Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kyaka
(hawapo pichani) ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John
Magufuli.
Baadhi ya wananchi wa Kyaka wakimsikiliza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani).
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa (kulia) akitoa maelekezo ya utekelezaji wa mradi wa maji Kyaka
kwa wataalam alipotembelea aneo linalopendekezwa kujengwa tenki la maji.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga.
Muonekano wa Mto Kagera kutokea eneo linalopendekezwa kujengwa tenki la maji Kyaka.
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa (wa pili kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa MWAUWASA,
Mhandisi Anthony Sanga mara baada ya kutembelea eneo linalotarajiwa
kujengwa tenki la maji.
****************
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Kyaka, Wilaya ya Misenyi Mkoani
Kagera kupata huduma ya majisafi na salama kutoka Mto Kagera ifikapo
Desemba, 2019.
Kauli hiyo aliitoa Julai 12,
2019 wakati wa ziara yake Wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
alilolitoa Julai 11, 2019.
Akiwa njiani akitokea Wilayani
Karagwe kuelekea Wilayani Chato, Rais Magufuli alisimama katika Mji
Mdogo wa Kyaka kusalimiana na wananchi na walimueleza kero ya muda mrefu
ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.
Rais Dkt. Magufuli alimuagiza
Waziri Mbarawa kwa njia ya simu mbele ya wananchi hao kufika eneo hilo
siku iliyofuata kuzungumza nao na kuhakikisha kero hiyo inatatuliwa na
ikifika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi mwaka huu wananchi hao wawe
wamepata huduma ya majisafi na salama.
Katika utekelezaji wa agizo
hilo, Waziri Mbarawa akiwa ameongozana na Watendaji na Wataalam kutoka
Mamlaka za Maji Mwanza (MWAUWASA) na Bukoba (BUWASA) alisisitiza kwamba
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria
kuwaondolea wananchi wake kero ya maji na aliwahakikishia wananchi wa
Kyaka kwamba kero ya maji inakwenda kuwa historia.
Profesa Mbarawa alisema
Mkandarasi mahiri atapewa jukumu hilo la kujenga mradi wa maji na
aliwasihi wananchi hao wa Kyaka kutakapojengwa chanzo cha maji kutoa
ushirikiano kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi ili ukamilike kwa
wakati na kwa kiwango.
“Tumesema sasa imetosha
wananchi kuhangaika, tunawahakikishia wananchi wote wa Kyaka kuwa
mtapata majisafi na salama kutoka Mto Kagera, tunajenga mradi mkubwa wa
maji ambao pia ni endelevu,” alisema Waziri Mbarawa.
Waziri Mbarawa aliamuagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga kushirikiana na
Mkurugenzi wa Maji Bukoba, Allen Marwa na wataalam wengine kutoka Wizara
ya Maji kusimamia na kuratibu haraka shughuli za awali za ujenzi wa
mradi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa MWAUWASA, Mhandisi Sanga alielezea walivyojipanga kwenye maandalizi ya awali ya ujenzi wa mradi.
Mhandisi Sanga alibainisha
kwamba shughuli za awali za utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na
kumpata Mkandarasi wa ujenzi zitakamilika ndani ya muda mfupi ili kazi
za ujenzi ziweze kukamilika katika muda ulioelekezwa na Rais Dkt.
Magufuli.
“Ili kukamilisha ujenzi wa
mradi katika kipindi kilichoagizwa na Mhe. Rais inatakiwa taratibu za
awali zifanyike kwa muda mfupi kadri iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na
kumpata mkandarasi atakaye jenga mradi,” aliongeza Mhandisi Sanga.
Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Kyaka, Bunazi na maeneo mengine ya Mutukula, Kakunyu na Bubale.
0 comments:
Post a Comment