Vijana nchini wameaswa kuwa wazalendo Na
wabunifu ili waweze kufikia malengo yao na kuacha kuwa tegemezi huku
wakisubiri kuajiriwa na badala yake wajikite katika kujiajiri wenyewe.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Sehemu ya
Utumishi na Utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Veronica Ndavo
wakati wa kuwaaga wanafunzi wa kitivo cha Tiba wa Chuo Kikuu cha Dodoma
UDOM.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyoandaliwa na wanafunzi hao ambao ni wanachama wa CCM, Ndugu Veronica
amewaasa vijana hao ambao ni wataalamu wa afya, wafamasia, wauguzi na
maafisa wa mazingira na matibabu kuhakikisha wanatumia elimu waliyopata
katika kukitumikia Chama chao, jamii inayowazunguka pamoja na Serikali.
” Nawapongeza sana kwa kuhitimu niwasihi
mnapoelekea mtaani msibague kazi lakini pia hizo kazi zisishushe utu
wako, nendeni mtaani mkafanye kazi ili tumsaidie Rais wetu katika
kufikia uchumi wa viwanda.
” Niwapongeze pia kwa kukuza kipato cha
tawi lenu la Chama kutoka Shilingi Laki Moja hadi kufikia Laki Sita,
naahidi kuwapa ushirikiano na nitatoa mifuko ya Saruji yenye thamani ya
Shilingi Laki Tatu, pamoja na vitendea kazi vyenu vya Chama zikiwemo
Kompyuta ambayo nitaikabidhi hapa leo. Lengo letu ni kuona hamkwami
kwenye shughuli zenu za Chama,” amesema Veronica.
Aidha Veronica amekabidhi kiasi cha
Shilingi Laki mbili kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya CCM ya Kata ya
Ng’hong’hona ambayo kwa asilimia kubwa imekua ikitumiwa na wananchi hao
ambao ni wanachama wa Chama hicho.
” Niwatake pia mkawe msaada mkubwa wa
Chama chetu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja hivi karibuni,
Rais wetu Dk John Magufuli amefanya kazi kubwa za kimaendeleo zawadi
pekee tunayoweza kumpa ni ushindi wa kishindo wa CCM kwenye chaguzi
hizi. Nyie ni vijana kaonesheni thamani yenu na nguvu yenu ndani ya
Chama kwa kukisaidia kushinda uchaguzi huu,” amesema Veronica.
Nae Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini,
Diana Madukwa amemshukuru Bi Veronica kwa kujitoa kwake katika
kuwachangia vijana hao na kuahidi kuendelea kuwalea wanafunzi wanaobakia
katika maadili ya kiuongozi na yenye utumishi ndani ya Chama.
” CCM Wilaya tutaendelea kuwa bega kwa
bega na vijana wanaohitimu na wale wanaobaki, tutawalea kichama ili
kutimiza ndoto zenu za kuwa viongozi wakubwa kisiasa na kiserikali
lakini zaidi kuwa wanachama waaminifu na wazalendo kwa Nchi yao,”
amesema Diana.
0 comments:
Post a Comment