Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipoweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa magahala na vihenge vya kisasa katika eneo la Kizota mjini Dodoma Aprili 21, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaongoza viongozi kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa kwenye eneo la Kizota mjini Dodoma Aprili 21, 2018. Kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa, Balozi wa Poland nchini, Mhe. Krzystof Buzalski na kulia Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na balozi wa Poland nchini, Mhe Krzysztof Buzalski wakati alipoweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa katika eneo la Kizota mjini Dodoma Aprili 21, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Spika wa Bunge, Mhe.Job Ndugai akizungumza Katika sherehe ya uwekaji jiwe la msingi la maghala na vihenge vya kisasa kwenye eneo la Kizota mjini Dodoma, Aprili 21, 2018. Mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya wageni waalikwa wakiwemo wabunge na Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati aliopozungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa magahala na vihenge vya kisasa kwenye eneo la Kizota mjini Dodoma Aprili 21, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki kwenye sherehe ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa kwenye eneo la Kizota mjini Dodoma, Aprili 21, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bibi Vumilia Zikankuba akitoa taarifa ya mradi huo unatekelezwa katika maeneo manane ya Kanda za Wakala huo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeimarika na kufikia tani milioni 15.9 kwa msimu wa mwaka 2016/2017 na 2017/2018 sawa na kuwa na ziada ya tani milioni 2.6.
Pia Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa kuiwezesha Wizara ya Kilimo kuongeza uwezo wa hifadhi ya Taifa ya chakula kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Aprili 21, 2018) wakati akiweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula, Kizota mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema mkakati huo utahusisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa nje ya nchi na hivyo kutoa fursa za ajira na kuwaongezea kipato wananchi.
Amesema Serikali imefungua mipaka na inaendelea na jitihada za kutafuta masoko ya nje pamoja na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.
Pia Waziri Mkuu amewasihi wananchi watumia fursa za kiuchumi kwenye maeneo ambayo mradi huo utatekelezwa kwa lengo la kuboresha na kuinua hali zao za maisha, hivyo watakuwa na uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huo mkubwa na baada ya kukamilika utakuwa na faida kubwa kwa Taifa, hivyo amewataka viongozi wa NFRAwahakikishe kwamba hakuna mahindi yatayoharibika katika maghala yao.
”Mikakati ya Serikali ni kuhakikisha NFRA inakuwa na uwezo wa kuhifadhi akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya dharula lakini pia kuweka mazingira rafiki ya kuwezesha wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya nchi bila vikwazo”.
Hata hivyp, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango na Wakuu wa Mikoa ambayo mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe wanatimiza wajibu wao ili mradi ukamilike kwa wakati.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bibi Vumilia Zikankuba alisema mradi huo unatekelezwa katika maeneo manane ya Kanda za Wakala huo ambayo ni Dodoma Mjini (Dodoma), Mpanda (Katavi), Songea (Ruvuma), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga Mjini (Shinyanga), na Babati (Manyara).
Bibi Vumilia alisema katika Kanda ya Dodoma wanajenga vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na kufanya kanda hiyo kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 59,000 kutoka uwezo wa sasa wa tani 39,000.
Bi Vumilia aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.
“Utekelezaji wa mikataba kati ya NFRA na wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo muda wa utekelezaji ni miezi 18 tangu tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji wa mikataba ya wakandarasi, hivyo kabla ya 2020 utakuwa umekamilika”. Alikaririwa Bi Vumilia
Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai , Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama.
Wengine ni Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi na Ajira, Anthon Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Balozi Krzysztof Buzalski.
0 comments:
Post a Comment