Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe Suleiman Jafo,akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ziara maalum ya kukagua
ujenzi wa Hospital ya Uhuru inayojengwa kwa maelekezo ya Mhe Rais Dk
John Magufuli katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), Daniel Mwakasungura,akitoa taarifa kwa waandishi wa
habari juu ya mpango wa ujenzi wa Hospitali hiyo ya Uhuru iliyopo
Chamwino,Mkoani Dodoma.
Mhandisi wa Suma JKT, Luteni Kanali
Onesmo Njau,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ambao
wamepewa jukumu la kujenga Hospitali hiyo.
Sehemu ya eneo ambapo ujenzi wa Hospitali ya Uhuru .
……………………….
Na.Alex Sonna,Chamwino
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe Suleiman Jafo amefanya ziara
maalum ya kukagua ujenzi wa Hospital ya Uhuru inayojengwa kwa maelekezo
ya Mhe Rais Dk John Magufuli katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Hospitali hiyo inajengwa baada ya Rais
Magufuli kuelekeza kufanya hivyo katika sherehe za Uhuru mwaka 2018
ambapo alifuta sherehe hizo na kupeleka Fedha zilizokuwa zimetingwa kwa
ajili ya sherehe hizo kujenga Hospitali mkoani Dodoma.
Mhe.Jafo amesema kuwa anashukuru siku ya
leo kwa kufanya ziara hii maalumu ya kukagua ujenzi wa Hospitali hii
ambayo ni malekezo kutoka kwa Mhe Rais, lakini pia hata hivyo baada ya
gawio la Serikali kutoka Kampuni ya Airtel Mhe Rais alielekeza Fedha
hizo kuletwa kwenye mradi wa ujenzi wa Hospitali hii ya Uhuru.
” Na kama mnavyokumbuka nilikuja siku za
nyuma Juni 19 kukagua lakini sikuridhishwa baada ya kukuta ujenzi
haujaanza ndio maana nimetoa maelekezo kwamba ujenzi uanze mara moja kwa
kutumia vikosi vya Jeshi ili kutimiza azma ya Mhe Rais katika kutoa
huduma za Afya kwa wananchi, na tayari wenzetu wa Suma JKT wameshaanza
kazi hii,” amesema Mhe Jafo.
Amesema tayari eneo lote la Ekari 40
limeshasafishwa ikiwemo kujenga uzio pamoja na ofisi kuleta vifaa vya
ujenzi huku pia akieleza kwamba TBA wataendelea kusimamia suala la
ramani na kutoa ushauri wa mradi huo na wataendelea kutumia utaratibu wa
‘false acount’ kutokana na kuwapatia mafanikio katika kufanikisha kazi
za Serikali za Mitaa.
” Kwa kweli leo nimeridhishwa na hatua ya
awali ambayo tumefikia katika ujenzi wa Hospitali hii, na niwaombe
wataalamu wangu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na tunapotoa maagizo basi
wayatekeleze kwa wakati, lakini ni matarijio yetu hadi kufikia Januari,
2020 tutakua tumeshamaliza ujenzi huu,” amesema Mhe Jafo.
Kwa upande wake Mhandisi kutoka Wakala wa
Majengo Tanzania TBA, Daniel Mwakasungura amesema Hospital hiyo ya
Uhuru itakuwa ni ya Ngazi ya Wilaya ambapo kwa agizo la Mhe Rais awamu
ya kwanza ni kujenga majengo ya wagonjwa wa nje ikiwemo huduma za
maabara na Kliniki ya Mama na Mtoto.
” Hela iliyotengwa ambayo Tumeingia
mkataba na Suma JKT ni Shilingi Bilioni 3 ambazo zitajenga hivyo
nilivyovitaja na tunatarajia kukamilisha mradi huu baada ya miezi sita
kama ambavyo tuliekezwa,” amesema Mwakasungura.
Nae Mhandisi wa Suma JKT, Luteni Kanali
Onesmo Njau amesema walikabidhiwa jukumu la ujenzi huo Juni 19 mwaka huu
na tayari washatekeleza maelekezo kutoka kwa Mhe Jafo ikiwemo kuandaa
ofisi, sehemu za kuishi kwa watendaji na muda sio mrefu wataanza ujenzi
ili kukamilisha mapema kama ilivyoelekezwa.
0 comments:
Post a Comment