Baadhi ya kinamama wanaonyonyesha
wakipita kwa maandamano maalum mbele ya mgeni rasmi katika uzinduzi wa
maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji iliyofanyika katika kijiji cha
Kisumba Wilayani Kalambo.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said
Mtanda akiongea mbele ya wananchi walioweza kuhudhulia katika uzinduzi
wa maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji iliyofanyika katika kijiji cha
Kisumba Wilayani Kalambo.
************
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said
Mtanda amewatahadharisha kinababa wenye tabia ya kunyonya maziwa ya
kinamama wanaonyonyesha kwani hicho ni chakula maalum kwaajili ya mtoto
aliyezaliwa na yeyote anayefanya hivyo anadhulumu haki ya mtoto ambaye
hutegemea maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita bila ya kula chakula cha
aina yoyote.
Amesema kuwa kazi kubwa ya
kinababa ni kuwawezesha kinamama kupata lishe bora ili wawe na afya
thabiti kutoa maziwa ya kutosha na kuweza kuwanyonyesha watoto wao na
kuongeza kuwa katika mkoa wa Rukwa asilimia 81 ya watoto wenye umri
chini ya miezi sita wanalishwa vyakula vingine vya ziada, jambo ambalo
halikubaliki kwa maendeleo ya mtoto.
“Ujumbe wa Leo ni kwamba watoto
wadogo chini ya Miezi Sita ndio wanaotakiwa kunyonyeshwa, kwahiyo
kinababa na wao wenye kupenda maziwa ya baba waache kwasababu hicho sio
chakula chao ni lishe kwa watoto wachanga, tusidhulumu haki za watoto za
unyonyeshaji, tuache tabia ya kunyonya maziwa ya mama kwa wasiohusika,”
Alisisitiza.
Aidha alisema kuwa tafiti
zinaonesha kuwa asilimia 17 ya watoto wenye umri chini ya miezi 6
wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa kinywaji au chakula
kingine kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani. Hii ina maana
kuwa asilimia 83 ya watoto wenye umri huo hawanyonyeshwi ipasavyo.
Mh. Mtanda aliyasema hayo katika
uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji kimkoa katika Kijiji cha
Kisumba, kilichopo Wilaya ya Kalambo akimwakilisha aliyetakiwa kuwa
mgeni rasmi wa uzinduzi huo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu
Tawala wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya aliisifu timu ya afya ya Mkoa kwa
kuwezesha kufanyika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji
katika Kijiji cha kisumba kutokana na Kijiji hicho kuwa na kinamama
wengi wanaonyonyesha.
“Katika Kijiji hiki Mheshimiwa
mgeni rasmi kuna Kaya 1300, na kwa takwimu ambazo tunazo kupitia idara
yetu ya afya kinamama wanaonyonyesha watoto katika Kijiji hiki cha
Kisumba ni 234, hivyo utaona kwamba tumekuja kuhakikisha kuwa ujumbe huu
unafika kwa wadau kwa njia muafaka,” Alieleza.
Halikadhalika alisema kuwa
maadhimisho hayo yankwenda sambamba na utekelezaji wa mradi wa Lishe
Endelevu unaolenga kuongeza idadi ya watoto wenye umri kati ya miezi 6 –
23 kuhakikisha kwamba wanapata vyakula vyenye mchanganyiko sahihi na
kusisitiza kuwa ni muhimu kinababa kushiriki katika maadhimisho hayo ili
wawe msaada mkubwa kwa kinamama.
Wakati akitoa neno la Shukrani
Meneja wa Mradi wa Lishe Endelevu Ali Omar alishukuru ushirikiano
anaoupata kutoka serikalini na kuwasisitiza kinamama kuwa unyonyeshaji
wa maziwa ya mama huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha afya,
kulinda uhai na maisha ya mtoto.
Asilimia 67 ya watoto wa umri
kuanzia miezi 6 – 23 wanapewa vyakula ambavyo havina mchanganyiko wa
kutosha, yaani mlo usiokamilika, hali inayodhihirisha kuwa, taratibu
duni za ulishaji watoto ni mojawapo ya sababu za utapiamlo katika Mkoa
wa Rukwa.
0 comments:
Post a Comment