**********************************************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amewataka waislamu wote nchini watumie siku kuu ya Eid el Fitr kwa
kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.
“Leo ni siku kubwa na muhimu
waislamu wanahitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na
kusherehekea siku kuu ya Eid El Fitr, hivyo tuendeleze matendo mema.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumatano, Juni 5, 2019) wakati aliposhiriki swala ya Eid El Fitr katika
msikiti wa Anwar uliopo Msasani jinini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema wakati huu ni
mzuri kwa kuimarisha mshikamano miongoni mwenu na madhehebu mengine,
hivyo hakikisheni mnayaendeleza mambo mema yote.
“Tumeona utulivu uliojitokeza
katika mwezi mtukufu, na jambo hili limesisitizwa na viongozi wa dini.
Tuendelee kuwa wamoja, tuimarishe mshikamano na tuvumiliane.”
Pia, Waziri Mkuu amewakumbusha
wazazi na walezi kuwaongoza watoto kwa kuwapa mafundisho ya dini
yatakayowawezesha kumjua Mwenyezi Mungu na kuwa raia wema.
Awali, Imamu wa msikiti huo,
Sheikh Mhina alisema waislamu wanatakiwa kuitumia siku ya leo kwa
kuhamasisha Amani pamoja na kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo.
Pia amewasisitiza wayaendeleze
mema yote waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani
ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu na kuwajali wazazi wao.
0 comments:
Post a Comment