
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa akizungumza na wananchi katika viwanja
vya Shule ya Msingi ya Nanganga wilayani Ruangwa, Julai 27, 2019. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Afisa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa anayeshughulikia elimu ya
msingi, Bw. Selemani Mrope atafute walimu wawili kutoka Ruangwa na
kuwahamishia kata ya Nanganga mara moja.
“Lazima kuna walimu wamejazana
pale Ruangwa mjini, leo tukitoka hapa nenda kaandike barua za uhamisho.
Kesho Jumapili, wahusika wapewe barua zao na Jumatatu waje kuripoti
hapa Nanganga,” amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe miongoni mwa
wakazi wa Nanganga.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumamosi, Julai 27, 2019) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha
Nanganga, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi alipopita kuwasalimia wakazi
hao.
Waziri Mkuu ambaye amewasili
Lindi leo kwa mapumziko mafupi, alipokea taarifa ya shule ya msingi
Nanganga ambayo ilionesha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 237 ina walimu
sita tu. Kati ya hao, wavulana ni 124 na wasichana ni 113.
“Shule hii ina madarasa nane
likiwemo darasa la awali, masomo yanayofundishwa ni tisa, mkibaki na
walimu hawa sita, mzigo unakuwa mkubwa kwa walimu hawa waliopo. Afisa
Elimu tafuta wawili walimu waje hapa Jumatatu, na Mkurugenzi wa
Halmashauri atakupa gari ya kuwahamishia hapa,” amesema. Shule ya msingi
Nanganga, iliyoko kata ya Nanganga, iko umbali wa km. 59 kutoka Ruangwa
mjini.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge
wa Ruangwa, amewataka wakazi wa kata hiyo wafikirie kuanza ujenzi wa
shule ya sekondari yao ya kata ili kuwapunguzia safari wanafunzi wa
kijiji hicho ambao kwa sasa wanalazimika kwenda kusoma Nangumbu, iliyoko
umbali wa km. 10.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa sh.
milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambayo yakikamilika
walimu watapata ofisi pia.
Amesisitiza kwamba fedha hizo zitumike kujenga madarasa manne ambapo walimu pia watapata ofisi moja.
Pia amemwambia diwani wa kata
ya Chinongwe, Bibi Maki Camillius kwamba katika bajeti ya mwaka huu,
kata hiyo itapatiwa sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za
walimu katika shule ya sekondari ya kata ya Chinongwe.
Mapema, akisoma taarifa mbele
ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Amiri Musa Kambona
alisema madarasa mawili na ofisi moja ya walimu vilibomoka mwaka 2014
kutokana na mvua na upepo mkali na kusababisha upungufu wa madarsa na
ofisi.
Akielezea changamoto nyingnea
za shule hiyo, Mwalimu Kambona alisema shule ina upungufu wa nyumba
moja ya walimu, darasa moja, matundu mawili ya vyoo vya walimu, ofisi
moja ya walimu na kukosekana kwa chanzo cha maji safi na salama kwa
matumizi ya wanafunzi na walimu.
0 comments:
Post a Comment