Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
(kaundasuti nyeusi) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh.
Julieth Binyura pamoja na kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa na
wataalamu wengine wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya
Kalambo.
Jengo la Maabara la Hospitali ya Wilaya ya Kalambo likiwa katika hatua ya Kenzi tayari kwaajili ya kuezekwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
(kaundasuti nyeusi) akiongozana na wataalamu kutoka ofisi ya mkuu wa
Mkoa wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo.
………………………
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangapo
amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Kalambo pamoja na kamati yake ya ulinzi na
usalama ya Wilaya kuwasaka na kuwatia nguvuni wananchi wanaosadikiwa
kuhujumu miundombinu ya maji katika Kijiji cha Kisongamile ambacho kipo
jirani na ujenzi unaoendelea wa hospitali ya wilaya ya kalambo hali
inayopelekea kurudisha nyuma kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Amesema kuwa hospitali hiyo ni ya kwao na
kwamba wao ndio wa kwanza kufaidika na ujenzi wa hospitali hiyo pindi
itakapokamilika, hivyo amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha
analimaliza tatizo hilo ndani ya muda mfupi ili kuendana na ratiba ya
umaliziaji wa ujenzi wa hospitali hiyo.
“Nimeona hii changamoto ya maji pamoja na
kwamba wanachimba kisima, lakini kile Kijiji pale ambacho kinakwamisha
kinahujumu miundombinu ya maji Mhe. DC pamoja na kamati ya usalama
muende pale, pamoja na mwenyekiti wa halmashauri, mkazungumze na kile
Kijiji, lakini pia kama kuna watu ambao wanadhaniwa wanahujumu kwa
makusudi miundombinu, haiwezekani Kijiji kizima kikawa kinahujumu
miundombinu, mchukue hatu ya kuwakamata hao wote wanaohujumu miundombinu
ya maji,” Alisisitiza.
Aidha, alieleza kutoridhishwa na kasi ya
ujenzi wa hoapitali hiyo ambapo mpaka tarehe 8.6.2019 bado wapo katika
hatua ya kuweka kenchi na huku hawajaanza kuweka plasta wala kununua
vifaa vingine kama milango, madirisha, vigae na mabomba na hivyo kumtaka
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kuhakikisha wananunua
vifaa hivyo mapema ili inapofikia hatua ya kuvipachika vifaa hivyo
kusiwepo na usumbufu.
Halikadhalika amewataka mafundi
wanaosimamia majengo ya hospitali hiyo kuhakikisha wanapiga plasta
majengo yote na kutahadharisha kuwa fundi yeyote atakayepitisha muda
wake bila ya kumaliza jengo itambidi fundi huyo kuilipa serikali na
kusisitiza kuwa serikali haitaongeza hata siku moja katika kuhakikisha
majengo hayo yanakamilika.
Ameyasema hayo alipotembelea eneo la
ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo inayotakiwa kukamilika ifikapo
tarehe 30.6.2019 akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa
pamoja na wataalamu kutoka katika ofisi yake.
Awali akielezea changamoto ya kusuasua
kwa upatikanaji wa maji katika eneo hilo la ujenzi Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Msongela Palela alisema kuwa miongoni
mwa changamoto kubwa ni uhujumu wa miundombinu ya maji inayoelekea
kwenye ujenzi wa hospitali hiyo unaofanywa na wananchi wa Kijiji cha
Kisongamile huku sababu kubwa ya uhujumu huo ni Kijiji hicho kukosa
umeme.
“Changamoto nyingine ni ya hawa wenzetu
wa Kijiji cha Kisongamile, ambao wao wanasema kwamba walipaswa kuwa
wamepata umeme ambao mpaka sasa hawana umeme, kwahiyo kwasababu hiyo hii
miundombinu ya maji wataendelea kuihujumu mpaka pale watakapokuwa
wamepatiwa umeme, tunaendelea kuwaelimisha na kukaa nao kuwashauri
kwamba wanachofanya ni hujuma kwa serikali yao lakini nimshukuru mkuu wa
Wilaya ameshachukua hatua za awali kwamba wanaohujumu watambuliwe na
kuchukua hatua,” Alisema
Pia, alisema kuwaendapo wananchi hao
hawatadhibitiwa huenda wakati zitakapoanza opereshi za hospitali
chnagamoto hiyo ikajitokeza hivyo ili kuhakikisha kwamba tahadhari
inachukuliwa na kuwa hospitali inakuwa na maji wakati wote ndio maana
tunakwenda kwenye wazo mbadala la kuchimba kisima.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Wilaya ya
Kalambo Dkt. Allen Kalekwa wakti akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa
hospitali hiyo alisema kuwa baadhi ya vifaa kwaajili ya umeme, bati na
mbao za kenchi zimeshanunuliwa na vingine vipo njiani na kuwa hadi
kufukia hatua hiyo tayari halmashauri imeshatumia shilingi milioni 940
na kubakiwa na shilingi milioni 560 ambazo ni kwaajili ya kununua vifaa
kama, marumaru, aluminian, gypsum na fedha ya mafundi na kisha kueleza
changamoto ya maji.
“changamoto kubwa tuliyonayo kwa sasa ni
tatizo la maji, tulishafunga mfumo wa maji mpaka hapa yalikuwa yanakuja
lakini bahati mbaya kuna baadhi ya sehemu wanakata mabomba ya maji,
lakini hatua za awali mpaka sasa hivi tumeshanunua madumu matatu ya lita
15,000 ya kuhifadhia maji na wenzetu wa ujenzi wa barabra wanatusaidia
kutujazia maji lakini pia tunatarajia kuchimba kisima kwaajili ya
utatuzi wa muda mrefu,” Alisema.
0 comments:
Post a Comment