METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 24, 2019

TAKUKURU DODOMA YAWANASA MTENDAJI NA MGAMBO KWA RUSHWA

Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma,Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa jinsi Takukuru ilivyoweza kuwakamata Mtendaji Kata na Mgambo wakiomba Rushwa.


……………………..

Na.Alex Mathias,Dodoma

Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma,Sosthenes Kibwengo,amewataka watendaji wa Kata mitaa na vijiji kuacha tabia ya kuomba rushwa kwa jamii ili waweze kuwasaidia kutatua matatizo yanayowakabili,badala yake wafanye kazi kulingana na maadili.

Hayo ameyasema leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake akitoa taarifa ya kukamatwa kwa mtendaji wa kata ya Mlowa Bwawani iliopo wilaya ya Chamwino jijini Dodoma, Luis Pearson na Mgambo Josephat Msambili wakiomba rushwa ya sh laki Nne kwa mahabusu Samwel Chilulumo.

Kibwengo amesema kuwa watuhumiwa hao walimkamata Chilulumo mkazi wa kijiji cha Wiliko na kumweka mahabusu ya Kata kutokana na kosa la ugomvi wa kifamilia na kumtaka awape rushwa ya sh laki sita ili mwachie huru,ambapo mahabusu huyo aliomba apunguziwe kiasi hicho cha fedha na kufikia sh laki nne.

Aidha amesema kuwa baada Chilulumo kuomba apunguziwe kiasi hicho aliomba atolewe mahabusu ili akatafute fedha hizo lakini alikataliwa na watuhumiwa kuamua kwenda kutafuta mteja wa mbuzi 10 zilizokuwa nyumbani kwake ili ziuzwe kiasi hicho kipatikane ndipo aachiwe huru.

“Baada ya kupata taarifa TAKUKURU ilifanya uchunguzi na kubaini kuna vitendo vya rushwa na kuanza kulifanyia kazi suala hilo na kuwabaini watuhumiwa hao,”amesema Kibwengo.

Hata hivyo Kibwengo amesema baada ya uchunguzi wao, walibaini mtuhumiwa Msambili alikwenda kutafuta mnunuzi wa mbuzi na kumpeleka mahabusu kwa ajili ya kufanya majadilianoya bei na Chilulumo ambaye alikuwa mahabusu,ndipo wakarejea nyumbani kuona mbuzi na kisha kurejea tena mahabusu ndipo wakakubaliana bei.

“Hivyo nawaomba  watendaji waache kufanya vitendo hivyo kwa sababu ni kinyume na kifungu cha 15 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007,”alisema Kibwengo.

Amefafanua kuwa baada ya uchunguzi walipokubaliana imethibitika
mnunuzi alitoa kiasi cha fedha hizo ambazo watuhumiwa walizipokea na kumwachia huru mtuhumiwa huyo.

Kibwengo amesema kuwa watuhumiwa hao wanatarajia kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka kutokana na kwamba TAKUKURU imekamilisha uchunguzi wake,huku ikiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona kuna uonevu wa vitendo vya rushwa katika maeneo mbalimbali hapa jijini.

Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa
Taaisisi hiyo kutokana na kwamba suala la kupambana na rushwa ni la kila mmoja na si TAKUKURU pekee.

Kibwengo amewata wasiogope wala kusita kutoa taarifa TAKUKURU kipindi wanapoona kuna uonevu unatendeka mahali popote na kuongeza kuwa lengo ni kutaka kuona kila
mwananchi anapata uwelewa juu ya haki zake za msingi.

Kwa hatua nyingine amewaomba watendaji kuacha tabia ya kudanganya watu watoe rushwa ili wapatiwe ufumbuzi wa tatizo hilo bali amewaomba wawe waaminifu katika utendaji kazi na kuweza kuwasaidia wananchi kupata haki zao pale panapositahili.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com