Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu Aakizungumza na makuruta wa
kikosi cha 825KJ katika kambi ya Mtabila wilayani Kasulu mkoani Kigoma,
alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini
katika wilaya hiyo.
Makuruta wa kikosi cha 825KJ kambi ya Mtabila wilayani Kasulu mkoani
Kigoma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, hayupo
pichani, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme
vijijini katika wilaya hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu,( katikati) akimkabidhi kifaa cha
umeme tayari( UMETA) mama mwenye ulemavu,Merania Katekwa, mkazi
wa Kijiji cha Nyankoronko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, ambaye hana
uwezo wa kulipia gharama za kuunganisha umeme licha ya nyumba yake
kukidhi viwango na kupitiwa na mradi wa usambazaji umeme vijijini.
Akina mama wa kijiji cha Shunga, Kasulu mkoani Kigoma, wakifurahi na
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alipowaeleza kuwa umeme katika
kijiji hicho utafika hivi karibu na tayari mkandarasi anaendelea na kazi ya
kusimika nguzo.
**************
Na Zuena Msuya, Kigoma
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewashauri wakandarasi nchini
kuwatumia vijana wanaomaliza mafunzo katika jeshi la kujenga taifa wenye
taaluma na ujuzi mbalimbali ikiwemo sekta ya Nishati ya Umeme.
Mgalu alisema idadi kubwa ya vijana wanaohitimu mafunzo ya JKT
wanakuwa na nidhamu, pamoja na uzalendo katika kutekeleza majukumu
yao kwa maslahi ya Taifa.
Naibu Waziri alitoa ushauri huo alipokuwa akikagua maendeleo ya
usambazaji wa Umeme vijijini katika kikosi Jeshi la Kujenga Taifa cha
825KJ Katika Kambi ya Mtabila, wilayani Kasulu mkoani Kigoma na
kuzungumza na uongozi wa kituo hicho pamoja na Makuruta, Julai
11,2019.
Aidha walishauri vijana wanaopata mafunzo ya jeshi kujifunza taaluma ya
umeme wanapokuwa vyuoni ili kuwepo na mafundi mchundo wengi pale
watakapohitajika kutumiwa na wakandarasi katika kujenga miradi ya
umeme.
Aliongeza kuwa endapo kutakuwa na vijana wengi wzalendo katika
taaluma hiyo, itasaidia kuondoa changamoto ya vishoka mitaani na watu
wasiowaaminifu katika kutekeleza miradi ya umeme na mafundi mchundo
katika kuwatanda nyaya kwenye nyumba za wananchi.
"Vijana wanaopitia mafunzo ya jeshi wengi huwa waadilifu na wazalendo
kwa miradi inayotekelezwa katika nchi yao, hivyo nawashauri wakandarasi
wote nchini kuwatumia vijana hao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya maendeleo hasa ile yenye gharama kubwa na inayotumia fedha nyingi,
kwa maslahi yao na nchi kwa ujumla", alisisitiza Mgalu.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kikosi cha 825 KJ katika Kambi ya
Mtabila, Meja Peter Lyanga alimueleza Naibu Waziri Mgalu kuwa katika
hiyo vijana wengi wanahitimu wakiwa na taaluma mbalimbali wakiwa na
nidhamu ya hali ya juu hivyo amewatoa hofu wakandarasi juu wa vijana
hao.
Aidha aliomba kuharakishwa kwa utekelezaji wa mradi wa umeme katika
eneo hilo ili kambi hiyo iweze kupata huduma hiyo,ambayo itawasaidia
vijana kuongeza ujuzi zaidi katika mafunzo yao yanayoendana na
teknolojia ya kisasa zaidi.
Katika hatua nyingine Mgalu aliwasha Umeme katika vijiji vya Wilaya za
Kasulu na Buhigwe mkoani Kigoma na kuwataka wananchi kutumia
Umeme huo kujiletea maendeleo.
Katika Wilaya ya Kasulu, Mgalu aliwasha Umeme katika Zahanati ya
Ruhita, Shule ya Sekondari ya Kasange pamoja na kijiji cha Ruhita.
Vilevile alizungumza na wakazi wa vijiji vya Shunga, Ruhita na Kasange
ambapo pamoja na mambo mengine alimtaka mkandarasi anayetekeleza
mradi wa usambazaji Umeme katika vijiji hivyo kuongeza kasi zaidi kwani
wananchi wamekuwawakiusubiri kwa muda mrefu.
Katika ziara hiyo pia, Mgalu alikagua kazi ya usambazaji wa umeme kijiji
cha Nyankoronko wilayani Buhigwe na kuwasha umeme katika jengo la
halmashauri ya Wilaya hiyo na kuzungumza na wananchi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wao, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Samson Anange na
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayalina waliwataka wananchi wa
wilaya hizo kutunza miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao
wakati wakiendelea kusubiri hadi pale watakapowafikiwa na mradi huo
katika nyumba zao.
Pia amewataka kutoa ushirikiano wa nguvu kazi hasa kwa vijana pale
ambapo wakandarasi watakuwa wakiwahitaji vijana hao kwa kuwa
watapata ajira za muda mfupi na kukidhi mahitaji yao.
Sambasamba na hilo waliwasisitiza wakazi wa wilaya hizo kuwa wasikubali
kulipa gharama za kuunganishiwa umeme kwa zaidi ya shilingi 27,000 wala
kuuziwa vifaa vya umeme kama vile nguzo pamoja na LUKU.
0 comments:
Post a Comment