Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimina
na Bibi Agnes Venance (kulia) na BW. Paskazi Mashimo (katikati) ambao
alisoma nao katika Shule ya Msingi ya Mnacho wilayani Rungwa kwenye
miaka ya 70 . Alisalimiana na wanafunzi wenzake hao baada ya kukagua
ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia iliyopo Mnacho
wilayani Ruangwa, Juni 2, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe
Mary wakisalimina na Watawa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mnacho baada
ya Waziri Mkuu, kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya
Lucas Malia wilayani Ruangwa, Juni 2, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza
na Paroko wa Parokia ya Mnacho, Padri Gerold Nyagau (wa pili kushoto)
wakati alipokagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas
Malia iliyopo Mnacho wilayani Ruangwa, Juni 2, 2019. Kushoto ni Mkewe
Mary na kulia ni Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu David Mwakalobo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia iliyopo Mnacho
wilayani Ruangwa, Juni 2, 2019. Kushoto ni Mkewe Mary na kulia ni Mkuu
wa Shule hiyo, Mwalimu David Mwakalobo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Paroko
wa Parokia ya Mnacho wilayani Ruangwa, Padri Gerold Nyagau wakimsikiliza
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa wakati alipozungumza baada ya
Ibada ya Jumapili kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mnacho, Juni 2,
2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………
*Ni baada ya kutoa sehemu ya eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa shule
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameushukuru
uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi kwa kutoa sehemu ya eneo lake
na baadhi ya majengo kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Jimbo Katoliki la Lindi limetoa eneo hilo
lilipo katika Parokia ya Mnacho wilayani Ruangwa ambalo awali ilikuwa
shule ya msingi ya Mnacho sasa imebadilishwa na kuwa sekondari.
Waziri Mkuu ametoa shukurani hizo leo
(Jumapili, Juni 2, 2019) alipokwenda kwenye kanisa Katoliki la Theresia
wa Mtoto Yesu, Parokia ya Mnacho kuwasalimia waumini.
Amesema lengo la kuibadilisha shule hiyo
kuwa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia ni kuwawezesha
watoto wa kike wa Wilaya hiyo kusoma katika mazingira mazuri.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na Mkewe
Mary amesema shule hiyo ya bweni itawapunguzia vishawishi watoto wa
kike, hivyo kuwawezesha kutimiza malengo yao.
Awali, uongozi wa
Parokia hiyo uliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuboresha huduma
za jamii zikiwemo za afya, elimu pamoja na miundombinu katika wilaya
hiyo.
Naye, Mkuu wa wilaya ya
Ruangwa, Hashim Mgandilwa amewaomba viongozi wa dini washikamane na
wahakikishe wanatatua changamoto ya mmomonyoko wa maadili.
Amesema changamoto ya mmomonyoko wa
maadiji katika jamii hususani kwa vijana ni kubwa, hivyo ni jukumu lao
kuhakikisha kwamba wanawarejesha kwenye maadili bora.
Kadhalika, Waziri Mkuu
amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia na
amesema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Shughuli zinazoendelea katika shule hiyo
ni pamoja na ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa, maabara na nyumba
nne za walimu ambazo tayari ujenzi wake umekamilika.
0 comments:
Post a Comment