Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
pamba wakati alipotembelea ghala la Chama cha Msingi cha cha Ushirika
cha kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga akiwa katika ziara ya siku moja
wilayani humo ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao hilo, Julai 15,
2019.
Waziri Mkuu, Kasism Majaliwa akipata
maelezo kutoka kwa Katibu na Meneja wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha
kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga kuhusu pamba iliyokusanywa na
wakulima kwenye ghala la ushirika huo, Julai 15, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
mikokoteni iliyosheheni pamba wakati alipotembelea ghala la Chama cha
Msingi cha Ushirika cha kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga alikofanya
ziara ya siku moja ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao hilo, Julai 15,
2019. Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wa pili kushoto ni
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
mkokoteni uliyosheheni pamba wakati alipotembelea ghala la Chama cha
Msingi cha Ushirika cha kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga alikofanya
ziara ya siku moja ya kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao hilo, Julai 15,
2019. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.
Wananchi wa kijiji cha Mwabakima wilayani
Igunga wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia
akiwa katika ziara ya siku moja wilayani humo ya kukagua mwenendo wa
ununuzi wa zao la pamba, Julai 15, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia
mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga akiwa
katika ziara ya siku moja wilayani humo ya kukagua mwenendo wa ununuzi
wa zao la pamba, Julai 15, 2019. Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet
Hasunga na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………..
*Waziri Mkuu asema hadi Julai 30 wakulima wote watakuwa wamelipwa
Na Mwandishi Wetu
ZAO la pamba ni miongoni mwa mazao makuu
ya biashara hapa nchini yakiwemo ya korosho, chai, tumbaku, katani na
chikichi ambayo yamekuwa yakitegemewa katika kuinua uchumi wa wakulima
na Taifa kwa ujumla.
Hivi karibuni kumetokea hali ya
sintofahamu kuhusiana na suala ununuzi wa zao hilo baada ya kutangazwa
kwa bei elekezi ambayo ni sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote
inayozalisha zao hilo.
Bei elekezi ya pamba kwa msimu huu ilitangazwa Aprili 30, 2019 mkoani
Shinyanga na kwamba bei hiyo ilitakiwa ianze kutumika kuanzia Mei 2,
2019. Hata hivyo ununuzi wa zao hilo ulianza kwa suasua jambo ambalo
Serikali haikuridhishwa nalo.
Jumapili ya Julai 14, mwaka huu ndipo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliamua kuitisha kikao kilichojumuisha wakuu
wa mikoa 11 inayolima pamba, wanunuzi wa zao hilo, taasisi mbalimbali
za kifedha pamoja na Gavana wa Benki Kuu.
Kikao hicho kilichoitishwa na Waziri Mkuu
na kufanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi kilikuwa na
lengo la kutafakari mwenendo wa zao la pamba ambalo ununuzi wake
unaendelea lakini kwa kasi ndogo.
Waziri Mkuu baada ya kusikiliza
changamoto za wanunuzi ambao wengi wao waliomba Serikali iwadhamini
katika taasisi mbalimbali za fedha walizoomba mikopo kwa ajili ya
kununua zao hilo kwa kuwa ilikuwa imekwama. Serikali iliwakubalia.
“Sasa tumefikia muafaka wa jambo hili
kibali kitatoka na wote watakaopata dhamana ya mikopo hakikisheni fedha
hizo zinaenda kutumia kwa ajili ya ununuzi wa pamba kama ilivyokusudiwa
na si vininevyo.”
Hivyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wa
mikoa na wilaya katika maeneo yote yanayolima pamba wawasimamie ipasavyo
wanunuzi wote ili kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinakwenda
kutumika kwa ajili ya kununulia pamba.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi
Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma aliishukuru Serikali kwa
kukubali kuwadhamini pamoja na Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa
kuhusu suala la ununuzi wa zao hilo.
Waziri Mkuu, baada ya kufanya kikao na wadau wa pamba wakiwemo na
wanunuzi ambao walikubali kwenda kununua pamba iliyoko kwa wakulima,
Julai 15, 2019 alifanya ziara katika wilaya ya Igunga kwa lengo la
kukagua mwenendo wa ununuzi wa zao la pamba.
Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Mkuu
alianza kwa kukagua ghala la ununuzi wa pamba la AMCOS ya Mbutu na kisha
alikwenda katika kijiji cha Mwabakina na kukagua ghala la kununulia
pamba la Mwabakima.
Baada ya kukagua maghala hayo Waziri Mkuu
alizungumza na wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao ni wakulima wa
pamba ambapo aliwahakikishia kwamba hadi kufikia tarehe 30 mwezi Julai
mwaka huu pamba yote iliyoko katika mikoa mbalimbali nchini itakuwa
imeshanunuliwa na wakulima wote kulipwa fedha zao.
Alisema Serikali imeamua kuingilia kati
suala la ununuzi wa zao la pamba kutokana na kusuasua kwa soko lake kwa
kutoa dhamana ili kuwawezesha wanunuzi kukopeshwa fedha na benki
mbalimbali kwa ajili ya kununulia pamba kutoka kwa wakulima.
“Tunatambua adha mliyoipata tangu kuanza
kwa msimu wa mwaka huu na hayo ni mapito tu. Nawasihi muwe na amani
kwani Serikali yenu inafuatilia suala hili na Rais Dkt. John Magufuli
anataka kuona pamba yote inatoka kwa wakulima ili kuwawezesha kupata
tija.”
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwasihi wakulima
wa zao hilo la pamba na wakulima wa mazao mengine nchini wahakikishe
mara baada ya kuuza mazao yao wanatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya
kununulia pembejeo watakazozitumia katika msimu ujao.
Wananchi kwa upande wao waliishukuru
Serikali kwa hatua yake ya kuingilia kati suala la ununuzi wa zao la
pamba pamoja na malipo kwa wakulima ambao tayari pamba yao
walishaipeleka katika AMCOS zao.
Kwa upande wake, Waziri
wa Kilimo Japhet Hasunga alisema Serikali itahakikisha inaendelea
kutafuta masoko ya mazao hayo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha
wakulima kuwa na uhakika wa masoko kwa mazao yao na hivyo kujiongezea
tija.
Pia, Waziri huyo alisema mbali na
kutafuta masoko, Serikali imedhamiria kufufua viwanda mbalimbali vya
nguo hapa nchini ili kuwawezesha wakulima wa zao la pamba kuwa na soko
la uhakika. “Kuhusu suala la maghala tunatambua tatizo hilo na
tutahakikisha tunayaboresha ili pamba iweze kuhifadhiwa katika mazingira
bora”.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya
viuatilifu, Waziri Hasunga alisema Serikali itahakikisha vinapatikana
kwa kuzingatia eneo husika ili kuweza kudhibiti wadudu waharibufu.
0 comments:
Post a Comment