MKUU wa Wilaya ya Ikungi Mh
Miraji Mtaturu ameshiriki harambee na kuchangia shilingi milioni 4.6 kwa ajili
ya ununuzi wa vifaa vya kwaya ya New Jerusalem ya Kanisa FPCT
Mbughantigha-Matongo lililopo wilayani humo.
Aidha kupitia harambee hiyo
amewezesha kupatikana jumla ya shilingi milioni 7.4 DC
Akizungumza katika harambee
hiyo mh Mtaturu amewaomba waumini kuendelea kuilinda amani ya nchi kwa kuwa
bila ya kuwepo kwa amani jambo lolote la kimaendeleo ikiwemo kuabudu halitaweza
kufanyika.
“Tumejumuika hapa kwa sababu
tuna amani,bila ya kuwa na amani tusingekuwepo hapa na kufanikisha jambo hili
la Mungu,niwashukuru sana Kanisa kwa kunialika kwenye jambo hili muhimu,kwani
vyombo hivi tunavyotafuta leo vitaenda kupeleka neno la Mungu kwa waumini na
wao wakimjua Mungu watakuwa Raia wema na hivyo watadumisha amani,
“Serikali yetu ya awamu ya
tano chini ya Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt John Pombe Magufuli inatambua na
kuthamini sana mchango wa Taasisi za Dini kwenye huduma mbalimbali za kijamii
sambamba na kudumisha amani,na imeendelea kuboresha huduma za kijamii kama
Elimu,Afya,na Miundombinu ili kuharakisha maendeleo ya nchi yetu”alisema mh
Mtaturu.
Amesema ushahidi wa hilo ni
katika wilaya hiyo ambapo kwenye kitongoji cha Mbughantigha mwaka jana serikali
imepeleka shilingi milioni 66.5 ili kujenga madarasa mawili na ofisi ya
mwalimu,matundu manne ya vyoo kwa ajili ya shule shikizi ambayo imeondoa tatizo
la watoto wadogo waliokuwa wanatembea km 14 kufuata shule ya msingi Matongo.
“Mbali na hilo serikali yetu
pia imeleta shilingi milioni 187.5 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma ya
madarasa14 ya shule 7 za sekondari na shilingi milioni 127 kwa ajili ya
kujenga vyumba vya madarasa ya shule za msingi pamoja na utengenezaji wa madawati,na
kila mwezi wilaya tunapokea shilingi milioni 103 kupitia mpango wa elimu bila
malipo maarufu kama Elimu Bure,”aliongeza mh Mtaturu.
Amewapongeza wananchi kwa
kuanzisha ujenzi wa madarasa mengine mawili na ofisi ambayo yamefikia
usawa wa madirisha na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono
ili watimize dhamira ya kujenga madarasa ya kutosha na kufungua shule mpya ya
msingi Mbughantigha.
Mchungaji kiongozi wa kanisa
hilo John Matheo amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa upendo wake wa kukubali kuja
kushirikiana nao na kusema wanabarikiwa sana kuwa na viongozi wa serikali
wanaowajali watu wao.
Akisoma risala ya kwaya
Mwalimu Mary Lengalenga amesema kwaya hiyo ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na
wanakwaya 6 na inahitaji shilingi milioni 13 ili kukabiliana na upungufu
wa vyombo vya uinjilishaji kupitia nyimbo.
Mh Mtaturu akiongozana na
viongozi wa Kijiji,Kata na Tarafa ya Ikungi wametumia shughuli hiyo pia
kukagua ujenzi wa shule ili kuona kazi zinazoendelea.
"Ikungi Yetu Sote
Tuijenge Pamoja"
0 comments:
Post a Comment