Mataragio alisema TPDC inalenga kuupatia gesi asilia mradi
wa mabasi ya mwendokasi (DART), ambapo kwa kuanzia, kituo cha kujazia gesi
kwenye magari kitajengwa eneo la DART, depoti ya Ubungo na kinatarajiwa
kukamilika Oktoba, mwakani.
Alisema, shirika limekubaliana na DART kuwezesha kuweka vituo maalumu
vya gesi katika depoti ya Gongo la Mboto na Mbagala ili kupunguza gharama za
uendeshaji wa miradi ya DART na kuongeza matumizi ya gesi asilia.
“Miundombinu hii pia itakuwa na matoleo ya kuwezesha usambazaji wa gesi
asilia kwa matumizi ya viwanda na majumbani katika maeneo mbalimbali ya Dar es
Salaam,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mikakati mingine inayofanywa na shirika hilo katika
kuwezesha ongezeko la matumizi ya gesi asilia nchini, Dkt. Mataragio alisema
TPDC imepanga kuendeleza miundombinu ya usafirishaji gesi asilia ikiwemo
kujenga bomba la gesi kutoka Tegeta hadi Bagamoyo katika eneo la viwanda.
Aidha, alisema shirika limepanga kujenga bomba la gesi kutoka Dar es
Salaam hadi Tanga ambalo litakuwa na matoleo ya kwenda mikoa mingine pamoja na
nchi za jirani kulingana na Mpango kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Nchini
(NGUMP).
Katika uwasilishaji huo wa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Ujumbe wa serikali uliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalu. Wengine walioshiriki ni viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka
wizarani, TPDC na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara.
0 comments:
Post a Comment