METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 31, 2019

Waziri Biteko Awataka Watumishi Kutokuwa Kama Mafarisayo wa Biblia


Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya Mara baada ya kuwasili katika eneo lililozungushiwa kiwanda cha Chokaa katika kijiji cha Makere.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Makere alipofika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika suala la uchimbaji wa Madini ya chokaa.


Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa mwezi mmoja kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mamlaka ya Misitu (TFS) na Ofisi za Madini mkoani Kigoma kukaa na kuamua namna ya kuwafanya wananchi wa makere kuendeleza shughuli zao za uchimbaji wa chokaa zilizosimamishwa tangu mwaka 2006 na kuepuka kuwa mafarisayo kwa kuwafanya wananchi kufurahia rasilimali ya chokaa iliyopo katika eneo lao.

Biteko ametoa kauli hiyo tarehe 30 Julai, 2019 alipokuwa katika mkutano na wachimbaji wadogo na wananchi wa kijiji Makere kilichopo katika halmashauri ya Kasulu Mkoani Kigoma alipofika ili kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.

Aliendelea kuwataka watumishi hao kuepuka kuwa kama mafarisayo kama walivyotajwa katika Biblia na kubainisha kuwa mafariisayo walikuwa wakiwabebesha wengine mizigo mizito ambayo wao wenyewe hawakuweza kuibeba.

Biteko alizitaka mamlakahizo kuhakikisha kuwa zinaupitia mpango wa uchimbaji Usioadhiri Mazingira (EPP) uliwasilishwa serikalini na kuonesha kuwa na mapungufu na kurekebisha mapungufu hayo.

Aliendelea kusema, ni wajibu wa watumishi wa hao wa Halmashauri, madini pamoja na Mamlaka ya Misitu kuhakikisha wanarekebisha kasoro hizo ili wananchi haowaweze kuendelea na shughuli za uzalishaji na wachangie maendeleo yao na ya Taifa kupitia kodi watakazokuwa wakilipa.

“Wajibu wa kuwasaidia wananchi hawa ni wenu, hata mkisema hawaruhusiwai kuchimba mje na maelezo yanayojitosheleza na kuwaelekeza wananchi kwani wajibu wa kuwaelimisha ni wenu” alisisitiza.

Biteko alieleza mamlaka hizo kuwa kila mahali pana rasilimali ambazo mwenyezi Mungu ameziruhusu kuwepo ili kuwasaidia katika kuendesha maisha yao na mji wa Makere Mungu aliweka chokaa hivyo ni vyema wananchi wakatafutiwa namna bora ya kufanya uchimbaji huo bila ya kuathiri mazingira na si kuwasimamisha.

“Kama ilivyo dhahabu Geita, Almasi Shinyanga, Tanzanite Mirerani, asali Tabora, na utajiri mwingine mwingi kama unavyopatikana katika maeneo mengine, wananchi wa Makere nao wamepewa chokaa, sasa tuwasaidie ili watumie rasilimali hiyo kuboresha maisha yao” Biteko alisisitiza.

Wananchi hawa walianza uchimbaji toka mwaka 1978 mpaka uchimbaji huo ulivyositishwa mnamo mwaka 2006 wako katika sintofahamu, tutawapeleka wapi wananchi hawa? Biteko alihoji.

Aidha, aliwataka watumishi hao wa umma kuja na njia mbadala kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa chokaa na si kuwazuia wananchi kwa kutumia sababu ya kukosa nishati mbadala kwa ajili ya kuchomea chokaa hiyo isipokuwa wao wawasilishe mapendekeo yatakayowawezesha wananchi kuondokana na adha hiyo.

“Hakuna sheria inayozuia watu kuchimba, sheria inatoa utaratibu wa namna gani bora ya kuchimba, wapeni huo utaratibu waufuate ili waweze kuchimba na kubadilisha maisha yao, hiyo ndio rasilimali waliyopewa watu wa Makere, waacheni wachimbe” alisisitiza.

Kwa upande wake Meneja Misitu wa Wilaya ya Makere, Donald Kabigi alisema walikwisha kuwapa maelekezo wananchi hao ya kufuata ikiwa ni pamoja na kutoa matanuru ya kuchomea chokaa hiyo nje ya hifadhi yam situ wa Makere ili kuwawezesha wataalamu kusimamia shughuli hizo jambo ambalo bado hawajalifanyia kazi.

Akizungumzia suala la Mpango wa Hifadhi ya Mazingira (EPP) Donald alikiri kuwa ulikuwa na mapungufu na kukiri kuwa wamepewa mwezi mmoja ili kuweza kurekebisha mapungufu hayo yanayotokana na changamoto za uchimbaji.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Saimon Anange kwa upande wake alikiri kuwa kuna changamoto kwa watumishi wa serikali katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo na kumuhakikishia Waziri Biteko kuwa atalisimamia na kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanakuja na majibu ya namna ya kuwasaidia wananchi hao kama walivyoelekezwa.

Aidha, Kanali Anange, alimshukuru Waziri Biteko kwa kuchukua hatua ya kufika katika Wilaya yake na kusaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake.

Baadaye Biteko aliwatembelea wamiliki wa kiwanda cha chokaa cha Makere (MAKERE LIME) na kufurahishwa kwa namna wanavyofanya kazi zao ambapo wanathaminisha madini hayo na kuyaweka tayari kwa kuuzwa.

Biteko alilitaka kampuni hilo kujitangaza kupitia maonesho mbalimbali ili madini hayo yaweze kuuzwa nje ya Kigoma na kuwaletea faida kubwa jambo lililopokelewa kwa bashasha na wamiliki wa kiwanda hicho.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com